Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufika asubuhi ya leo na kuweza kufikia majumuisho ya michango ya Waheshimiwa Wabunge katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Mwongozo wa Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa uongozi wenu katika mjadala wote huu tuliokuwa nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana ilikuwa tarehe 5 Februari, 2026. Miaka 49 iliyopita siku kama ya jana, katika Uwanja wa Amani Zanzibar vyama viwili vya ukombozi TANU na ASP viliunganishwa na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa kwa kuadhimisha miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi. Ni matumaini yangu kuwa chama hiki kitaendelea tena kuongoza katika miaka 49 ijayo na kitaendelea kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa Taifa hili, ikizingatia yale ambayo wananchi wanayahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Bajeti, na tulipokea maoni na michango kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, ambapo kimsingi mwongozo huo umepata maoni ya namna ya kuimarishwa kabla ya kuweza kutolewa kwenda kwa Maafisa Masuuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, waliendelea kutoa ushuhuda wa kazi kubwa ya maendeleo iliyofanywa nchini kote katika muda wa miaka minne iliyopita, ya kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika sehemu kubwa ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni maoni ambayo tumeyapokea kwa heshima kubwa. Ninaomba uniruhusu nitoe maelezo mafupi kwenye maoni, hasa kutokana na yale ambayo yametokana na Kamati yetu ya Bajeti, ambayo mimi ni Mjumbe, kupitia uongozi wa Mwenyekiti mahiri Mheshimiwa Mashimba Ndaki Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maoni ya Kamati moja ya hoja ambayo ilitolewa ilikuwa ni kuitaka Serikali kuangalia upya suala la kutenga asilimia tano ya mapato ya mifuko kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za kuendeleza miundombinu kwenye maeneo maalum ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipendekeza kama Serikali kwamba katika mifuko mbalimbali asilimia tano itengwe kwa madhumuni haya, lakini maoni ya Kamati ikawa kwamba tuliangalie hili na ikiwezekana kuliacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunadhani kwamba, tutoe maelezo ya ziada kwamba maelezo yetu yanaambatana na yanaendana na maoni ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge ya haja ya kufungua fursa zilizoko katika mikoa na maeneo ya kijiografia mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia mikoa ya Mara, Mbeya, Kigoma na kwingineko kwamba kuna fursa kubwa za kiuchumi zinahitaji kuendelezwa na zinahitaji kufunguliwa. Sasa katika hili pendekezo letu lilikuwa siyo kubadili mfumo uliopo wa matumizi ya fedha za mifuko isipokuwa ni kuendana na uamuzi wa Serikali wa kuweka maeneo maalum ya kiuchumi katika kila mkoa. Kwa hiyo, pendekezo ilikuwa ni kwamba pale ambapo Mfuko wa TARURA au TANROADS utapeleka barabara katika mkoa, sehemu ya barabara ziwe zinapelekwa katika maeneo haya maeneo huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, mifuko ya maji, UCSAF, na mifuko mingine yote nayo ielekeze sehemu ndogo ya asilimia tano tu ielekezwe katika miundombinu katika maeneo ya kiuchumi ili tuweze kuyafungua haya maeneo na tuweze kutumia vizuri fursa ambazo zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili lilikuwa ni marekebisho, ambapo Kamati ya Bajeti ilipendekeza katika ile 10% ya awali kwa ajili ya makundi maalum, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, tulipendekeza kuongeza asilimia nyingine tano ambayo nayo ikaonekana kwamba kuna tofauti ya uwezo wa halmashauri zetu, na kwamba pendekezo hili lilenge kwenye halmashauri ambazo zina uwezo pekee na zile nyingine zisubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pendekezo la Kamati lilikuwa ni kwamba, kwenye mwongozo tufanye marekebisho ili tuweze kuchukua haya maoni ambayo yamejitokeza na mwongozo elekezi iwe halmashauri zenye uwezo peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri huu na tumekubaliana nao. Isipokuwa niongeze tu kwamba, tunapokwenda katika mwaka unaofuata wa fedha tumekubaliana na wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kwamba tutafanya study maalum kuangalia uwezo wa halmashauri zote na kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwenye kupunguza tofauti ya uwezo wa kimapato baina ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatazama horizontal physical imbalance ambayo tunajaribu kui-address kwa utaratibu maalum. Kwa hiyo, hili tutalifanyia utafiti wa ziada na tutalitolea mwongozo baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu lilikuwa ni kuisaidia sana Mamlaka ya Mapato (TRA) kuweza kuimarika na kukusanya mapato yetu zaidi, hasa katika upande wa mifumo ya TEHAMA. Katika hili niseme kwamba, Serikali imekuwa ikichukua jitihada kubwa sana za kuimarisha TRA. Mwaka huu tukijaliwa TRA itatimiza miaka 30 tangu kuanza kwake rasmi shughuli zake. Ilianza mwaka 1996 na mwaka huu itakuwa imetimiza miaka 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi katika miaka 30 hiyo takribani yote nimekuwa mdau wa TRA. Ninaijua TRA ilipotoka, nilikuwa mfanyakazi kwa miaka 12, nilikuwa katika senior managers wa TRA kwa miaka tano na nusu, na nimehudumu katika bodi yao kwa takribani miaka 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaifahamu TRA tulioanza nayo, haikuwa na mfumo wowote wa mapato. Leo hii TRA ina mifumo takribani 21 ya