Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu. Niwapongeze Mawaziri waliotuonyesha at least framework ya mpango wa muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho kinanitia moyo katika mpango huu ninaona mpango huu unajali ustawi wa maisha ya Mtanzania. Ninawapongeza sana wanaendana na ndoto ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kusema tusilenge tu kwenye miundombinu, tusije tukaishia mpango wetu tunaona tu SGR, flying overs na majumba makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu kwa kulingana na dira unaonyesha kwamba ifikapo 2050 angalau Watanzania wawe na maisha bora na Mtanzania awe na miaka 75 akiwa na maisha yenye furaha. Tofauti na Biblia inavyosema umri wa mtu kuishi ni miaka 70, lakini tena iliyojaa tabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia hapo tunahitaji Watanzania wawe na lishe bora, wawe na huduma bora ya afya kila mtu aweze kufikia huduma bora ya afya ya matibabu, maji safi na salama, makazi mazuri, nishati safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguvu ya kufika hapo hata kwenye dira wametuonyesha, tu kwamba katika mikakati yote hii iliyowekwa kwenye sekta zote za kijamii na za kiuchumi kwamba Pato la Mtanzania litapanda kutoka dola za Kimarekani 1,275 mpaka 7,000, huo ni mkakati mzuri sana kama angalau tutafikia hapo. Ndipo ambapo tunaweza tukamudu kupata haya maisha bora ambayo yanasemwa kwa Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo ili kufikia hizo ndoto za Tanzania kwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi wa juu na pato la Mtanzania kuweza kupanda ili ajipatie maisha bora ndiyo maana tunasema uwekezaji uelekezwe kwenye sekta za kiuzalishaji, uelekezwe kwenye kilimo, uelekezwe kwenye mifugo, uelekezwe kwenye nishati, uelekezwe kwenye madini pamoja na maliasili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuisemea kilimo ni halali kabisa pamoja na kwamba wachangiaji wengi wameisemea. Kilimo ndiyo ajira ya Watanzania; Watanzania wengi wako kwenye kilimo, zaidi ya 65% au 70%, kilimo ndiyo tunapata malighafi ya viwanda kwa 65%, kilimo kinachangia GDP kwa 26% mpaka 30%, kilimo ndicho tulitarajia kupata fedha za kigeni. Kwa hiyo, uwekezaji kwenye kilimo uzingatiwe kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo chetu kina namna ya kuweza kukitazama, kwanza kilimo cha Tanzania kwa sehemu kubwa kinafanywa na wakulima wadogo wadogo kwa 90%, hawa wakulima wadogo wadogo ndiyo wanaotosheleza chakula kwa zaidi ya 128%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha Tanzania katika mnyororo mzima wa thamani lazima kila hatua ufanyike uwekezaji mkubwa sana. Tumesema kwenye hatua ya uzalishaji sababu ya kuwa na uzalishaji mdogo, tumesema ni mvua zisizoaminika kwa hiyo tumeishauri Serikali izingatie kuwekeza kwenye miradi ya umwagiliaji, tumeongelea habari ya pembejeo bora Serikali iwekeze kwelikweli kwenye pembejeo bora, affordable na ambazo watu wanaweza ku-access. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea habari ya huduma za ughani. Huduma za ughani ni muhimu sana hasa kwa wakulima wadogo. Tanzania tuna fursa kubwa sana ukiona duniani, kwanza sisi Tanzania idadi ya watu inaongezeka, lakini duniani tu tuna idadi ya watu inayoenda bilioni nane. Hii bilioni nane ni fursa ya kuilisha, lakini huku duniani pia watu wanao-suffer na njaa ni milioni 828 na huku Afrika milioni 249. Hizo zote ni fursa pengine sisi ni namna gani tunatakiwa kufikia hizo fursa za kuwalisha watu duniani na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema kilimo biashara kama kweli tunataka tusogee kwenye kilimo biashara, hatuna budi sasa hivi kuwekeza kwenye mashamba makubwa large scale farming pamoja na block farming. Serikali itafute mashamba ipime afya ya udongo iwe na hati na kila kitu halafu iwaalike wawekezaji waje wawekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema private sekta kwenye mpango wetu watachangia 70% sehemu moja kubwa ambayo private sekta wanaweza kutusaidia ni kwenye kilimo na kama ni kwenye kilimo wafanye basi mashamba makubwa: mashamba makubwa ni yale ambayo unaweza ukafanya mechanical agriculture, uka-mechanize agriculture. