Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kusimama hapa mbele kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2026/2027. Mpango uliokuwa na dhima kubwa ya kuinua uchumi wa Nchi yetu ya Tanzania na kutimiza maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, ninasimama kwa mara ya kwanza, ninaungana na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia uzima na afya kufika siku ya leo. Pia, ninatumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuniamini mimi Asha Salum Motto kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Tatu, 2025 - 2030. Aidha, ninawapongeza viongozi wote waliopo ndani ya Bunge hili tukiongozwa na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu ninatumia fursa hii kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Mtwara, hasa wanawake, kwa kuniamini mimi kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili Tukufu. Pia, ninatumia fursa hii kuwashukuru viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi na wa Serikali pia, kwa kuwa pamoja na mimi kipindi chote tulichokuwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia fursa hii kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi wa kishindo wa takribani 97%. Haikuwa bahati mbaya kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kushinda, watu waliona kazi alizozifanya kwa miaka yake yote minne. Hakuna mradi ambao ulisimama, shule ziliendelea kujengwa, vituo vya afya viliongezeka kwa hiyo, hakupata zile kura kwa bahati mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitomshukuru Mwenyekiti wangu wa UWT Taifa, Mheshimiwa Mary Pius Chatanda. Mama huyu ni mtu na nusu, amekuwa akimsaidia sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuunganisha sisi wanawake wa Tanzania, hususan wanawake wa Mkoa wa Mtwara. Unaweza ukaona ni namna gani Bunge hili la Kumi na Tatu asilimia ya wanawake imeongezeka. Hii ni kazi kubwa ya hamasa aliyoifanya Mheshimiwa Mary Pius Chatanda kutuhamasisha sisi wanawake, kutuweka pamoja na kutujengea uwezo wa kutokuogopa kugombea nafasi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nijielekeze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Sekta ya Nishati. Kama inavyofahamika, Mikoa ya Kusini sisi ni matajiri; Lindi, Mtwara na Ruvuma ni matajri wa gesi na makaa ya mawe. Jukumu letu kubwa ni faida zinazopatikana na miradi hiyo zianze kwanza kufaidiwa na Wazawa wa Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti za Kituo cha Lindi na Mtwara zimebaini uwepo wa gesi asilia takribani 32%, mbali na ule Mradi wa TPDC-Mtwara. TPDC-Mtwara inafanya kazi kubwa ya kusambaza mtandao wa gesi majumbani na mpaka sasa kwa takwimu iliyopo imesambaza kati ya kaya 491,811. Mkoa wa Mtwara una kaya 491,811, kaya 373,172 ziko vijijini, sawa na 75.9% na kaya 118,639 sawa na 24.1% ziko mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TPDC linaloendelea kutekeleza miradi ya usambazaji wa gesi asilia nchini hadi sasa imesambaza kaya 428, ukiangalia tofauti bado idadi ya kaya zilizobaki kufikiwa na mradi huo ni nyingi, ninaishauri Serikali kuongeza nguvu ili mtandao huu wa mabomba ya gesi uweze kufika kwenye kaya nyingi zaidi na kufikia malengo ili wananchi wa Mkoa wa Mtwara waweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuona pia TPDC imefanikiwa kusambaza mtandao wa gesi katika taasisi nne (4) kati ya taasisi 108. Hii inaonesha kwamba bado kasi ni ndogo ya mradi huu, kwa hiyo wajitahidi ili taasisi zilizobaki na zenyewe ziweze kufanikiwa. Ukiangalia taasisi hizi ziko mjini, nasi ukiangalia kaya nyingi zinatoka vijijini, kwa hiyo TPDC na Wizara husika wajitahidi wahakikishe na wale wa vijijini wananufaika na mradi huu kwa kuwa tumeshaona gesi inatoka Mtwara inaenda Dar es Salaam, inatoka Dar es Salaam inaenda na mikoa mingine, ukiangalia takwimu ya TPDC unaona kabisa labda mikoa ile mingine ina asilimia kubwa ya kaya walizopata hii gesi kuliko mkoa wenyewe ambao ndiyo tunazalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa CNG, hii ni gesi asilia iliyoshindiliwa. Hapa nchini kwa sasa kuna vituo 14 vinavyouza gesi kwa ajili ya matumizi ya vyombo vya usafiri wa magari na bajaji. Mkoa wa Mtwara una kituo kimoja tu ambacho kipo maeneo ya Dangote na hiki ni kituo cha Dangote kwa shughuli yake ya kusafirisha saruji yake, wananchi wa Mkoa wa Mtwara hawanufaiki na hiki kituo. Kwa hiyo ninaiomba Serikali ione haja ya kwenda kuwekeza kituo ambacho kitawasaidia wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Kusini kwa ujumla kubadilisha mfumo wa magari kutoka kwenye diesel au petrol kutumia gesi ambapo pia itawasaidia kupunguza gharama ambazo wanazitumia sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya idadi ndogo ya kaya zilizounganishwa na gesi asilia majumbani hapa Mkoa wa Mtwara. Ninashauri Serikali kuongeza kasi ya uunganishaji wa kaya hizo pamoja na kuboresha miundombinu ya usambazaji wa mabomba ya gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kusini hasa Mkoa wa Ruvuma kuna makaa ya mawe, makaa ya mawe haya yanatoka Ruvuma yanakuja bandari ya Mtwara, tuna depot ambayo ipo kulekule bandarini na Bandari ya Mtwara iko mjini, athari tunayoipata Mtwara kwa makaa ya mawe kwa kweli ni kubwa sana na sijui kizazi kijacho itakuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia fursa hii kuishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga bandari kubwa kule Mgao, bandari iliyogharimu takribani shilingi bilioni 434 na bandari hii itakuwa ya kisasa na ya kwanza kwa ukubwa Tanzania.