Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Mwanahamis Athumani Munkunda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo nimepata ya kuchangia leo kwenye Dira na Mpango wa Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha kwa wasilisho zuri ambalo kwa kweli lilikuwa siyo wasilisho tu, bali ni darasa tosha ambalo lilikuwa limejitosheleza kueleza namna Serikali ilivyojipanga kwenye Dira ya Maendeleo, pia kwenye Mpango wa Miaka 25 na ule Mpango wa Niaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaomba nijielekeze sasa kwenye mchango wangu ili kuhakikisha kwamba mipango hii pamoja na mambo mazuri ambayo yameelezwa na Serikali. Vilevile niwapongeze pia Kamati ya Bajeti kupitia Mheshimiwa Mwenyekiti kwa namna walivyochambua nyaraka hizi zote tatu ambazo kwa kweli zikifanyiwa utekelezaji mzuri kama ambavyo Kamati imeelekeza, kutakuwa na tija kubwa kwenye Taifa letu na kufikia dira ya maendeleo, hasa ile ya mpango wa miaka mitano hata kabla ya miaka mitano kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie hasa kuhusu Serikali kuongeza mapato yasiyo ya kikodi. Hizi non tax revenue ziwe kama mbadala wa mikopo ambayo inagharimu fedha nyingi kwenye uchumi wetu. Hapa tunategemea mashirika na taasisi zetu za umma kuwa wabunifu na kuongeza mikakati katika vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mashirika na taasisi ambazo zinafanya biashara zije na mikakati mipya ya kubuni biashara ambazo hazihitaji stake kubwa ya Serikali kwenye uwekezaji. Kwa mfano, kuja na mbinu mpya kwenye uwekezaji wa biashara ya carbon.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa mashirika kama TRC wanayo maeneo makubwa ambayo ukiangalia barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma wana eneo kubwa ambalo pia wanaweza wakajielekeza kwenye uwekezaji wa carbon kama ambavyo wanafanya vizuri Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, ambao kwa mwaka wanapata mapato zaidi ya shilingi bilioni 20 kwenye uwekezaji ya biashara ya carbon. Biashara hii haihitaji mtaji wa Serikali, inahitaji tu kubadilisha mindset na kufanya uwekezaji na kuongeza mapato ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye mashirika ambayo yana assets nyingi ambazo non-performing assets kwa shirika kama Shirika la Posta, shirika kama hili linazo rasilimali nyingi ambazo zipo idle, hazitumiki, haiziingizi, zinaweza zikafanyiwa mikakati, hasa zile assets kama majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanashindwa kuyatumia kama assets za uwekezaji, matumizi yake yanaweza yakabadilishwa au yakafanyiwa PPP na private sector yakaweza kuleta tija kubwa kwenye ukusanyaji wa mapato ambalo ndiyo changamoto kubwa kwenye miradi mikubwa na hasa kwenye mapato ya Serikali, kuliko kuacha, kama ambavyo sasa hivi hizi non-performing assets zinaendelea kuleta hasara kwenye mashirika haya, na hasa Shirika hili la Posta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuja na mikakati na mawazo chanya. Kwa mfano, leo shirika la Posta linaweza likageuka likawa Amazon ya Tanzania. Wafanyabiashara hasa wanaofanya kwenye hizi digital platform, wakatumia Shirika la Posta kwa kushirikiana na TCRA ikawa ni platform kubwa ya kufanya biashara kama ambavyo Amazon au na mashirika mengine ya kimtandao yanavyofanya baishara, kuliko kusubiria biashara ambazo imeendelea kufanya au imeendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa shirika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa ambalo Kamati pia wamelisema, nami ninaungana nao, mashirika au taasisi zetu kupunguza mzigo wa bajeti au kutegemea ruzuku ya Serikali na kuanza kujiendesha kibishara ili kuongeza ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kuongeza ushindani, bali pia kuanza kufikiria mashirika haya, kama ambavyo makampuni binafsi yanaweza kufanya ushindani kwenye masoko; kwa sababu mashirika na taasisi za Serikali zina rasilimali ya mtaji mkubwa, zina rasilimali watu wa kutosha lakini bado yanaweza kufanyiwa reforming kubwa ambayo inaweza ikaleta tija ya mageuzi ya kifikra na kuanza kufikiria mashirika haya kujiendesha kibiashara kuliko kutegemea ruzuku ya Serikali. Hii itasaidia sana kupunguza utegemezi na kupunguza bajeti ya matumizi ya Serikali kwenye mashirika haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lingine ambalo tunaweza tukalifanya, na Kamati wamelisema, kutumia utalii kwenye maeneo ambayo bado hatujayagusa. Ni kweli kabisa utalii imekuwa sekta muhimu sana katika pato la Taifa. Kwa mfano, kwa mwaka 2024 waliweza kuingiza pato la Taifa 3.5 billion US Dollar, lakini mapato haya yote yameingizwa kwenye utalii wa aina moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo diversity kubwa kwenye utalii kama utalii wa asili lakini pia utalii wa vivutio mbalimbali ambavyo kwa mtawanyiko wetu na namna ambavyo Tanzania ilivyo kwa wingi wa makabila na wingi wa mikoa na mgawanyiko wa rasilimali watu, tunaweza tukatumia utalii mwingine wa ekolojia na mambo mengine ukatusaidia sana kuongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunao utalii ambao bado haujaingizwa, ambao tukiusimamia vizuri kama Serikali tunaweza tukapata mapato makubwa. Tumezoea kuona ile migration ya Serengeti, lakini kule Mtwara tunayo migration ya nyangumi ambayo kwa duniani inapatikana Tanzania pekee, kwenye maingilio ya Ghuba ya Mnazi Bay.