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba makubwa ndiyo yale ambayo tunaweza tukafikia quality ya vitu vinavyotakiwa kwenda nje. Haya mashamba madogo madogo ya wakulima heka moja, heka mbili, mkulima ni anajua kufanya risk management kwenye shamba moja ata-intercrop mahindi, maharage na kila zao. Haya mazao ya namna hiyo pengine kuyatoa nje tunakuwa hatujafikia ule ubora wa kimataifa. Sasa huu ubora wa kimataifa tutapata kwenye hii large scale farming ambapo sasa tayari sisi tufanye lobbying pamoja na mahusiano na nchi za nje tutangulize kupata soko ili tuwaambie hawa wazalishaji watuzalishie kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ninatamani katika vipaumbele vya mradi huu tuendelee kuviangalia viwanda. Nchi zote zilizofanya na zilizokua uchumi kwa kasi kubwa ni waliowekeza kwenye viwanda. Sisi viwanda kongani ya viwanda imekuwepo toka Baba wa Taifa, tunakumbuka tulikuwa na viwanda, tukapata sera ya ubinafsishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine tuliobinafsisha wakati ule viwanda labda hawakuwa Watanzania wazalendo sisi watu wameondoka na mashine na kila kitu kwa mfano General Tire kwetu unajua kiwanda kizuri kabisa katika Afrika Mashariki lakini tumebakiwa na magofu. Hata sasa sera yetu ya viwanda ni rafiki inashawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuiangalie ili kukuza kongani ya viwanda. Ukiangalia soko la kwanza la viwanda vyetu vya ndani ni Watanzania wenyewe ni kwa kiasi gani Watanzania ni wazalendo na wanapenda kutumia vitu vya nchini kwao? Ubora wa vitu vinavyozalishwa huku kwetu nani anapaswa kusimamia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine hatuna skills na knowledge, hatuna wataalam wa kutosha, viwanda vyetu vizalishe vitu ambavyo Watanzania watavipenda, lakini affordability. Vitu vinavyozalishwa huku ndani vinazalishwa kwa gharama kubwa, hebu turudi chini kwenye sera zetu kwa nini vitu vinavyozalishwa huku ndani vinakuwa gharama kubwa, kwa hiyo vitu hivi ni vya kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni malighafi. Viwanda vyote vilivyopo vya wawekezaji vinavyozalisha bati chuma, vioo, chumvi sukari vitu gani, sehemu kubwa ya malighafi inatoka nje mpaka viwanda vya bia. Kimea tu cha kutengeneza bia ukienda breweries tunaagiza kutoka nje. Tuangalie sisi Mungu alivyotubariki na fursa tulizonazo na rasilimali zetu. Sehemu kubwa ya malighafi inayotakiwa kama chuma na vingine vipatikane huku ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni skills; wataalam lazima tuwapeleke nje kuliko na viwanda vilivyoendelea ili warudi huku ndani waje waendeleze viwanda. Viwanda ni sehemu pekee itakayoweza ku-absorb nguvu kazi ya Taifa lakini sehemu pekee ambayo Watanzania wanaweza wakapata kipato cha kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ninaona mpango wetu uweke vipaumbele ni vichochea uchumi na hii inamaanisha miundombinu ya usafirishaji, nishati, teknolojia sayansi, mageuzi ya kidijiti pamoja na utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema miundombinu ya Barabara; barabara imekuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi mahali. Hebu ona sehemu yoyote marginalized ambazo ziko pembeni, usafiri na usafirishaji siku zote uchumi wake umekuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara huko vijijini hazipitiki kabisa, barabara ni zote, hizi feeder roads zinazotoka kijijini kuja kwenye miji midogo haziwezi kupitika mwaka mzima. Kuna sehemu kama kipindi hiki mvua zimenyesha mawasiliano yamekwisha kabisa, mkulima kuchukua mfuko wa mbolea kama amechukua mjini kufikisha mpaka kwake ni zaidi ya 5000, hebu ona gharama kubwa ya uzalishaji, lakini amezalisha mazao yake jinsi ya kuyatoa kule kijijini na kuyaleta sokoni inakuwa tabu hata mnunuzi kufuata yale mazao ya mkulima kwenda kijijini ni shida vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miundombinu ya barabara pengine tungekuwa na ubunifu, kwa huu Mfuko ambao unakusanya fedha kwa ajili ya TARURA, TANROADS tuone namna gani tupate vyanzo vingine, hela ziongezwe huku na barabara zote zipitike mwaka mzima, barabara za vijijini lakini na barabara kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni nishati, tumebarikiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia muda umeisha.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa hiyo, mpango uzingatie upatikanaji wa nishati kwa bei nzuri, lakini pamoja na sayansi na teknolojia na mageuzi ya kidijiti ili kwamba tuweze kwenda na mpango wetu na Dira ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)