Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Japhael Masanja Lufungija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali cha kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na vikao vyake vyote kuniwezesha kuniteua mimi kuwa Mbunge katika Jimbo la Ulyankulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ulyankulu wote wa Chama cha Mapinduzi na wananchi wote kwa kuniamini, naweka ahadi yao kwamba nitawawakilisha vema kwa muda wangu wote, nikiwa ndani ya Bunge na nje ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mpango mzuri wa Serikali, mpango wa utekelezaji wa miradi kwa wananchi wetu. Mchango wangu nataka nijikite kwenye Wizara yetu ya Kilimo, ambapo naamini ajira kubwa ya Watanzania iko kule. Pamoja na mipango mizuri iliyoelezwa na Waziri wetu hapa, ninataka niishauri Serikali kwamba uwekezaji wetu mkubwa wa Serikali, twende tukawekeze kwenye kupima mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na mashamba ambako shughuli zote za kilimo zinafanyika kule, tutatambua kwamba eneo fulani linatumika kwa kilimo gani? Pia maeneo ya ufugaji tunaamini wananchi wetu ndio wakulima na wafugaji. Yapo maeneo mengi ambayo Baraza la Mawaziri lilifanya maamuzi ya kubadilisha matumizi, lakini tunayo migogoro mikubwa kwenye maeneo hayo ya mipaka baina ya uhifadhi na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili kuweza kuitekeleza vizuri dira hii ni vizuri kila eneo wataalam wetu, Maafisa Mipango Miji, lakini pia na watu wa Idara ya Ardhi waliopo huko kwenye maeneo yetu, kwenda kusimamia mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo. Mpango huu usiposimamiwa vizuri, malengo haya tutakwenda kukwama. Nilikuwa najaribu kusisitiza sana kwenye hilo eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mpango wa uchimbaji wa mabwawa, umewekwa vizuri na umeainishwa. Katika bajeti ambayo inapangwa, nilikuwa naweka sisitizo, maeneo haya ambayo yameainishwa kuchimbwa mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji ni vizuri yakapewa kipaumbele ili kuendelea kutekelezwa. Tukitekeleza haya, nina imani kubwa kwamba tutaondokana na kilimo cha kutegemea mvua ili wananchi waweze kuzalisha kwa wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka niliwekee uzito kuishauri Serikali ni suala la huduma za afya. Tumejenga vituo vingi vya afya na zahanati, lakini katika maeneo hayo ni vizuri kuimarisha afya za Watanzania kuendelea kuimarisha miundombinu kwenye vituo vya afya ambavyo tayari vimeshaanza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua vimejengwa vingine watumishi wetu kwa maana ya Madakari na Manesi hakuna hata nyumba za kuweza kuishi. Wanalazimika kuishi mbali ambapo ili kuwapata wananchi, wanalazimika kutafuta usafiri wa kumfuata mhudumu kwenye eneo la kituo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka kuishauri Serikali iweze kusimamia jambo la kuhakikisha kwamba miundombinu rafiki kwenye maeneo yetu ya vituo vya afya, zahanati na hospitali yanaimarika ili kumarisha afya za Watanzania kwa ajili ya kutengeneza Taifa lenye afya bora na kuimarisha afya za Watanzania ili waweze kutimiza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hotuba pia ya Mwenyekiti wa Kamati, pamoja na ushauri wake, nami naungana nao kabisa, kwamba yako maeneo muhimu sasa yanatakiwa kuangaliwa. Ule ushauri wa Kamati uzingatiwe ili kwenda kuitekeleza vizuri hii Dira ya Taifa ya Maendeleo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unanionesha kwamba, asilimia kubwa ya Watanzania walioko kijijini ni vijana ambao ndio Taifa tunalolitegemea. Kwa hiyo, naendelea kushauri kwamba kuwe na sheria na sera nzuri za kuweza kutengeneza mazingira kuhamasisha vijana hawa wanakwenda kutimiza majukumu, utendaji wa kazi kuliko vijana wengi kubaki wakizurura wakati wa kazi. Kwa hiyo, nashauri sana Serikali ili kuweza kwenda vizuri na Mpango wetu wa Dira ya Maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, tunavyo vijiji vingine vipya ambavyo Baraza la Mawaziri lilikubali viendelee ambavyo vilikuwa ndani ya hifadhi. Eneo hilo la wananchi wetu halipitiki. Ninaiomba Serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi kupeleka miundombinu ya barabara katika maeneo hayo. Kuwekwe bajeti kubwa ili barabara zifunguke ili kuwasaidia wananchi kusafirisha bidhaa wanazozalisha na kuyapata masoko bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanakosa fursa ya kupata bei kwa sababu tunakuwa na changamoto maeneo mengine, usafirishaji wa mazao yao wanaingia gharama kubwa. Kwa hiyo, magari hayawezi kufika wanalazimika kusafirisha kwa usafiri ambao ni duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuiomba sana Serikali kuyatazama wakati wa bajeti maeneo haya ya vijiji vipya ili kuweza kufungua miundombinu ya barabara iweze kuimarika ili wananchi wetu waweze kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ambao tumeupokea hapa ni mpango mzuri. Kikubwa tu ni kuweka sheria na sera nzuri za kwenda kutekeleza vizuri mpango huo. Mimi natoka Jimbo la Ulyankulu, iko mipango ambayo Serikali iliekeza kwa muda mrefu, lakini unaweza kuona utekelezaji wake, pamoja na mambo mazuri ambayo yamefanyika, inahitaji speed ya kukimbia tu ili kuweza kuitimiza mipango ya wananchi ili waweze kupata fursa ya maendeleo katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi hii ya mchango wangu nilipenda kuishauri hivyo Serikali katika maeneo hayo ya uwekezaji kwenye kilimo, kwenye mifugo, kwenye mambo ya afya kuhakikisha kwamba tunaelekeza fedha nyingi ili Watanzania waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)