Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia. Nami kama ilivyo ada kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu nianze kwa kumshukuru Mungu aliyeniwezesha kupata nafasi hii adhimu ya kuwa mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Geita. Ninamshukuru sana Mungu kwa sababu aliijua siku hii kabla ya kufanyika misingi ya dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais, yeye ndiye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Ninaamini kwa baraka zake alipokuwa akisimamia vikao na teuzi zote aliweza kulipitisha jina langu, ninamshukuru kwa dhati ya moyo wangu. Pia, ninawashukuru Wanawake wa Mkoa wa Geita walionichagua kwa kishindo na kunifanya leo kuwa mwakilishi wao. Ninawashukuru sana na ninawaahidi kwamba nitawatumikia kwa moyo wangu wote na kwa akili zangu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia kwa kuishukuru familia yangu. Wamekuwa wakini-support kwa hali na mali, wameniombea wamenitia moyo. Kwa hiyo, sina budi kuwashukuru na ninasema ahsante sana na mimi nipo kwa ajili yao sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninapoelekea katika kuchangia ninaomba niwaelekeze katika suala moja la elimu ya amali. Elimu ya Amali ni jambo ambalo ni geni. Limeletwa kwetu katika huu mtaala mpya ambao umeboreshwa, lakini jambo hili likifanyika kwa jinsi ambavyo limeratibiwa litakwenda kuleta matokeo makubwa sana katika Nchi yetu ya Tanzania. Kwa nini litakwenda kuleta matokeo makubwa katika Nchi ya Tanzania? Kwa sababu itakwenda kugusa vijana wengi wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea ninaomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa mwasisi wa kwanza na ndiye aliyetoa agizo kwamba mtaala uliokuwepo ufanyiwe marekebisho na uwekwe mtaala ambao utatoa elimu ya amali ili vijana wengi wa Kitanzania na wananchi kwa ujumla waweze kupata mafunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo hilo alipokuwa akihutubia Bunge tarehe 22 Aprili, 2021 na leo tunaona hata tunapokuja kujadili dira lakini Mheshimiwa Rais alikuwa na maono ya mbele. Aliliona jambo hili mapema hata kabla hatujatengeza dira hii ya muda mrefu wa 2026 mpaka 2050. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais. Tunatambua mchango wake na maono yake kwa vijana wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana kwamba taifa lolote ambalo halishirikishi vijana haliwezi kufanikiwa na kama tumeamua kuwa na uchumi jumuishi ni lazima tuhakikishe tunakwenda na vijana wetu. Sasa mtaala huu umelenga kuhakikisha watoto wanaosoma elimu ya sekondari wanaanza kupata elimu ya mafunzo na hivyo mtoto anapomaliza kidato cha nne anaweza akajiajiri au akaajiriwa endapo atakuwa amechagua mkondo wa amali. Kwa hiyo, hili ni suala muhimu sana na ambalo litakwenda kutupatia maendeleo katika Taifa letu na litakwenda kutatua changamoto ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Mheshimiwa Rais alipoiagiza Wizara ya Elimu, imetekeleza na imekwishaanza kutekeleza mtaala huu kwa kupitia vyuo vya ufundi vya VETA. Mkakati uliopo, Wizara ya Elimu inakwenda kujenga vyuo vya VETA kwa kila wilaya. Sasa kama tunakwenda kupata vyuo vya VETA katika wilaya, ninaamini huu utakuwa ni mwarobaini wa kutatua changamoto ya ajira kwa watoto wetu na watoto wetu wanakwenda kujiajiri na wanakwenda kupata fursa mbalimbali zikiwemo fursa za ujasiriamali, viwanda na fursa mbalimbali za ajira kwa sababu hata katika mafunzo wapo ambao wanaajiriwa na wanaajirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana kwamba mfumo wetu wa elimu ulikua ni mfumo ambao ulikuwa umekaa katika eneo la pembetatu (pyramid). Watoto wengi walikuwa wakianza huku chini wanaanza wengi, lakini inaenda inawachuja. Huyu amefaulu anaingia sekondari, huyu anachujwa tena anaingia form five na six, anachujwa tena anaingia chuo kikuu, lakini mfumo huu unakwenda kuwajumuisha na kuwapa fursa watoto wote wa Kitanzania na watoto hawa watakapopata elimu na mafunzo haya hatutamwacha mtoto nyuma hata mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivi tunakwenda kukomesha matatizo ya dawa za kulevya, tunakwenda kukomesha changamoto za watoto kutumia mitandao ya kijamii vibaya kwa sababu watoto wetu watakuwa busy, watakuwa wameji-keep busy katika kufanya shughuli mbalimbali za mikono na ambazo zinawapatia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kutoa mchango wangu kwa mambo machache ambayo ninaishauri Serikali iyaangalie ili kuweza kufanikisha mpango huu muhimu sana ambao utatusaidia kuendeleza na kuleta matokeo makubwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niombe Serikali iweke bajeti ya kutosha ili kuhakikisha kwamba shule za VETA zinajengwa kama walivyotuahidi katika kila wilaya nchi nzima. Kwa hiyo, litengwe fungu, lakini pia tuhakikishe kwamba tunapata walimu wa kutosha na walimu walio wabobevu. Kwa hiyo, Serikali itunze pesa za kutosha ili tupate walimu ambao watatusaidia kuwekeza ujuzi unaohitajika kwa watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, niombe kwamba watoto hawa wanakwenda kumaliza kwa wingi sana. Ikiwa kila wilaya itapata shule ya VETA tutakuwa na watoto wengi sana wanaomaliza kwa muda mfupi. Tusipoweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha kuwapatia mitaji muda siyo mrefu tutapa tena janga lingine la vijana kuwa mtaani wana ujuzi lakini hawana mitaji. Kwa hiyo, niombe Serikali iweke pia bajeti ili kuwasaidia vijana hawa wanaomaliza katika elimu hizi za mafunzo ya amali waweze kupata mitaji na waweze kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuishauri Serikali ni kwamba mafunzo haya yatolewe kwa kujali mahitaji ya kieneo, kwa mfano, ninatoka katika Mkoa wa Geita. Kule tuna wachimbaji, wakulima, na wafugaji. Sasa tunapoweka VETA pale katika Mkoa wetu wa Geita, nishauri tuangalie course ambazo zitasaidia kuleta manufaa katika eneo husika katika kila wilaya. Kwa mfano, pale Geita tuna Mgodi mkubwa wa GGM ambao unatoa fursa za ajira nyingi. Kwa hiyo, Chuo cha VETA kitakachokuwa katika mkoa wetu pale na katika wilaya yetu kihakikishe kwamba kinawatengeneza vijana kwa kuangalia mahitaji yanayohitajika au course zinazohitajika katika mgodi ili vijana waweze kujiajiri katika mgodi huo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa malizia muda wako umeisha.
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuwapongeza Wizara ya Elimu kwa utekelezaji mkubwa wa elimu hii ya amali na niwaombe waitangaze fursa hii ya chuo cha VETA kwa wananchi. VETA imekuwa ikidharaulika kwamba ni elimu ambayo inachukuliwa na watu ambao hawakufaulu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu waitambue na waweze kujiunga na elimu ya VETA. Ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)