Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii uliyonipatia na mimi nichangie kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninaipongeza Serikali kwa kuja na mpango mahususi wa kiungwana kabisa kwa Watanzania wazalendo wa kimkakati wa kuhakikisha Taifa letu linatoka hatua moja kwenda hatua nyingine kwa kipindi cha miaka mitano. Ninaona hapa projection ya uchumi kwa maana ya economic growth kwa mwaka 2025 imekuwa kwa asilimia tano nukta sita, lakini pia tunatarajia mwaka huu inaweza ikaenda asilimia sita halafu mwakani ikaenda kama asilimia sita nukta nane au around hapo saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona malengo ya Wizara na malengo ya Mpango wetu ni kutengeneza uchumi imara, uchumi ambao utakuwa jumuishi, lakini pia wa kiushindani. Nianze na kwenye uchumi imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchumi imara, hapa lazima maana yake kama Taifa tuwe na base ya Kitaifa ambayo itasababisha uchumi wetu kuwa stable katika kipindi chetu cha miaka mitano au kipindi cha miaka 25 mpaka 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wangu, kama Taifa ni kweli tunatamani mambo yote yaende vizuri, sekta zote ziende vizuri, lakini ningetamani kama Taifa tuwe na vipaumbele vichache ambavyo kama tutajikita na halafu tujivunie kupitia vipaumbele hivyo kama Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kilimo. Ninashauri kama Taifa, tujikite sana kwenye kilimo kwa sababu kina tija kubwa sana kwa wananchi wetu mmoja mmoja na kwa Taifa kwa ujumla. Kwenye andiko hili inaonyesha kilimo, ndio wanaochangia sehemu kubwa ya pato la Taifa, wastani wa 20% mpaka 24%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeshauri kama Taifa tuwe na mikakati madhubuti ya kimakusudi ya kuhakikisha tunaki-boost kilimo ili angalau tusiwe na kilimo ambacho kinaweza kikayumba kutokana na msimu. Maana yake hapa nashauri tuongeze mikakati ya umwagiliaji, mikakati ya uvuvi, mikakati ya kutumia vyanzo vyetu vya maji tulivyonavyo kama Taifa kuhakikisha wananchi wetu tunawahakikishia kilimo muda wote na mazao muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kilimo hapa labda nizungumze, kwa mfano, Jimbo langu la Kasulu Vijijini tuna maeneo mengi sana ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambayo kama yakitumika vizuri kwa kweli wananchi wangu kwa kweli ni neema ya pekee na utakuwa umegusa maisha ya almost robo tatu ya wananchi wangu wa Jimbo la Kasulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa ushauri wangu kama Taifa tungewekeza msukumo mkubwa tuka-boost kilimo pengine kichangie hata 30% pengine mpaka 40% kwenye uchumi wetu au pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie upande wa masoko. Changamoto nyingine iliyopo kwenye kilimo, ni masoko. Kwenye mchango wangu uliopita kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nilishauri kwamba ikiwezekana tuitumie TEHAMA vizuri ili kutafuta masoko ya uhakika kwa wananchi wetu. Tuje na mifumo ambayo mwananchi wa vijijini, mwananchi wa mbali anaweza akaangalia Soko la Dar es Salaam linasemaje kuhusiana na mazao yake yaliyoko kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishauri kwamba ikiwezekana tuwe na mfumo software au application ambayo mwananchi aki-click kama ni Mchele, kama ni Pamba na kadhalika, ataona soko linasemaje hapa Dodoma, Kilimanjaro, au Babati na maeneo mengine. Vilevile, anaweza kuona mpaka nchi jirani kunasema nini kuhusiana na zao hilo kuhusiana na suala la bei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba uwepo pia mkakati wa kimakusudi wa kufungua maeneo ya vijijini, kwa maana ya barabara zipitike kwa kiwango cha changarawe, kwa kiwango cha lami. Nilikuwa ninaangalia kwenye ujenzi wa mtandao wa lami waliojenga kwa barabara zilizoko TANROADS ni kama kilometa 100 na kidogo tu ambapo ukiangalia pale kwa kweli inasikitisha kama tuna makusudi kweli ya kuhakikisha kwamba tunafikia malengo yetu kwa kipindi cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusiana na upotevu wa mapato. Kama Taifa, nimeona hapa wanasifiwa watu wa Local Government Authorities kwamba wamechagiza sana performance ya ukusanyaji wa mapato, lakini kinachoendelea kwenye Serikali zetu za Mitaa pamoja na performance inayoonyeshwa hapa kwamba wamefanya vizuri kwa kweli kinasikitisha sana. Kinachotokea kule moja, kuna wakati kule wanajitengea bajeti ndogo yaani wanafanya underestimation ya vyanzo vyao vya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano; kuna mahali fulani nilienda wameandika watakusanya pale milioni 50, lakini ukiangalia kile chanzo cha mapato yako mapato ya waziwazi kabisa ambayo wanaweza kukusanya mpaka milioni 150. Kwa hiyo, baadaye wakiweka ile kadirio la chini la milioni 50 wakishafikia milioni arobaini na kidogo wanajipongeza kwamba wame-perform sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninafanya Masters yangu nimefanya utafiti kwenye Local Government Authorities hasa kwenye ukusanyaji wa mapato. Kule mapato mengi yanapotea ukilinganisha na kile ambacho tunakusanya yaani pengine inaweza ikawa ni nusu kwa nusu, yaani kinachopotea na kile tunachopata kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba, kama Serikali tujikite kwenye matumizi ya TEHAMA ya kisasa. Kwanza nipongeze kwamba point of sales imekuwa ikifanya vizuri, lakini baadhi ya maeneo haifanyi vizuri hasa kwenye stendi zetu. Kwa mfano stendi zile za Magufuli na stendi zingine kuna maeneo ukienda pale getini hali ni mbaya, ukienda vyooni hali ni mbaya, mtu anaingia hakuna chochote kinachokusanywa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali nilijaribu kuuliza baadhi ya watu wanasema wanatumia loopholes iliyopo kwa sababu mtu anaingia au anaweza akapitisha gari getini ikiishapita gari au ikapita pikipiki hachani karatasi ile yaani ha-print kwa maana ile risiti ya point yaani point of sales kwa maana ya POS hampatii risiti ili mradi tu amepita kama ni chooni ameenda amerudi, kwa hiyo, unakuta tunapoteza mapato mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niishauri Serikali tuangalie namna ya kuziba mianya hasa kwa yale mapato tutakayokusanya kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri kuhusiana na uchumi wa ushindani. Tunavyoangalia uchumi wa ushindani lazima tujipime na wenzetu. Sasa kwa Afrika Mashariki inaonekana uchumi kwa mwaka jana 2026 ulikuwa wastani wa 5.3, lakini uchumi wetu umekua kwa asilimia 5.6. Hapo hapo kuna mataifa mengine kama Rwanda yako saba lakini pia Uganda na yenyewe iko sita na kwa mujibu wa IMF inasema kwamba wakianza uzalishaji tu wa mafuta kama Uganda uchumi wao utakua mpaka kwa 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri hapa kama Taifa tuwe na mkakati wa kimakusudi tusijikute tunaburuza mkia kwa miaka mitano mingine inayokuja ukilinganisha pengine kwa Afrika Mashariki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda.
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)