Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Musa Godfrey Mbuga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii uliyonipatia. Nianze kwa kumshukukru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Nchi kwa kunipatia nafasi hii, lakini hata kwa kukubali niwe sehemu ya hili Bunge la Kumi na Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, na pia ninampongeza kwa kura nyingi alizopata. Ninamshukuru kwa sababu ya kuidhinisha kuteua jina langu, na baada ya hapo kuingia kwenye mchakato na Mungu akanisaidia nikashinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninawapongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Hassan Mwinyi; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ninampongeza hata Spika pamoja na Naibu Spika kwa kupata ridhaa ya kuwa sehemu ya uongozi wa Bunge hili. Ninawapongeza pia Mawaziri mbalimbali hususan ni Mawaziri ambao wamewasilisha Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa. Vilevile, ninawapongeza Wabunge kwa ujumla kwa kuaminiwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kueleza yale ambayo nimejifunza baada ya kusoma huu Mpango. Wakati ninausoma nimeona kwa sehemu kubwa umejibu haja za wananchi wetu. Umejibu mategemeo na matarajio ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaangalia jinsi ambavyo Mpango wa Maendeleo umeandaliwa, ni vipaumbele gani ambavyo vimezingatiwa? Nikiangalia vipaumbele ambavyo vimezingatiwa kwenye mpango huu wa maendeleo na malengo ambayo yamewekwa, ninaona moja, Mpango umeeleza kwamba lengo ni kuimarisha uchumi imara; pia, kuimarisha uchumi jumuishi na kuongeza ushindani katika uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninaangalia hivi vipaumbele vimeandaliwa kwa kuzingatia nini, napo Mpango ukawa umejibu kwamba vipaumbele vimeandaliwa kwa kuzingatia namna ambavyo tumetekeleza ule Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano. Pia, umeandaliwa kwa kuzingatia mabadiliko ya uchumi na mabadiliko ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita zaidi kwenye sekta ya kilimo na kwenye sekta ya mifugo. Mpango wetu umeeleza namna ambavyo utatekelezwa na ukawa umeeleza pia risk ambazo zinaweza zikajitokeza na namna ambavyo zinaweza kuwa mitigated. Umeeleza sehemu ya tathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana waandaaji pamoja na Tume ya Mipango kwa sababu wameweka hata ile Tume ya Mipango ambayo imehusika kuandaa hii kuwa sehemu ya tathmini. Ingeweza tu kuandaa, halafu ikakaa pembeni, lakini kwa kuwa inakuwa ni sehemu ya kufanya tathmini ya kile ambacho tutaenda kutekeleza, inatupa matumaini kwamba tutaenda kukiishi kile ambacho tumekiandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ile ya risk imenifurahisha zaidi kwa sababu kupanga ni kitu kimoja, lakini ikiwa hautabaini risk ambazo zinaweza kujitokeza njiani unaweza kuwa na mipango mingi na isitekelezeke. Ndiyo maana wengi tunaanzisha vitu, lakini havifiki mwisho. Kwa hiyo, mpango umejibu kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sehemu ya Kilimo ambayo ndiyo najikita, kwa sababu mimi wananchi wangu ni wakulima, lakini wananchi ambao wameniamini ni wafugaji. Mpango wa Maendeleo umeeleza kwa kuzingatia ile reference ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo, umeeleza mafanikio ambayo tumeyapata kupitia huo mpango. Zipo changamoto ambazo nimeziona kwenye huu Mpango, kwa mfano, Mpango kwenye kilimo umeeleza kwamba, tutaenda kuboresha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukifanya reference ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa ile miaka mitano, ukiangalia tumepiga hatua kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka hekta 695,000 mpaka hekta 983,000 kwa maana kwamba, kuna ongezeko la hekta 288,000. Sasa ukiangalia hizi zimeongezeka kwa muda gani? Utaona ule ukuaji hauendani na malengo yetu. Ikiwa tulikuwa tumejiwekea tufikie angalau hekta 1,200,000, maana yake tumepiga hatua kama kwa 24% tu. Ukiangalia kwa muda uliobaki kukamilika kwa utekelezaji huu utaona speed yetu haiendani na kile ambacho tumejipangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninaangalia hili ongezeko la hizi hekta, ninaona pia, halijaenda kwa usawa. Kwa mfano, jimboni kwangu mimi hakuna bwawa hata moja la umwagiliaji wala hakuna kisima hata kimoja kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Maeneo ambayo wengine tunatoka ni maeneo ambayo ni nusu jangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri tunapoenda kwenye Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ni vizuri yawe yanazingatiwa maeneo kwa kufuata vipaumbele. Yale maeneo ambayo yana hali ya jangwa zaidi yapewe vipaumbele ukilinganisha na maeneo ambayo siyo ya jangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango umeeleza kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. Ukiangalia tumeongeza tani 5,655,000 ambapo hii rate na lengo ambalo tulikuwa tumejiwekea, ni speed nzuri, lakini haijaonesha hapa benchmark. Ukiangalia tumetoka tani 17,148,000 mpaka tani 22,000, maana yake ni ongezeko la tani 5,000,000, lakini mpango hauoneshi kuwa tulikuwa tumejipangia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikawa ninapata wasiwasi inapofika wakati wa kufanya tathmini, tutafanya tathmini kwa rejea ipi ikiwa hatukuweka lengo? Kwa hiyo, yapo madhaifu ambayo nimeyaona. Nikawa ninashauri, ni vizuri sasa kila sehemu tuweke benchmark, tuweke lengo la kulifikia, ili unapokuja wakati wa kufanya tathmini, inakuwa ni rahisi kurejea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwenye sehemu ya kilimo imeeleza mazao ya biashara jinsi ambavyo yameongezeka. Sasa mimi ninataka niongelee zao la pamba kwa sababu, kwetu pamba ndiyo dhahabu, kwetu pamba ndiyo Tanzanite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mpango wa Tatu wa Maendeleo zao la pamba lilikuwa kwenye kilimo cha mkataba na kilimo cha mkataba kilikuwa kinalazimisha mnunuzi mmoja. Kimeleta madhara makubwa kwa wananchi wetu kwa sababu, mnunuzi mmoja inafika hatua anazidiwa na wakulima, analazimika kuwakopa na wakati mwingine wanalazimika kutoa rushwa, ili walipwe haki yao. Kwa hiyo, kilimo cha mkataba kwenye zao la pamba hakijafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa kwa sehemu kubwa tume-address ulimaji wa tija, lakini hatujaangalia kwenye upande wa bei. Hata kama Soko la Dunia likiwa limeshuka, kama tuna wanunuzi wengi maana yake ni panakuwa na ushindani wa bei. Kwa hiyo, ninashauri tunapoenda kwenye Mpango wa Nne, ni vizuri zao la pamba, ikiwa tutaendelea na kilimo cha mkataba, basi tuangalie namna ya kuwa na wanunuzi wengi, ili kuwa na ushindani kwenye bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa mifugo, tumefanya vizuri, lakini ili tuongeze tija, ni lazima tuhakikishe tunajenga majosho kila sehemu. Ni lazima pia, tuongeze malisho.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana, muda wako...

MHE. MUSA G. MBUGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)