Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Rashid Habib Ali

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. RASHID HABIB ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi hii niweze kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Kwanza, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na leo kuweza kuwa hapa katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninakishukuru chama changu, ACT-Wazalendo, chama ambacho kimenilea kisiasa na hatimaye kikaniamini kunipa dhamana ya kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi wa Mwaka 2025 kwa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Mtambwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa, pia ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Mtambwe kwa kunichagua kwa kura nyingi za kishindo na hatimaye leo nikawa mmoja miongoni mwa Wajumbe wa Bunge hili la Kumi na Tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ijumaa ya tarehe 19 Disemba, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, wakati akiwa kwenye semina inayohusu muungano na wahariri wa vyombo vya habari Zanzibar, alinukuliwa, na mimi ninaomba ninukuu sehemu ya hotuba yake. Alisema kwamba, “Wizara hii haihitaji kuzungumzia tena kuhusu kero za muungano badala yake inahitaji kuzungumzia fursa zinazotokana na muungano huo”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya ya Mheshimiwa Waziri bado tunayaweka kwenye mabano. Tukiangalia Mpango wetu wa Mwaka 2026/2027 na Mwaka 2028/2029, moja ya nyenzo iliyotumika hapa ni Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti katika Mwaka huu wa Fedha wa 2026/2027. Maelekezo ya mwongozo huu ni moja kati ya mambo ambayo yamezungumzwa. Wamesema kwamba, zitengwe fedha kwa ajili ya miradi ambayo inahusu mambo ya muungano na utekelezaji wake uonyeshwe wazi kwa pande zote mbili za muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msikitiko makubwa, pamoja na maelezo ya mwongozo huu, lakini haioneshi dhamira ya utekelezwaji wa mambo haya kwamba, yatachambuliwa na pande zote mbili za muungano, zitaoneshwa maslahi yake kwa uwazi, kwa sababu, tukiangalia bajeti ya mwaka 2024/2025 miradi yote ya kimkakati ambayo imetekelezwa, imetekelezwa kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar anatajwa kama jina tu bila kuonesha bajeti na mkakati mahsusi, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Zanzibar. Badala yake Wizara hii inajificha kwenye vikao vya pamoja ikisema kwamba, inaenda kujadili masuala ya muungano kama kichaka cha kuinyamazisha Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunajadili Mpango huu ambao ni dira yetu itakayotuongoza mpaka mwaka 2050, ni lazima twende tukakirekebishe kipengele hiki na hatimaye…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.




TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rashid, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango anaochangia Mheshimiwa Mbunge, ninaomba afahamu na kutambua juhudi kubwa inayofanywa na Serikali kwenye kudumisha Muungano wetu. Muungano wetu huu ni tunu ambayo wote kwa pamoja tunapaswa kuilinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamtoa mashaka, lakini pia ninaomba Kiti chako kiendelee kujielekeza kutufundisha jinsi ya kutumia lugha nzuri ili tusiendelee kutumia lugha ambayo ni ya kuudhi kwa kusema pengine Serikali inatumia kama kichaka, ambayo inakuwa siyo lugha nzuri ya Kibunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rashid taarifa unaipokea?

MHE. RASHID HABIB ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge atulie, sisi tunajenga nchi na hatuwezi kujenga nchi kwa kichaka cha kufichaficha, tutajenga nchi kwa kuweka kila kitu wazi, ambapo pande hizi mbili za Muungano kila mmoja atapata maslahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sekta ya anga, miradi pekee ambayo wamesema inaenda kutekelezwa katika mpango huu ni kupanua viwanja vya ndege. Huwezi ukaichukua Zanzibar ukaiweka na Songwe, huwezi ukaichukua Zanzibar ukaiweka na Mwanza, lazima kuwe na specific chapter ambayo inazungumzia masuala ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi pekee ambayo inatekelezwa Zanzibar ni miradi ambayo ina hadhi ya kuetekelezwa kwa fedha za maendeleo ya Mfuko wa Mbunge lakini miradi ya kimkakati huikuti ikitekelezwa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba mpango huu ndiyo dira yetu na utakaodumisha Muungano wetu ni haki na siyo vinginevyo. Hivyo basi, Kamati ikakae iende ikafanye tena uchakachuzi ili ituletee rasimu ambayo iko vizuri ioneshe maslahi ya pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)