Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze maelezo yangu kwa kuhitimisha kwa shukrani. Kwanza nakushukuru sana wewe pamoja na wasaidizi wako, kwa jinsi ambavyo mmendesha mjadala huu kwa umahiri na umakini wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa Mbunge wa Dar es Salaam tunajivunia kuwa na wewe, Spika wetu mwema, rahimu sana, mtu very simple, but not simplicity. Ukimkuta Kariakoo kule anakuwa kama Mbunge wa Ilala tu. Tunakushukuru sana Spika, lakini mimi nikiwa natoka Singida pia najisikia nimewekwa katikati ya ulinzi wa hali ya juu. Nikiwa Dar es Salaam, ninaye Spika, nikienda Singida ninaye Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, narudia kuishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa uchambuzi wao makini sana, na jinsi walivyoibua maeneo mapya katika mapendekezo yao. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati mnaoongozwa na Mheshimiwa Mashimba Ndaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango. Hakuna shaka kwamba siku hizi tano, Bunge lako hili limethibitisha kwamba humu ndani unao Wabunge mahiri kwa kuzingatia michango yao. Ilikuwa ni michango ambayo ni very high quality, to say the list, nashukuru zaidi kwamba ni rahisi sana kuorodhesha makosa, lakini ni ngumu sana kupendekeza majawabu juu ya changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mmekuwa tofauti katika michango yenu, hamkuishia tu kulalamika, mmeonesha changamoto, lakini mmeonesha majawabu ya changamoto ambazo mmezitoa. Kwa hiyo, tunawashukuru sana na tumeona kabisa kupitia mjadala huu ni wazi kwamba vipaumbele ambavyo mmeviibua ndivyo vipaumbele ambavyo vipo ndani ya Mipango na tunashukuru kwamba Mipango ambayo tumeileta hapa imeakisi matakwa ya wananchi kwa jinsi michango yenu ilivyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake sekta ambazo zinazalisha fedha, watu wote hapa wamezungumzia umuhimu wa kuwafanya Watanzania wapate fedha, na tumeeleza sekta nyingi, lakini nifanye summary kidogo. Tunazo sekta tatu tu kimsingi ambazo hapa nchini kwetu na duniani kote zinaweza kuzalisha fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna shaka sekta ya kwanza ni sekta ya kilimo. Kitu kipya ni kwamba, Mpango unazungumzia kilimo cha biashara, na tumefanya vile kwa sababu tatizo ambalo tumekuwanalo la msingi limekuwa ni kuwa na kilimo cha kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tutoke hapo twende kwenye kilimo, tupate chakula, kwa maana ya kuhudumia tumbo, lakini tupate fedha kwa maana ya kuwa na fedha mfukoni. Kwa hiyo, kilimo cha tumbo na kilimo cha mfuko ili watu wetu wapate fedha kutoka kwenye kilimo, hicho ndicho kitu kikubwa sana ambacho Mpango umeeleza hapa na ninyi mmesema aina mbalimbali ya mazao na kadhalika na kadhalika. Kwa hiyo, ni eneo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya pili, ni suala zima la ufundi. Teknolojia na uzalishaji viwandani. Kwa hiyo, huku ndiko ambako tunamaliza rasilimali kutoka kwenye kilimo, zinaingia kule, zinafanyiwa Agri processing, zinabadilisha kilimo mazao yale kuwa bidhaa, unaongeza thamani, unaweza ukaiuza. Tunazo rasilimali mbalimbali hapa za kupeleka wenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni eneo kubwa, hapa pia ndiyo tunaongelea habari za ile inaitwa knowledge-based industries kama vile IT na kadhalika, ubunifu wote unaingia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni huduma (service). Hili ni eneo ambalo linabeba watu wengi sana. Tunazungumzia hoteli, usafiri, kwa hiyo, ukiona bodaboda, mabasi yote, hiyo ni sekta ya huduma. Music ambao sisi tumebarikiwa kuwa na muziki sana hapa Tanzania; muziki ni sekta ya huduma, na ni sekta muhimu ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za kitaalamu kama afya, elimu, zote hizo utalii. Huduma