Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kuridhia mimi kusimama hapa leo. Ninachukua pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupendekeza jina langu Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Halmashauri Kuu ya Taifa na hatimaye kwenda kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru Magharibi kwa kumchagua Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, ninawashukuru wananchi hao kwa kuwachagua Madiwani wote wa Jimbo la Arumeru Magharibi kuwa Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi hawa wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi ninawashukuru sana kwa imani kubwa waliyonayo kwangu wakanichagua kwa kura nyingi sana kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Arumeru Magharibi. Wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi ninawahakikishia imani waliyonipa sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho katika shukrani, ninapenda pia kuchukua nafasi hii kuishukuru sana familia yangu hususan mke wangu kwa kipindi chote cha harakati kuhakikisha kwamba yupo na mimi katika masuala mengi hususan kuniombea Mwenyezi Mungu, ilikuwa siyo rahisi. Mama ninakushukuru sana kwa jitihada zako na ninakuombea na wewe Mungu aendelee kukulinda na kuweza kwenda kuona matunda ambayo wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi wataenda kuyapata kupitia uwakilishi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sina fadhila nisiposhukuru uwekezaji mkubwa ambao Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika Jimbo la Arumeru Magharibi. Zaidi ya shilingi bilioni 69.9 ziliwekezwa katika Jimbo la Arumeru Magharibi, ikilenga kwenda kushughulikia changamoto za afya, elimu (elimu sekondari na elimu msingi), nishati (umeme) na miundombinu ya barabara. Ninajua bado tuna changamoto kubwa katika Jimbo la Arumeru Magharibi ikiwemo changamoto ya miundombiunu ya barabara, changamoto ya miundombinu ya maji na Sekta ya Umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kumshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchagua kwa umakini wasaidizi wake ambao waliendelea kufanya kazi kubwa sana. Tukianza na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninamshukuru ametembelea na nimemweleza mambo mengi katika Jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni alitembelea Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa. Yule ni Waziri wetu wa Afya na amezindua, siyo tu bima ya afya lakini mpango au Programu ya Ongea na Waziri wa Afya, yaani Mtanzania wa kawaida unaongea na Waziri anakujibu pale pale. Ile itaenda kutusaidia katika suala la Bima ya Afya kwa Wote, watu wataelezea matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwona Mheshimiwa Reuben Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI alikuja, lakini pia kuna Mheshimiwa Ulega, Waziri wa Ujenzi na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI aliyeko upande wa ujenzi. Hawa Waheshimiwa wote walipokuja niliwaeleza changamoto za Jimbo la Arumeru Magharibi na wamesema wataenda kufanyia kazi. Ninamshukuru sana sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa umakini na upendo kwa watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nichangie Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ilivyowasilishwa. Mpango unaelekeza kuchukua hatua 10. Kwa sababu ya muda nitachangia kidogo, kidogo sana hatua ya nne na kama utaridhia ninaomba ninukuu. Inasema hivi: “Kutokana na muda ...” ninarudia tena kunukuu. Inasema hivi; “Kulenga kuwa na kituo kinara cha Utalii wa Tiba ambacho kitaboresha ubora wa maisha ya Watanzania wote na kitakuwa na sekta ya afya kama engine muhimu ya maendeleo na uchambuzi wa Kimataifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili haya yatokee sasa, kutekeleza hii hatua ya nne Taifa liwekeze katika huduma ya kinga kuliko kuwekeza katika huduma ya tiba. Uwekezaji wa kutosha kwenye huduma za kinga una manufaa makubwa sana katika Taifa. Kinga inasaidia kupunguza gharama kubwa ya tiba. Kinga inasaidia kufanya Taifa kuwa lenye nguvu kwa sababu watu wanakuwa wanafanya kazi. Tunakuwa tuna uwezo mkubwa kushiriki shughuli za kiuchumi hususan uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinga inasaidia pia hata ile tiba kuwa rahisi, kwa sababu watakaokuwa wanaugua ni wachache. Kwa hiyo, watu wanapata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende sehemu ya pili kwenye hilo. Kuna utoaji wa huduma nchini na mgawanyiko wa rasilimali. Vituo vya kutolea huduma Tanzania hii ni vituo 13,774. Hiyo inajumuisha maabara binafsi na kliniki mbalimbali, lakini kati ya hizo, vituo vya kutolea huduma (zahanati, vituo vya afya na hospitali) ngazi mbalimbali vinafika 10,588. Kati ya hizo tena, vituo 7,689 sawa na 85% ziko chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Primary Health Care) na hizi ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mgawanyo wa rasilimali kama alivyoelezea ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mahera hapa, fedha nyingi zinabaki katika sehemu ya uratibu. Wale watu wengi ambao tumesema ni 73% wanapata sehemu kidogo. Kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kuangalia namna ya kugawa rasilimali hizi kwa kufuata formula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendeeza labda tutumie formula ya Mfuko wa Pamoja ambao tunasema kwamba ni Basket Fund ambao unaweza ukasaidia kugawa rasilimali hizi hususan rasilimali fedha, ili wale wananchi wengi walioko vijijini waweze kupata huduma bora za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumalizia kwamba, tukiwekeza kwenye kinga hususan suala la chanjo, suala la uchunguzi tunaita Screening ambayo inasaidia kutambua magonjwa kabla hayajafika mbali au kwa hatua za mwanzo ambazo zinaweza zikapata tiba zinaweza kusaidia kuimarisha maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo ninaomba kusema kwamba ninaunga mkono hoja. Mungu ibariki Tanzania na Mungu libariki Jimbo la Arumeru Magharibi. Ninakushukuru sana. (Makofi)