Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii, kwa kuwa ni mara ya kwanza kusimama katika Bunge Tukufu, kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kuweza kutufikisha mahali hapa na mimi nikiwa mwakilishi wa kundi la Vyuo na Vyuo Vikuu, ninashukuru sana kwa kibali alichonipatia na kuweza kusimama mahali hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kushukuru chama changu Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wajumbe wa Kamati Kuu kwa kuteua jina langu na hatimaye leo ninasimama hapa kama Mbunge wa Viti Maalum, kundi la Vyuo na Vyuo Vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisahau Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa, ambao walinichagua na kuwa miongoni mwa Wabunge watatu wa Vyuo na Vyuo Vikuu, ninashukuru sana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nichukue fursa hii pia kusema jambo katika mipango hii ambayo tangu asubuhi ikiwa ikiwasilishwa hapa, ni jambo zuri sana kama nchi kuwa na mikakati kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia miongozo hii tukiona Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na hiyo miongozo mingine. Yote haya ni mambo ambayo ni ya msingi katika Taifa ili kuwa na Taifa lenye ustawi wa wananchi, lakini ikiwa pia na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kabisa Taifa linafika katika mipango ambayo imejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Kamati ambayo imeandaa na kuratibisha mambo haya. Ni mambo ya kitaalamu sana. Kwa hiyo, tunapongeza sana juhudi za kuhakikisha kuwa tunakuwa na mikakati kama hii na mipango kama hii katika Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja muhimu za kuongeza katika hotuba mbalimbali ambazo zimetolewa kuhusiana na mipango hii. Kwanza ni utekelezaji kwa vitendo hadi ngazi ya chini. Tumeona kabisa ya kwamba hata Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza habari ya ushirikishwaji wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ninaliona kama ni jambo la msingi sana. Ni lazima kuwe na utekelezaji kwa vitendo hadi ngazi ya chini, ambapo tunaita localization of vision 2050. Hii itasaidia kutafsiriwa katika lugha nyepesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tunaona ni mkakati ambao upo kitaalamu sana. Mimi nipongeze lakini nitoe ushauri kwamba dira hii itafsiriwe kwa lugha rahisi na kushushwa hadi mikoani katika halmashauri, hata kata na vijiji ili basi ownership ya wananchi iwepo, waweze kufahamu nchi inatoka wapi, na inakwenda wapi? Kwa hiyo, ninaomba, mpango huu mahususi uwe na mikakati ya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu uhusiano wa moja kwa moja kati ya Dira ya 2050 na Mipango ya Miaka Mitano na ule Mpango wa Mwaka Mmoja. Tumeona kabisa ya kwamba ni vizuri mipango yote hii ikawa inaenda pamoja, yaani kuwe na link kati ya mipango hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, mpango ule wa mwaka mmoja pamoja na bajeti za kila mwaka, ni vizuri ikasomana. Nilitamani, na ninafikiri wenzangu pia waliongea habari ya kuwa na legal framework; binding legal framework ambayo itakuwa inalinda hii mipango mikakati ambayo tumejiwekea kama Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, na hiki wenzangu pia wameongea, ni habari ya mtaji wa watu (human capital development). Tumeshuhudia Serikali ikiwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kabisa kuwa Taifa linakuwa na mtaji wa watu ambao watafanya kazi katika viwango na katika tija inayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kupitia Wizara ya Elimu, wamekuwa wakiwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta hii. Tumeona kabisa upande wa vyuo na vyuo vikuu bajeti za mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu imeongezeka. Hili siyo jambo la kubeza, ni jambo la kuipongeza Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii niseme ni initiative ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kabisa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu wanapata mikopo na kusoma vizuri. Hii ukijaribu kuioanisha na Dira ya 2050 na hii mipango mingine utaona kabisa tunahitaji uwekezaji mkubwa katika elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize tu kwamba uwekezaji huu uende sambamba na afya, ujuzi na ubunifu ili tuwe na manpower ambayo itaweza kuhimili soko la ajira na kuweza kufanya kazi katika tija na hivyo Taifa liweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee jambo lingine, kuhusu usawa wa kimaendeleo kati ya mikoa. Hili ni jambo la msingi sana. Mipango hii ikajaribu ku-reflect jambo hili kwa wigo mpana; usawa wa kimaendeleo kati ya mikoa (regional equity). Ni kwa nini ninasema hivi? Kama tunavyojua, kuna mikoa haifanani, mikoa inatofautiana kimaendeleo na namna ambavyo jiografia zilivyo. Kwa hiyo, ninaomba mipango hii ijaribu kuliangalia hili kwa mapana yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa ambayo ipo pembezoni, kuna mikoa ambayo ipo katika visiwa. Kuwe na special intervention; kuwe na miradi ambayo ni maalum katika maeneo haya. Hii inaweza ikaleta ile balance ya maendeleo katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapongeza, na Kamati wamejaribu kulielezea kwa mapana ni kuhusu masuala ya ufuatiliaji, tathmini pamoja na uwajibikaji (monitoring, evaluation and accountability). Hili ni jambo la msingi sana. Tunapokuwa na miradi, lazima jambo hili liwe kazini kuhakikisha kabisa kila kinachofanyika kinakuwa na tija katika Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi ambalo ninaomba niongee hapa ni kuhusiana na sekta ya maendeleo ya jamii kama chombo cha utekelezaji. Tumeona kabisa ya kwamba dira inaongelea habari ya maendeleo ya watu, lakini ni nani atawajibika katika utekelezaji wa majukumu haya?
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ninaomba tu niongee hii nikiwa na lengo la kuonyesha namna ambavyo sekta ya maendeleo ya jamii ni muhimu sana katika utekelezaji wa mpango huu, kwa sababu ni taaluma hii ambayo watu wa maendeleo ya jamii wanapaswa kuhakikisha kabisa kuwa mpango huu unawafikia wananchi kule walipo; kujua kabisa ya kwamba ni nini ambacho wamepanga? Wana vipaumbele gani? Mchango wao ni nini katika mpango huu maalum wa nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sekta ya maendeleo ya jamii iwe ni kiungo kati ya sera, iwe ni kiungo muhimu kati ya dira na maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninaweza kuliongea hapa ni kuhusiana na masuala ya utawala bora na mabadiliko ya tabia, (mindset change). Utawala bora umetajwa kama msingi katika miongozo hii. Ninaomba tu, kuwa tuongeze masuala ya maadili, uwajibikaji wa viongozi na pia tuongeze masuala ambayo viongozi wanaweza wakawa wabunifu. Kunaweza kukawa na innovation na mambo kama hayo. Viongozi wa namna hii watalisaidia Taifa kuhakikisha kabisa mambo haya yanasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii ya pekee sana ambayo nimepewa. Pia niongeze kitu kimoja, ni kuhusu ushirikishwaji wa wadau muhimu hususan wa sekta binafsi. Tumeangalia, hapa kuna sekta binafsi, vyuo vikuu, na taasisi za utafiti. Ninaomba Serikali ihakikishe kabisa inashirikisha taasisi hizi muhimu ili nao wawe na umiliki wa dira na kuongeza ubunifu katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise, ninashukuru sana kwa nafasi hii ya pekee ambayo nimepewa. Kwa kumalizia niseme tu ya kwamba, ninasisitiza kuwa Dira ya Taifa 2050 siyo hati ya sera pekee, bali ni mkataba wa kijamii kati ya Serikali na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo tunayoitekeleza leo inaweka msingi imara wa Tanzania tunayoitamani kesho. Hili ndilo tabasamu ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka liwe katika maisha ya Watanzania siku zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuwasilisha. (Makofi)