za dini, tunapowaona Wachungaji, Hashehe, na wenyewe wanachangia, ni huduma katika sekta ya uchumi. Uuzaji wa bidhaa, TEHAMA zote hizo ni huduma. Kwa hivyo, sekta zote hizi tunazizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichopo katika modernization ni kwamba, uchumi unavyokua watu wanaanza ku-move kutoka kwenye kilimo kwenda kwenye viwanda kwenda kwenye huduma, ndivyo ilivyo trend duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatarajia hapa kwetu, na kwa kweli, takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kwamba idadi ya Watanzania ambao wanategemea kilimo kwa sasa imepungua kutoka 65% mwaka 2021, mwaka 2024 inaonesha kwamba ni 54% na tunatarajia katika kile kipindi cha utekelezaji wa ilani itashuka, itafika 50%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo haimaanishi kwamba uzalishaji utashuka, uzalishaji utaongezeka, isipokuwa watu wengi zaidi unapokuza viwanda, unapokuza sekta ya huduma, wanazidi kumezwa kule, na GEN-Z tulionao ni watu ambao wanapenda zaidi kwenda kwenye huduma na kwenda kwenye viwanda. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tumeliweka hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati ambayo tunayo ni kwamba siyo kila nchi duniani zina maeneo hayo matatu. Zipo nchi ambazo zina huduma pekee. Ukienda Japan, kwa mfano huzungumzii kilimo kwa sababu hawana eneo la kulima. Sisi ni miongoni mwa nchi tatu ambazo maeneo yote matatu tunayo. Tunaweza kulima, tunaweza kufanya viwanda na tunayo sekta ya huduma. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tunalo na ni advantage na mipango imejaribu kuainisha ni namna gani hayo mambo matatu yanazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi lazima tu-balance uzalishaji na ulaji, mambo yote mawili haya; uchumi lazima uzalishe, na pia uchumi lazima watu wale. Sasa ndiyo umuhimu wa kukuza middle class. Ndiyo maana kwenye mpango, tunazungumzia kukuza middle class. Hakuna sababu ya kujenga hoteli kama hamna walaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuona middle class inakua kwa kiasi gani, zungukia kwenye migahawa. Watu wamejaa. Ukikuta watu wawili, mmoja ujue hapo ni changamoto. Kituo kimojawapo angalia, je, kwenu hapo, katika nchi yenu, kuna MacDonald? Kuna KFC? Kama hizo hazijaja, maana yake bado middle class ipo chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, moja ya eneo tuliloweka mkazo mkubwa ni kukuza middle class, lengo ikiwa ni kukuza pia uchumi wa ulaji kwa maana ya consumption. Kwa sababu, uzalishe na walaji uwe nao, kwa kuwa soko la kwanza ni soko la wananchi wako mwenyewe. Kwa hiyo, ni eneo ambalo tumeliwekea mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu ufafanuzi wa maeneo kama mawili, matatu, ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza hapa. Kwanza ni umuhimu wa sekta ya kilimo, hili hakuna shaka. Niseme kwamba pamoja na changamoto ambazo wameziainisha, tusisahau katika utekelezaji wa mpango wa miaka mitano huu, tumepiga hatua kubwa sana hususan tangu mwaka 2021, Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia aliweka mkazo na kipaumbele kikubwa sana kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuangalia takwimu zifuatazo; kwa mfano, bajeti ya Wizara ya Kilimo peke yake, imeongezeka wa 324% kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi trilioni 1.25, imepanda mara 324. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia angalia upandaji wa mbegu bora, Waheshimiwa wamezungumzia mbegu bora hapa, tulikuwa na tani 50,000. Sasa tunazungumzia tani karibia 80,000 hatujafikia lengo, lakini hatua kubwa imepigwa, matumizi ya mbolea yameongezeka tani 363,000 mpaka tani 850,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la umwagiliaji wetu wengi wamezungumzia hapa. Kwa muda mrefu tulikuwa na lengo la kufikisha hekta milioni moja ya umwagilliaji, ndiyo lilikuwa lengo kwenye Mpango wa Maendeleo uliopita. Kwa miaka yote ilibaki kwenye hekta 410,000, lakini ninavyozungumza leo tumeshafikisha hekta 983,466.