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuanzia Julai mpaka mwezi wa Novemba tunapata makundi ya nyangumi maelfu kwa maelfu yanakuja kwa ajili ya kuzaliana kwenye maingilio ya Mto Ruvuma na kwenye Ghuba ya Mnazi Bay pekee, Tanzania hii. Hilo tu linaweza likaingiza fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ukanda tu wa bahari na eneo dogo ambalo linaweza likafanyiwa kazi na mapato haya yakaweza upanda kama ambavyo Serengeti imekuwa ikifanya vizuri kwenye hii migration ya nyumbu. Pia tunao ukanda wa bahari mkubwa; na Kamati pia wameeleza vizuri kwamba tunaweza kutumia ukanda ule wa Bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatolea tu mfano kwa Wilaya moja ya Mtwara ambayo ina ukanda wa bahari wa kilomita zaidi ya 101, tena ni clean na ina beach nzuri. Ukanda ule, pamoja na kuleta uchumi wa buluu tunaweza pia kuutumia kwa biashara ya carbon ambayo haiihitaji mtaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii tukiweza kuisimamia vizuri italeta fedha nyingi sana. Leo hii kwenye halmashauri 189, tukiweza kusema, halmashauri ambayo inaweza ikatoa dividend kwa Serikali ni Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambayo inafanya vizuri kwenye biashara hii ya carbon. Imekuwa kinara kwa sababu viongozi walikaa wakaamua na wakasimamia na ikawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tunaweza tukalifanya vizuri na kuongeza mapato ni kwenye miundombinu na viwanda. Serikali iendelee kuunganisha miundombinu ya barabara na umeme, hasa kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu, huku kukiwa na umeme wa uhakika hasa kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo ambao wanatumia gharama kubwa sana kuendesha shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapata umeme na miradi inaendelea, tunaipongeza sana, lakini wajielekeze kwenye maeneo ya kimkakati, hasa haya maeneo ya uzalishaji, kama vile maeneo ya wachimbaji wadogo au maeneo ya wavuvi ambayo yataleta mapato makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia wachimbaji wadogo wenyewe wakisema kwamba siyo tu wachimbaji wadogo, bali ni nguzo kubwa ya mapato ambayo wananchangia kwa asilimia kubwa na kufanya stabilization kwenye sekta hii ya uchimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwepo wa migodi mikubwa ya wachimbaji wadogo, lakini hawa ndio wanasaidia pia kufanya stabilization ya uchumi kwa sababu fedha yao inazunguka ndani ya Watanzania na manufaa yake tunayaona moja kwa moja kwenye maisha ya Watanzania ambao pia ndiyo uchumi jumuishi ambao tunausema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi ambalo tunaweza tukalifanya, yapo maeneo ambayo Serikali imewekeza mtaji, tena ambayo ni minority shareholder. Kwa mfano, kwenye Benki ya NMB Serikali inapata gawio hadi kufikia shilingi bilioni 70, lakini ni maeneo ambayo wamewekeza mtaji ambao siyo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo tukiyasimamia vizuri, Serikali inaweza ikapunguza stake yake na bado tukapata gawio kubwa. Serikali ibadilishe mindset, siyo tu kwenda kwenye umiliki, na kuja na fikra mpya ya uwekezaji. Kwa sababu unapomiliki ile hali ya uwekezaji inaondoka. Kwenye maeneo ambayo Serikali imewekeza kwa asilimia kubwa hatuoni kama tunapata faida kubwa kama maeneo ambayo tumewekeza kwa asilimia kidogo na yanaleta tija kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni hii Benki ya NMB ambayo mwanzo ilikuwa haileti gawio kubwa, lakini sasa imekuwa kinara pia kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, tunaweza tukabadilisha uelekeo tukaenda kwenye uelekeo huu ambao Serikali imeufanya kwenye Benki ya NMB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunaendelea kuishauri Serikali kuja na fikra mpya ya uwekezaji na siyo tu ya umiliki mali. Ikija na fikra ya uwekezaji, tutakuja na mikakati mipya kwenye maeneo ambayo yataleta tija kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninataka niungane na Kamati ya Bajeti, kwenye yale maeneo yote ambayo wamesema kwamba Serikali ije na mikakati mipya ya uwekezaji hasa kwenye maeneo ambayo yataleta tija kwa haraka, ambayo ni maeneo ya migodi, maeneo ya madini pia na maeneo ya utalii. Maeneo haya yakiwekewa nguvu na tija tunaweza tukapata rasilimali ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja.