Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwanza kabisa, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuwa mahali hapa, muda na wakati huu. Pia nikishukuru Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kupendekeza jina langu na kuendelea kuwa mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam. Vilevile, niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuendelea kuwa na imani na mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kumpongeza Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, kaka yangu Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Mpango huu. Pia Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar kwa maandalizi mazuri ya huu Mpango. Mpango huu ni mzuri sana, lakini endapo utatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa Mpango Elekezi ni Dira ya 2050 ambayo imejikita kabisa katika kuhakikisha pato la Taifa linaongezeka na uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa kuzingatia fursa za usawa kwa wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utekelezaji wa Mpango huu ili tuone tija na matokeo na kupima utekelezaji wake, mdau wa kwanza ni mwananchi na ndiyo maana kukawa na suala la kufikiria namna ya kuongeza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kuwainua wanawake kiuchumi, kuwainua jamii kiuchumi au pato la mwananchi, tukienda kuangalia Mpango huu na fursa ya mikopo ya 10% kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, nilikuwa ninapendekeza Maafisa Biashara wa Halmashauri wawe karibu sana na vikundi vinavyonufaika na mikopo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Biashara hawa watasaidia sana katika suala la elimu, kuwaonyesha namna ya kuzifikia zile fursa, mafunzo ya ujasiriamali na mafunzo ya fedha. Vikundi vingi vimefeli katika mikopo wanayopewa kwa sababu ya kukosa elimu. Lengo la mikopo hii ni zuri sana, lakini utekelezaji wake umefeli, sababu wanufaika wengi wanapata pesa kabla ya kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi viko vya aina tatu. Kuna kundi la kwanza ambalo wao wanaunda vikundi kwa kusubiri mikopo, na wengi wao wamepata, lakini wameshindwa kurejesha. Kuna kundi la pili ambalo tayari wameshaanza uwekezaji mdogo mdogo, wao kama wao. Mikopo hii imewasaidia lakini bado haijafikia lile lengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la tatu, ni makundi ya wanawake wawekezaji wa huduma ndogo za kifedha almaarufu kama vikoba. Hawa tayari wana mitaji yao, wanawekeza hisa kwenye vikundi vyao, wanakopeshana mikopo midogo midogo, wenyewe wanahitaji fedha kubwa kwa ajili ya kufanya uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninapendekeza fedha hizi ziangalie makundi yote matatu. Kuwe na makundi mbalimbali, yaani kundi hili lipate mkopo huu; kundi hili, mkopo huu; na kundi hili mkopo huu. Dira inasema, kuwe na viwanda vidogo vidogo. Sasa ili tuvione hivi viwanda, lazima vikundi ambavyo vinajiweza na vina mitaji viweze kukopeshwa mikopo kwa ajili ya kuanzisha viwanda. Vikundi hivi Mkoa wa Dar es Salaam vipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam kuna vikundi vya akina mama vina mitaji mpaka shilingi milioni 700 mpaka shilingi bilioni moja. Sasa watu hawa hawatafuti mikopo kwa ajili ya kukopeshana wao, hawa wapewe mikopo kwa ajili ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makundi haya ambayo yanajiweza, tunaomba waunganishwe kwa wadau mbalimbali wakubwa au makampuni, viwanda na wawekezaji. Dar es Saalam ni mkoa ambao una viwanda vingi sana pale. Kuna wawekezaji wakubwa. Kazi ndogo ndogo za usafi, chakula, ku-supply baadhi ya material, wapewe wakina mama wa vikundi ambao tayari wana mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ni Mkoa ambao umebeba sura ya Tanzania, ni jiji la kibiashara. Shughuli kubwa na ya msingi ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam ni ujasiriamali na biashara tu. Kwa hiyo, mitaji ndiyo hitaji kubwa na la msingi na la kwanza ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna makundi ya vijana wengi sana Dar es Salaam. Kuna vijana waliomaliza vyuo, vijana ambao hawakwenda shule wote, wapo; na wote hawa wanatakiwa kunufaika na fursa hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yukiangalia kundi la vijana, Maafisa Usafirishaji maarufu kama bodaboda, kwa Mkoa wa Dar es Salaam asilimia nne tu ya vijana ndio wanamiliki bajaji zao wenyewe. Wengi wao wanatumia bajaji za kukodi, anapata fedha yake ya kujikimu na ya kupeleka kwa mwenye bajaji. Pia, wengi wao ni vijana ambao tayari wana familia au wanalea wazazi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanaomiliki usafiri wa bodaboda wa kwao ni 30% tu, 70% ni bodaboda za kukodi, lakini pia asilimia mbili tu ndio wanamiliki maguta yao wenyewe. Sasa vijana kama hawa tuangalie namna ya kuwawezesha vitendea kazi badala ya kuwapa fedha. Uhitaji ni mkubwa mno katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kata ninayoishi mimi, kuna vijana bodaboda 300 na Mwenyekiti wa Vijana wale ni kijana ambaye ni graduate wa chuo kikuu. Tulikaa tukatengeneza jukwaa la vijana wale ndani ya kata, tukakubaliana tukaenda kwa mtu ambaye ana-supply pikipiki akatupa masharti. Sharti la kwanza