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado safari ni ndefu, lakini msisahau pia tumepiga safari kubwa sana ukilinganisha na ambapo tumetoka. Lengo ambalo tumejiwekea kwenye Mpango uliopo ni kufikisha hekta milioni tano ifikapo mwaka 2030/2031. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, ajenda ya kilimo ni ajenda ya kudumu kwa CCM na ni kipaumbele mama kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ukitaka kuthibitisha hilo, tazama amewateua makada bora kabisa. Waliokabidhiwa sekta ya kilimo ni waliokuwa Makatibu Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo, kakabidhiwa Ndugu yetu Mheshimiwa Daniel Chongolo, moja ya Makatibu Wakuu bora wa CCM. Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amekabidhiwa Ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ambaye ni moja wa Makatibu Wakuu bora wa CCM. Hii siyo bahati mbaya, ni kuonesha kwamba Rais ameweka mkazo na kipaumbele kikubwa sana katika sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili, Waheshimiwa Wabunge, wameeleza haja ya kutunga sheria ya ugatuaji. Tuseme ni kweli, kwa muda mrefu tangu 1998 ugatuaji umeendeshwa na tamko la kisera la ugatuzi la mwaka 1998. Serikali imeshaamua pamoja na mafanikio yaliyopatikana, tunaenda kutunga, kuandaa Sera ya Taifa ya Ugatuaji. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI analifanyia kazi hili, na baada ya hapo, tutakuja na Sheria ya Ugatuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana tuzingatie kwamba, Mpango Elekezi na Mpango wa Miaka Mitano umeainisha hatua za kuimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sana, lazima tukubali kifikra, kimatendo, kimwenendo na kisheria kusogeza madaraka na mamlaka na fedha kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitawezekana kuleta maendeleo katika nchi hii kutokea Dodoma. Maendeleo lazima yatokee kwenye Local Government kwa sababu ndiko kuliko na wananchi. Haiwekezekani tulivyoweka kwenye Mpango tunatarajia ifike mahali Bunge lako hili lisijadili habari ya kujenga vituo vya mabasi, Bunge hili lisijadili habari ya kujenga madarasa, Bunge hili lisijadili habari ya matundu ya vyoo, mambo haya yafanyike kwenye Local Government. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tujadili namna ya kwenda space kule. Kwa hiyo, ili tufanye hayo, lazima tuimarishe Local Government. Tusipoimarisha, tutakuwa tunajadili kero hapa. Kuna tofauti ya kujadili kero na maendeleo. Kero zishughulikiwe kwenye Local Government na Bunge lijadili mambo ya msingi ya maendeleo. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo lazima tulizingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni mchango wa sekta binafsi. Tunaungana, ile tumeweka 70 na 30 imefanyiwa utafiti mkubwa. Hata sasa, tunapimaje mchango wa sekta binafsi? Tunaangalia ile Wazungu wanaita Gross Fixed Capital Formation unavyounda ile mitaji hata sasa, kwa miaka mitano 2020 - 2024 utaona kwamba jumla tuliweza ku-raise capital ya shilingi trilioni 344.2, sekta binafsi shilingi trilioni 241 na sekta ya umma shilingi trilioni 103. Kwa hiyo, tayari shilingi trilioni 201, hiyo ni 70% ya all the capital formation in the country. Kwa hiyo, tayari sekta binafsi inachangia katika mitaji yote ya uwekezaji nchini 70% na sekta ya umma only 30%. Kwa hiyo, tayari hiyo ambayo tumeweka inaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la kutunga sheria na taasisi ya ufuatiliaji na tathmini. Sheria ambayo mmeitunga hapa ya Tume ya Taifa ya Mipango Sura ya 127, moja ya jukumu lake ambalo imepewa ni kubwa, ni suala la M&E. Suala hapa ni utekelezaji. Taasisi ndiyo hiyo imekabidhiwa jukumu, Mwenyekiti wake ni Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu, tusimamie utekelezaji na Wizara za kisekta kazi yake kubwa itakuwa ni sera, usimamizi na vilevile M&E. Mambo mengi yafanywe katika shughuli za chini, na miradi siku ambayo wameizungumzia hapa nimemsikia Mheshimiwa Ado, hili suala la LNG, suala la Liganga Mchuchuma, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya takribani zaidi ya miaka 20, hii miradi amesha-unlock.
