Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo na mimi kuwa mchangiaji wa mwisho wa taarifa ambazo zimewasilishwa ndani ya Bunge hili Tukufu. Hii imetokana na maono yako licha ya kwamba, ilihitajika tujadili Novemba, lakini uliona Bunge hili la Januari – Februari tujadili Mipango ya muda mrefu, Mipango yetu ya miaka mitano ijayo na mapendekezo ya Mpango mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mungu. Nakupongeza na kuwapongeza waliowasilisha taarifa mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na pia, Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajielekeza kwenye programu za kielelezo, na hasa kwenye Mji wa Ekolojia ya Bahari ya Usafirishaji wa Kimataifa, Bagamoyo. Kwa nini nimeona niliunge mkono hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu, baada ya kuona mapinduzi makubwa yaliyofanywa katika uboreshaji wa bandari zetu, Bandari ya Dar es Salaam na ya Tanga, namna ambavyo zimechangia ongezeko la mapato, kwa taarifa inavyosomeka, Bandari ya Dar es Salaam baada ya kuboreshwa na kuweka mbia (DP-World) imeongeza mapato kiasi cha shilingi trilioni moja na bilioni 200 zinakusanywa kutoka shilingi bilioni 800 iliyokuwa inakusanywa kila mwezi na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaamini mradi huu ambao una miradi shikizi nane, na ni kwa mara ya kwanza kwa kweli hatua hii. Alipokuja Mheshimiwa Waziri Kitila katika ile miradi shikizi, miongoni mwao likiwemo eneo la viwanda na kuwakabidhi wawekezaji saba, lakini niliwiwa na hatua ya Serikali ya kuwawezesha hawa wawekezaji kuwapunguzia gharama ya ardhi kwa kuwapa hati bila ya ununuzi. Hatua hiyo imekuwa kivutio na ni mara ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu ni kama nilivyochangia siku za nyuma kwamba, kwa kuwa mradi huu utakuwa na miradi shikizi ikiwemo reli ya kisasa, ikiwemo upanuzi wa barabara ya Tegeta – Bagamoyo kwenda Tanga njia nne, ikiwemo barabara ya lami, ikiwemo pia na kufangamanisha eneo la viwanda lililojengwa kwa maono ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Awamu hii ya Sita, Kwala, na limeanza kufanya kazi na tija yake tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali katika kuhakikisha kwamba hii miradi ya kielelezo inaenda kutekelezwa, ihakikishe wananchi wa maeneo hayo, yale mahitaji yao, ikiwemo fidia na hapa ninaisemea lile eneo la Liganga na Mchuchuma, wameshakamilisha. Hata hivyo, bado eneo la Lindi la LNG, maeneo haya ya Bagamoyo na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika uwezeshaji kuhakikisha tunafikia uchumi wa kati wa kiwango cha juu, na uwezeshaji wa wananchi, kama ambavyo hii mipango imesema, ninaishukuru Serikali, imekuwa ikifanya tathmini, hususan katika suala zima la mikopo ya halmashauri. Tulikotoka ni mbali, tulikotoka tulishuhudia mikopo hiyo ikipelekwa kwenye vikundi hewa na ndiyo maana Serikali ilisimamisha kwa kipindi cha mwaka mmoja ikaja na tathmini, ikaja imejipanga vizuri. Kana kwamba haitoshi, imekuja na mfumo sasa wa kuomba mikopo hii kupitia mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu katika hili, tumeona ziko fedha tumetenga katika halmashauri, katika dhima ile ile ya kumwezesha mwananchi na katika hatua ile ile ya kuzalisha ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ifanye mfumo ule kuwa rafiki. Mafunzo kwa wananchi wetu: wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na hasa hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika maeneo yetu mbalimbali; uwepo wa vifaa vya TEHAMA katika halmashauri zetu na maeneo ambayo yatakuwa rafiki, ili makundi haya yaombe hii mikopo isiyokuwa na riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninaona hii hatua, tumeanza utekelezaji wa miaka hii mitano ya Mpango huu kuelekea 2026/2027 – 2050/2051 pale ambapo tumeona utoaji wa shilingi bilioni 200; jana tumemwona Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa mgeni rasmi amekabidhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba katika utekelezaji wa hizi shilingi bilioni 200 za Mheshimiwa Rais, ambazo zimetolewa, na ameonesha anatenda, kuwe na mpango mahsusi, tujue kila wilaya ni benki gani zitahusishwa? Wizara zinazohusika zisimamie kikamilifu, ili kusiwe na usumbufu wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hizo fedha, tumeona namna gani Serikali imejipanga, hata kupitia hizo fursa nyingine, kwenye benki mbalimbali. Ufafanuzi ambao umetolewa leo na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, hata maelekezo ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kuhakikisha kwamba urasimu unatolewa, ili ahadi zilizotolewa zitekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hilo pia, tumeona Mpango huu wa miaka minne utahitaji shilingi trilioni 474, sehemu ya 70% ni Sekta Binafsi. Ninaungana na Waheshimiwa Wabunge waliosema ni namna gani Serikali iende kusimamia mkakati ule wa Blueprint, ili uweze kuleta tija. Pia, kuendelea kuweka vivutio vile ambavyo vina tija zaidi, kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi, kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania, ili lengo la Serikali la 30 ya kuwezesha mipango hii litekelezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuendelea kuhakikisha inatumia ile taarifa ya Sensa ya Mwaka 2022 ambayo ilikuwa ya aina yake, ilihakiki majengo yetu, ambayo nayo ni miongoni mwa chanzo cha uhakika. Vilevile, Serikali kupitia mamlaka zake mbalimbali, kubuni vyanzo vipya vya mapato, ili tuweze kuratibu na kusaidia mipango hii kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Niseme wazi, tunapoenda kwenye Mpango mwingine wa Miaka Mitano, tunajivunia mafanikio ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ambapo mafanikio yameainishwa hapa, katika sekta mbalimbali. Tunawiwa na kuona sasa Serikali imekuja na miradi ya vielelezo, imekuja na miradi shikizi na ni mipango ya aina yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta nzima ya madini ninaipongeza Serikali yetu na ninaipongeza Serikali na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba, yeye ni sehemu ya Bunge. Bunge lina sehemu mbili, Rais na Bunge lenyewe. Kwa hiyo, tuna kazi ya kuishauri na kuisimamia. Sasa mtu unayemshauri, ukiona mambo yametekelezeka, ni wazi lazima utampongeza na kumtia moyo, lakini utaweka mambo mengine Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema kwenye suala zima la madini, tumeona namna gani Serikali kupitia wawekezaji binafsi imeanza ku-support jambo la kurusha ndege na kufanya uhakiki kutoka eneo la 16% kuelekea eneo la 50% mwaka 2030. Ni imani yangu mipango iliyoko itatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwenye suala zima la sekta wezeshi na masuala ya nishati namna ambavyo imejipanga, uwezeshaji, uzalishaji wa umeme na kadhalika. Ninaamini Mpango huu utatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni namna watakavyoendelea kuwajibishana katika kusimamia Mipango hii, namna ambavyo imejipangia Serikali hatua kwa hatua, uwasilishaji wa taarifa za Mawaziri miezi kadhaa, taasisi nyingine na Tume yenyewe ya Mipango, itakayoenda kusimamia ni kiasi gani mipango hii inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Kitila Mkumbo, tutaendelea kuunga mkono na tutaendela kushauri na kuisaidia Serikali na kuona namna gani Mpango huu wa Miaka Mitano tunaouanza safari, unatekelezeka kwa ufanisi na dalili tumeziona kwa sababu kazi imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)