lazima kuwe na ofisi. Jukwaa lile lisajiliwe na kila mwanajukwaa lile awe na kitambulisho cha NIDA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyote hivyo tulifanya, tukakubaliana kwamba wakati vijana wanasubiri mkopo wa halmashauri, basi tuanze kuwekeza wenyewe. Tukaanza kuweka shilingi 40,000/= kila kijana kwa wiki kwenye mfuko ambao tulifungua kwenye Benki ya CRDB, ile shilingi 40,000/= kwa wiki, kwa mwezi tuna shilingi 160,000, na kwa mwaka itakuwa shilingi 1,920,000/= ambayo tukipeleka kule kwa muuza pikipiki, anatupatia pikipiki mpya kwa umiliki wa yule kijana, na iliyobaki anamalizia ndani ya miezi sita. Cha ajabu, ndani ya vijana 300 walioweza kufanya hilo ni vijana 20 tu na hao ni kati ya wale wanaomiliki pikipiki zao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vijana 280 wote imeshindikana kwa sababu anachokipata hakimtoshi yeye na kupeleka kwa mhusika mwenye pikipiki zake. Kwa hiyo, ninaomba, mikopo hii ya halmashauri tuangalie zaidi kwenye vitendea kazi. Tusiangalie zaidi kwenye fedha. Fedha tumeshatoa sana na zimeshindikana nyingi kurudi. Fedha nyingi hazikurudi, kwa hiyo, tuangalie pia na vitendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninatoa shukrani za dhati kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye suala la kuwasaidia watu kupata elimu ambayo itawasidia kujikwamua kiuchumi ametusaidia sana wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ametoa ufadhili wa wanawake 3,000 kwenda kusoma VETA mafunzo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kwa wanawake wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, batch ya kwanza ya wanawake 405 wamesha-graduate wapo mtaani, batch ya pili ya wanawake 543 wamesha-graduate mafunzo yao, wapo mtaani, na mwezi Aprili mwaka 2026 tuna batch nyingine ya wanawake 400, lakini mpaka sasa walionufaika na mafunzo hayo ni wanawake 948. Wote hao wapo mtaani, wamesoma kozi tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe halmashauri, kundi hili lipate mikopo na mikopo yao wapate vitendea kazi waingie kabisa site. Wameshajifunza kutengeneza batiki, ku-print, kupamba, salon, na kila kitu wameshajifunza. Wanahitaji vitendea kazi waingie kazini. Hawa waweze kuzalisha, wajikwamue wenyewe na waongeze pato la uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya kundi hili tutengeneze walipa kodi wapya. Hasa Kundi la wanawake 948 Mheshimiwa Rais ameshawapa ujuzi, wapo mtaani, hawana mikopo, haisaidii na inavunja moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya wajasiriamali wa Taifa hili. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imeshapata shilingi bilioni 10.5 ambayo inakwenda kwa makundi ya wajasiriamali hawa hawa wadogo wadogo ambao kwa mwaka return yao isizidi milioni tano, lakini huku mtaani kuna wajasiriamali ambao wanasubiri hii fursa hata ukiwaambia return ya shilingi milioni moja hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya mwasisi wake alikuwa ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais aliyaanzisha mwaka 2016 yalienda yakafa. Mwaka 2022 yakazinduliwa tena, kukawekwa mpango mzuri sana. Ukiusoma ule mpango unaona kabisa majukwaa haya yanaenda kuwa mkombozi wa wanawake wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam tayari kila kata katika kata zote 102 zina makundi ya akina mama. Majukwaa haya yana uongozi, wamejisajili, wapo tayari wanasubiri fursa za mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe hili sharti la kuwa na return chini ya shilingi milioni tano kwa mwaka, hebu liangaliwe vizuri ili wanufaika wawe wengi. Kwa sababu haya majukwaa yapo tangu mwaka 2022. Sasa kwa vigezo kama hivyo watajikuta na fursa hii inawapita, na kwenye kila foleni ya halmashauri bado wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshajitahidi kutafuta wadau kuwapa semina, sasa inakuwa kama vile tunawadanganya na muda unazidi kwenda. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara ya Maendeleo, Jinsia na Maendeleo ya Jamii waliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiacha kundi hili, Dar es Salaam tuna Jukwaa la Wanawake Wajane. Wanawake wale wamepambana wale wachache ambao wanafanya shughuli zao ndogo ndogo za ujasiriamali, wamekubali kujitoa kwa ajili ya wenzao. Tumepata mashamba Kibiti ekari 20, lakini pa kuanzia ndiyo shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, awasaidie wanawake hawa wa Jukwaa la Wanawake Wajane wachimbiwe kisima. Wanataka kulima mboga mboga. Hawa hawana mradi, hawana biashara, wana mashamba. Wanasaidiwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi hata halmashauri zetu, kwa sababu jukwaa hili ni la wanawake wote wajane wa Wilaya ya Kinondoni, wakati tunaendelea kutafuta fursa na kuwakusanya na kuwaweka pamoja, wilaya nyingine walau hili la Kinondoni lianze ili kuwe na uhalisia, nao waone kweli inawezekana. Wana ari na wanatamani kulima mboga mboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam pana hoteli nyingi, pana migahawa mingi, pana kila aina ya biashara, lakini wanawake hawa wakilima mboga mboga soko lipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi ya muda ninashukuru sana, niishie hapa, mengine nitaweka kwenye maandishi. (Makofi)