Mheshimiwa Mwenyekiti, LNG nimeeleza hapa, tupo hatua za mwisho, Liganga, Mchuchuma imeshalipwa fidia, GNT wanamalizia majadiliano, miradi hii inaenda kuanza. Ameshaanza kuikamilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kwamba Mipango ambayo tumewasilisha hapa ambayo ni nyenzo za utekelezaji wa dira, Mipango hii imeandaliwa na Watanzania, wataalam wetu wa ndani ndiyo wameandaa. Hata hivyo, ili kuhakikisha kwamba nyaraka hizi zinakidhi viwango vya Kimataifa, zimefanyiwa mapitio na taasisi za tafiti za ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, tulifanya utafiti, lakini walipoandaa tulifanya pia external review kukaribisha taasisi za Kimataifa wakazipitia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie jambo moja, taasisi moja ya Uingereza ilipokuja hapa tulikaa nao, waliposoma Mpango wetu na dira yetu, wakasema: “Uchumi wenu umekuwa ukikua vizuri miaka yote 20. Hata mkibaki hivi hivi mlivyo, mkafanya mambo kama mnavyofanya bila kubadilisha chochote, uchumi wenu utaongezeka mara mbili na nusu mpaka mara tano.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mkibaki hivi hivi ifikapo mwaka 2050 uchumi wenu unakaribia kwenda Dola za Kimarekani bilioni 500. Wakatuambia, “kama mkibadilisha mwenendo, mkafanya mambo isivyo kawaida, badala ya kutembea, mkaanza kukimbia, what they called business unusual mnaweza uchumi wenu ukakua ukaenda zaidi ya shilingi trilioni moja ifikikapo mwaka 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi walipokutana na wenyewe wakawa na maoni hayo hayo. Kwa hiyo, tulipompelekea Rais mapendekezo, tulipeleka scenario zote hizi. Tulipomweleza Rais, kwa ujasiri mkubwa, aliamua, akachagua, na kuelekeza kwamba tuende na business unusual, kwenda kwenye shilingi trilioni moja, lakini it is only possible if we begin doing things, business unusual. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uniruhusu nieleze hapa kwa mujibu wa Mpango ambao tumeuwasilisha, mambo kumi ambayo lazima tuyafanye ili ku-attain business unusual. Jambo la kwanza, ni lazima tubadilishe mtazamo kuhusu kazi ya dola kutoka kuwa mdhibiti kwenda kuwa mwezeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu kabisa, na kwa kweli tunatafakari mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, wamependekeza kwamba tuwe na regulatory authority moja, tuvunje zote zilizopo, tuwe na moja ili kuondoa kero. Hili ni pendekezo kubwa, tumelichukua, na Serikali italitafakari tuone namna ya kulitekeleza. Hoja ya msingi hapa ni kwamba, ni lazima Serikali ipunguze udhibiti iende kwenye uwezeshaji. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, muda wako umeisha naomba umalizie.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuanza kupimana kwa kuzingatia matokeo na viashiria vinavyopimika badala ya kupimana kwa kuangalia shughuli ambazo mtu amezifanya. Hapa tunapimana sana kwa shughuli. Mtu yupo busy anafanya shughuli nyingi kwa matokeo yapi? Kwa hiyo, Mpango unaeleza twende kwenye results-based performance. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kukubali kuchagua sekta chache ambazo ni engine ya ukuaji wa uchumi na kuzipa nguvu isiyo ya kawaida. Hapa Waheshimiwa Wabunge, turejee mchango makini sana wa Mheshimiwa Prof. Sospeter Mwijarabu Muhongo, wale wanaodharau elimu wasikilize mchango wa Mheshimiwa Prof. Muhongo kama ni wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumechagua sekta chache tisa za kimageuzi, na tumechagua vichocheo vitano ambavyo vitapewa msukumo usio wa kawaida ili uchumi wetu uweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa ninamalizia. Jambo la nne ni kuifanya sekta binafsi kuwa sehemu muhimu kama nilivyosema awali. Hapa tukizungumzia sekta binafsi, hatuzungumzii malaika hapa. Sekta binafsi kama ilivyo sisi, watafanya makosa, lakini tuzingatie utawala wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la sekta binafsi, mtu mmoja anafanya makosa, anazomewa nchi nzima, haiwezi kutusaidia. Sekta binafsi moja ikifanya makosa, achukuliwe hatua za kisheria, kuliko kana kwamba sekta binafsi yote ni mbovu, hapana. Hii haiwezi kuwa sawa. Watakuwa na makosa, lakini tuzingatie utawala wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeainisha mambo mengine, lakini la mwisho niliseme, kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria. Hili ni muhimu kabisa, hatuwezi kufanya mipango hii bila kuzingatia utawala wa sheria. Haya ni mambo ambayo lazima tukubali, lakini kujenga utamaduni wa kukumbatia weledi, utaalam na wenye weledi na wataalam, uadilifu na waadilifu, uwajibikaji na wawajibikaji, na mwisho kuchapa kazi na wachapakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu tuna utamaduni kidogo. Mtu akichapa kazi sana, wakati mwingine wanasema huyu naye anajipendekeza, anataka uteuzi, ahaa, tuache hizo. Watu wanaochapa kazi, wenye weledi, wenye uadilifu, tuwaheshimu, tuwakumbatie, ni jambo la msingi sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nihitimishe kwa kusema tu, hapa duniani tunayo mambo mengi ya kushukuru ambayo tumebarikiwa nayo, na wakati mwingine hatuwezi kuyamaliza yote kuyasema, lakini mambo matatu hatuwezi kuacha kuyashukuru. Kwanza, tunapaswa kushukuru kwa anayetupa uhai, neema, rehema na baraka. Huyu ni Mungu na Mungu pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunapaswa kumshukuru mtu anayetupa hifadhi na kututunza, hapa ni familia. Tatu, tunapswa kumshukuru mtu anayetupa fursa ya kutumikia umma kwa kuwa siYo kila mtu ana fursa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii adimu na adhimu kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fursa aliyonipa ya kutumikia katika Serikali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, kwa fursa aliyonipa ya kuongoza mchakato wa kuandika nyaraka ambazo zitaongoza mustakabali wa nchi yetu kwa miaka 25 ijayo, hili kwangu ni jambo kubwa, ni upendeleo wa kipekee na sitausahau katika maisha yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba wengi hapa wamenipongeza, lakini wasisahau, wamenipongeza, wameuona uwezo wangu kwa sababu nimepewa fursa. Kama nisingepewa fursa, wasingefahamu uwezo wangu. Ninamheshimu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu amenipa fursa hii, nao wakaniona. Ninamshukuru Mheshimiwa Samia, na Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mdogo wangu, Baba Levo amesema pale, ametoa historia yetu kidogo. Ni kweli, hapa duniani ipo hadithi moja. Alikuwa anakimbia ndege maarufu angani, ikatokea baridi na theluji, akazidiwa, akaanguka anasubiri kufa. Kwa bahati nzuri, akawa anapita pundamilia, akamnyea. Kile kinyesi kwa sababu kilikuwa ni cha moto, kinyesi kikawa pona yake, akapata joto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, duniani hapa siyo kila kinyesi ni kibaya. Mdogo wangu Baba Levo, siyo kila teke ni baya. Kuna teke ukipigwa linakupeleka pazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie. Serikali imepokea maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na tutayazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)