Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili nichangie katika Mpango huu wa Taifa wa Maendeleo. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijalia uhai na afya njema lakini pia niendelee kuwashukuru wananchi wema wa Jimbo la Kahama Mjini ambao walinichagua na kuniamini ili nije kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia familia yangu kwa maana ya mke wangu Happiness Kalugaba, lakini na Mama Gaudensia Ngayiwa na Mzee Ngayiwa Pascal Maziku na ndugu na jamaa wote wanaoendelea kunitia moyo katika kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze sasa katika kuchangia mapendekezo ya Mpango huu elekezi wa maendeleo wa muda mfupi, muda wa kati na mrefu. Niseme tu kwamba Mpango huu umetambua rasilimali zetu ambazo tupo nazo katika Nchi yetu tukufu ya Tanzania. Rasilimali hizo ni uoto wa asili; ardhi kubwa ambayo ina rutuba inayo support kilimo cha aina zote kwa maana ya mazao ya chakula na mazao ya biashara, lakini tuna water bodies ambayo ni mito; maziwa lakini na bahari ambayo yote haya yana support shughuli za uvuvi na kilimo lakini na matumizi mengine ya nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu hapa, ninaamini Serikali yetu ambayo inaongozwa na Mheshimiwa mama yetu Rais mpendwa Mama Samia, ipo na nia thabiti na ya dhati katika kuwatumikia wananchi wetu. Kwa hiyo, hapa nishauri tu katika mikataba ambayo inajumuisha rasilimali zetu hizi nilizozitaja basi ipitie katika Bunge hili ili Wabunge tuweze kutoa ushauri wetu kwa sababu mikataba inayohusu rasilimali, inahusu pia kizazi chetu na dira hii ya maendeleo ya miaka 25, tunapoongelea mtoto wa miaka mitano, leo baada ya miaka 25 kufikia 2050 atakuwa ni mtoto mwenye miaka karibu 30. Sasa tunakuwa na Mpango huu wa maendeleo ambayo kwa kweli umelenga katika kuendeleza kizazi chetu ambacho kitakuja kunufaika na rasilimali hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mpango huu wa maendeleo umeweka vichocheo vya maendeleo ambavyo ni imetambua kuhusu nishati, logistics kwa maana ya uwekezaji katika miundombinu lakini sayansi na teknolojia, mageuzi ya kidijiti, mazingira ya biashara na uendelezaji wa uwekezaji katika kuboresha mifumo ya kisheria na kukuza ubia kati ya sekta za umma na sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa niseme tu kama wachangiaji waliotangulia kuchangia, idadi ya vijana kwa maana hawa ndiyo wabeba maono na watekelezaji wa huu Mpango wa Maendeleo wa Muda Mfupi, Muda wa Kati na Muda Mrefu. Hawa vijana kati ya umri wa miaka 15 na 35 ni zaidi ya 60% na hawa ndiyo nguvu kazi: kwa maana wale watoto na wazee ni tegemezi kwa nguvu kazi hii. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie sera na mpango wetu katika kuwawezesha vijana wetu, waweze kuingia moja kwa moja katika kutumia hizi rasilimali nilizotaja hapa ikiwemo madini; ikiwemo rasilimali zetu za ardhi, lakini na maji ambayo tupo nayo katika mito, maziwa na bahari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali kupitia Wizara na ninashukuru kwamba Wizara ya Vijana imeanzishwa, kwa hiyo tuweke sera ambazo zitaenda kuwawezesha vijana wetu kwa mitaji, lakini kuwawezesha vijana wetu kwa skills kwa maana ya teknolojia ili waweze kuhimili ushindani wa kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliposema kwamba tuboreshe miundombinuā¦
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Jimbo langu la Kahama Mjiniā¦
MWENYEKITI: Mheshimiwa Benjamin, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Nilitaka kumpa taarifa mchangiaji, anachangia vizuri kabisa kwenye kuishauri Serikali jinsi ya kuhakikisha kwamba vijana ambao ndiyo nguvu kazi wanawezeshwa kuhakikisha kwamba wote wanakuwa ni wazalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu za sasa hivi 87% ya population tuliyo nayo ni tegemezi, kwa maana watoto chini ya miaka 15 na wazee kuanzia miaka 65. Kwa hiyo, wazalishaji tu ni 13%, sasa Serikali ikichukua hizo takwimu ikazifanyia kazi kwa vile anavyosema mchangiaji pale ni hakika sasa hii percent ndogo ambao ndio wazalishaji ambao ndiyo wanabeba jukumu kubwa la kuwasaidia hao wengine ambao ni tegemezi itasaidia kukwamua hilo eneo ambalo linategemea sana 87%.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Benjamin, taarifa ya Mheshimiwa Matiko, unaipokea?
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea na ninaomba niendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongea hapa kuhusu uboreshaji wa miundombinu, lakini na mazingira ya kibiashara. Pale Jimboni kwangu Kahama ni jimbo zuri na lina watu ambao wanajituma sana katika kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iwawezeshe wafanyabiashara pale ambao Mji wa Kahama ni kama lango la kuingia na kutokea katika nchi yetu ambayo inaunganisha Nchi zaidi ya nne; tunaunganisha Burundi, Rwanda, Kongo, Sudani na Uganda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale ningeomba sana wafanyabiashara wale wawezeshwe kwa mitaji, lakini na zile kodi, sipingi kwamba Serikali ikusanye kodi, lakini tuangalie namna ya kuwawezesha wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale pia kuna ujenzi wa ghala la biashara kwa maana ya kuweka kitovu cha kuuza mazao ya biashara na chakula nchi jirani. Ninaomba lile soko liweze kumaliziwa, lakini na miundombinu kama ambavyo Mheshimiwa Rais, alieleza katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge, kwamba ipitike muda wote wa mwaka mzima wa kiangazi na masika, basi twende kuiboresha ili wananchi wetu waweze kusafirisha mazao yao kutoka sehemu nyingine na kufanya biashara bila bugudha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, wawekezaji kupitia EPZ na SEZ wawezeshwe wapunguziwe masharti ili waje nchini waweze kuwekeza. Pale Kahama tuna kongani ya viwanda pale katika Mgodi wa Buzwagi. Wawekezaji wapunguziwe masharti waje wafungue viwanda, waweze kuzalisha ajira kwa vijana wetu na hapo Serikali inaweza ikaanza kukusanya kodi kwa maana ya kwamba zile raw materials wanazozitumia, lakini na huduma nyingine kwa maana ya service levy, watakuwa wameweza kulipia na wakati huo huo wakiwa wameajiri sehemu ya vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waache kucheza mabonaza vijana wetu, kwa sababu mabonaza haya kwanza ninapendekeza hata Serikali iangalie kuyatokomeza kabisa, yasiwepo katika nchi yetu ya Tanzania. Mabonaza haya yamekuwa tu mufilisi kwa vijana na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)