Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Neema Peter Majule

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi na nimefurahi sana kumfuata kijana kuongea, maana kijana amejikita kwenye mambo ya vijana mpaka wote tumefurahi na hii ndiyo sura ya Bunge lako lina wawakilishi wa kila sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya kutusaidia na kutuwezesha kutupa Mawaziri pamoja na Manaibu Waziri ambao wamekaa kwenye Wizara hizi na hata kuweza sasa kutoka na Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka 25. Moja kwa moja niipongeze Wizara ya Mipango na niipongeze Wizara ya Fedha: Mpango uliopita wa miaka mitano ulikuwa mzuri umetusogeza mpaka tulipo na kweli maendeleo makubwa yamefanyika nchi za Kiafrika zinashangaa, dunia pia nayo inashangaa kwa maendeleo makubwa ambayo Tanzania imeweza kupiga kwa miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumepata Mpango mwingine ambao kama wanavyosema wenzangu na walivyounga mkono ya kwamba Mpango huu ni wa Kisayansi na Kiteknolojia: Mpango ambao unaweza kutupaisha tukaenda mahali pazuri zaidi, lakini tuna Mpango huu wa muda mrefu sasa wa miaka 25 na huu Mpango wa miaka mitano, halafu tumepewa Mpango wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchambuzi wangu mimi nataka kuchangia nafasi sasa ya mwanamke katika Mpango huu. Nimeupitia Mpango na kuweza kuona nafasi ya mwanamke, Wabunge wengi wamechangia mambo mbalimbali na wamegusa kwa namna moja au nyingine mambo ya wanawake katika Mpango huu. Hata hivyo, ninataka niseme kwamba, wanawake tumepaishwa zaidi kipindi hiki cha kuwa na Rais, Mwanamke Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mpango huu ambao tumeletewa wa miaka 25, pia wanawake wamepewa nafasi kubwa sana. Lakini niseme tu kwa nini nimekuwa na interest hiyo, kwanza, kwa sababu mimi zaidi ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, mimi pia ni Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake idadi yetu sisi ni 51% population ambayo tumehesabiwa mwaka jana 2025, lakini pia ndiyo wazalishaji wakubwa na ndio wanaoweza kuupeleka uchumi huu kutoka hatua hii kwenda hatua nyingine. Kwa sababu wanawake wamejikita zaidi kwenye kilimo, asilimia kubwa ya wakulima ni wanawake na pato la Taifa ambalo linachangia ni 54%, ambao watendaji wakubwa kwenye field ni wanawake. Hivyo basi, hatuwezi kutenga maendeleo makubwa ambayo tunayatarajia pasipo kuwahusisha na kuwaongelea wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wanawake wamejikita kwenye biashara ndogondogo ikiwepo biashara za kati (SME), kwa hiyo ni wanawake ndiyo waliofanya. Wanawake pia wamejikita kwenye kazi za huduma za jamii, hivyo basi niseme kwamba, Mpango huu ambao tunao, tutaenda vizuri tukiwa kwenye usawa wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipendekeze moja kwa moja nisije baadaye mwishoni nikashindwa vitu vya kupendekeza. Niseme basi Mpango huu kama tutaweza kuenenda ukiwa na mlengo wa usawa wa kijinsia viwekwe moja kwa moja viashiria mahususi vya kijinsia katika Mpango mzima, lakini pia kwenye bajeti, yaani kuwe na indicators ambazo ni mahususi kabisa za kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, ushiriki mzima wa wanawake kuanzia kwenye Mpango, lakini pia kwenye ufuatiliaji kwa maana ya monitoring, lakini pia kwenye tathmini. Kuwepo na ushiriki wa wanawake kwenye stage zote hizo kuanzia kwenye mipango; kwenye utekelezaji mpaka kwenye tathmini. Tukienda kwa pamoja hivyo, ninaamini kwamba tunaenda kufikia haya malengo vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niseme kwamba, uchumi jumuishi ambao tumeamua kwenda nao kwa sasa hivi utaenda kuinua mapato yetu ya Taifa mpaka dola za Kimarekani trilioni moja, lakini pia pato la mtu mmoja mmoja linaenda kwenye dola za Kimarekani 7,000 ifikapo 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yatatokea tu kama tutaongeza fursa za ajira kwa wanawake: wanawake ndiyo ambao ni wazalishaji, lakini siyo hivyo, tutaweza kujikwamua tu kwa kupunguza umaskini kuanzia ngazi ya kaya au kuanzia ngazi ya familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini ukiuongea kati ya mwanamke na mwanaume aliye masikini zaidi ni mwanamke kwa sababu ya mila zetu na desturi ya kwamba kwenye ngazi ya kaya mmiliki wa mali ni mwanaume na utaweza kuona haya mara mwanaume anapoondoka duniani yule mwanamke hawezi kuruhusiwa kumiliki ardhi aliyonayo pale inachukuliwa na familia ya mwanaume. Kule alipotoka kwenye familia yake hajapewa ardhi, huku alipoolewa nako hapewi ardhi, hivyo umaskini wa mwanamke ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kwenda kwa pamoja basi tulenge kuzikwamua kaya ambazo mara nyingi zinakuwa headed au zinakuwa zinaongozwa na wanawake, huko ndiko ulipo umaskini. Kama tutakuwa na Mpango mzuri wa kuwakwamua wanawake kwenye ngazi ya familia, moja kwa moja tutakuwa tumefanikiwa kulikwamua Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mambo ya elimu; kama tutaweza kutoa elimu kwa wasichana vizuri kabisa, tunawapanua wasichana uwezo kama unavyoona Mheshimiwa Magreth ame-present pale, uwezo wake umepanuka, msichana huyu amepewa elimu. Hivyo basi tunaweza kumkwamua, tunaweza kuwakwamua wanawake kuanzia kuwapa elimu ya kutosha kuanzia wakiwa wadogo. Mpango huu umeonesha tunaongeza idadi ya shule za sekondari na ushiriki wa wasichana kwenye elimu ya sekondari na tunaongeza pia hata teacher-student ratio kutoka 105 kwa Mwalimu kwenda wanafunzi 40 kwa Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo itasaidia kuongeza fursa ya elimu kwa wasichana na tutawaongezea wasichana sasa uwezo wa kushiriki kwenye biashara za ushindani. Siyo hivyo tu, tunapoenda kuangalia mambo haya moja kwa moja tunapoongelea mwanamke tunaongea juu ya mwanamke na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumefanikiwa sana kupunguza vifo vya wanawake na Watoto wachanga. Mpaka sasa hivi ni vizazi 104 tu katika 1,000 wanawake wanaopoteza maisha. Mpango huu unaenda kupunguza vifo hivi mpaka vizazi 85 tu kati ya vizazi 1,000, lakini inapunguza vifo vya watoto kuanzia 33 hadi 27. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa nini sasa? Ni kuzidi kuwekeza zaidi katika sekta ya afya ili tuendelee kuboresha maisha ya wanawake na Watoto, lakini siyo hivyo huduma za dispensary zinapoanzishwa na vituo vya afya zilenge kuwapa ajira nyingi zaidi wanawake kwa maana ndiyo watoa huduma za kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutaweza kufaulu sana kuwanufaisha wanawake kwenye huu Mpango wetu wa miaka 25, lakini Mpango wetu wa miaka mitano ambao moja kwa moja umejikita kupunguza umaskini. Pia tutaweza kufanikiwa kwa huu Mpango wetu wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe mapendekezo yangu, zaidi ya kuongeza indicators kwenye kila Mpango na pia na bajeti, lakini pia fedha za mikopo za wanawake ziongezwe kwenye bajeti, ambayo itatengwa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Tunashukuru sana kwa mchango mzuri. Muda umekwisha malizia sentensi ya mwisho.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)