TEHAMA. Upande wa Customs wana mfumo mkuu mmoja unaitwa Tancis ambao unaungana na mifumo miwili mingine ya taasisi tofauti wa Electronic Single Window System na TANOGA ambao unaungana na mamlaka zote za udhibiti kwenye utoaji wa mizigo bandarini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mapato ya ndani kuna mifumo tisa, halafu kuna mifumo mingine miwili kwa upande wa malipo, na kwa upande wa utawala kuna mifumo tisa. Kwa hiyo, kwa ujumla TRA ina mifumo 21. Tumelichukua pendekezo la kuimarisha zaidi mifumo ya TEHAMA, lakini hili nilitaka tuliseme na tuliwekee maelezo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusu kutumia kifungu cha 13 (a) cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ili kuzisaidia benki za uwekezaji kupata mikopo kutoka nje ya nchi. Kwenye hili niseme, tumelipokea vilevile, lakini tunaupokea ushauri huu wa Kamati kwa tahadhari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hivi Tanzania ina benki 42 ambazo zimeshapewa leseni na Benki Kuu, ikiwemo benki moja ya maendeleo TADB, benki moja ya uwekezaji TIB, benki 35 za biashara, benki mbili za jamii, na benki tatu za sekta ndogo ya fedha (microfinance banks).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushauri wa kwamba tuziruhusu benki kwenda kukopa nje, niseme kwamba kwa upande wa TADB tayari sheria ilishafanyiwa marekebisho na inaruhusu hili, lakini inategemea na uwezo wa benki yenyewe kwa kutizama mizania ya benki. Kwa hiyo, kwa upande wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB, hii imeshasaidiwa na imeweza kufanikisha mkopo kutoka nje wa shilingi bilioni 562 ambao umetokana na Benki ya Maendeleo ya Afrika na Shirika la Maendeleo la Japan (JAICA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazungumzo yanaendelea kwenye upande wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na tunatarajia nako itafanikiwa. Benki ya TIB inahitaji kwanza kuimarisha mizania yake ili tuje kuepuka hili jukumu la mkopo kuja kuhamia upande wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabumbe pamoja na Kamati lilikuwa ni upande wa deni la Serikali na haja ya kuendelea kulidhibiti na kutumia vigezo vingine. Tumepokea ushauri, lakini niseme, kama ambavyo tumezungumza kwenye upande wa kuimarisha mapato na deni la Serikali, tumeendelea kuliangalia kwa ukaribu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifanya uchambuzi wa kuangalia uhimilivu wa deni lenyewe, na kwa bahati takribani miaka yote kila tunapofanya uchambuzi imebadilika kwamba ni deni himilivu. Hata hivyo, nilitaka niseme, wakati tunaangalia deni letu, ni muhimu sana kuliunganisha na uwekezaji mkubwa, hasa kwenye maeneo ya miundombinu ambao unaendelea nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetumia wapi deni letu katika miaka iliyopita? Tukikamilisha ujenzi wa kipande cha kwanza mpaka cha sita (lot 1 to 6) za SGR itakuwa tumejenga kilomita 2,102 za reli ya kisasa ya SGR hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya ujenzi wa SGR reli iliyokuwa inaongoza ilikuwa ni TAZARA ambayo urefu wake ni kilomita 1,860. Kwa hiyo, SGR ambayo inaunganisha kutoka Mashariki kwenda Magharibi itakuwa ni ndefu zaidi kuliko reli ya muda mrefu tuliyokuwa tunajivunia ya TAZARA. Jumla ya dola bilioni 10 zitahitajika. Hadi sasa hivi bilioni nane zimeshatumika kwa madhumuni hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo limeongeza uwezo wetu wa nishati mpaka kufika Gigawati nne na limegharimu takribani shilingi trilioni 7.542.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa miradi iliyopo ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato hapa Dodoma ambao utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka, na ambao utaweza kuhimili ndege za aina hii zikiwemo ndege za aina ya Boeing 737 na 767 Dreamliner kwa mara ya kwanza zitaweza kutua Dodoma. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tunahitaji kuendelea kuangalia deni letu, lakini tuangalie deni lenyewe linatumika kwa ufanisi kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka nilitolee ufafanuzi, ni suala la misamaha ya kodi, ambalo Waheshimiwa Wabunge nalo wamelizungumza sana; na Kamati ilipendekeza tufanye tathmini ya misamaha yote ya kodi na kuiondoa ile ambayo haina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini zimeendelea kufanyika na tathmini ya mwisho ambayo ilifanyika mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025 ilitoa matokeo mazuri. Kwa upande wa uwekezaji wa kawaida, ilionesha kwamba, katika kipindi hicho jumla ya miradi 2,293 iliwekezwa nchini, iliidhinishwa nchini, ambapo misamaha ambayo ilitolewa ilikuwa ni shilingi trilioni 1.35. Miradi hii ilipelekea kupatikana kwa ajira 666,940.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa upande wa miradi ya uwekezaji ya kimkakati, jumla ya miradi 36 iliwekezwa nchini katika kipindi hicho, ambapo misamaha ya kodi iliyotolewa ilikuwa ni shilingi milioni 144,806.78; lakini kodi ambazo zililipwa kutokana na miradi hiyo ilikuwa ni shilingi milioni 931,953.81.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miradi mingine, picha ambayo ilijitokeza ni hii hii, ambapo miradi hii ilichangia ajira 27,820. Kwenye upande wa misamaha ya kodi, kama nilivyosema, tumepokea ushauri mzuri na tutaendelea kuifanyia kazi yale yasiyo na tija ili misamaha isiyo na tija tuiondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Mipango amezungumza, nchi yetu iko katika hatua ya uwekezaji na tunakoendelea tunaamini kwamba sekta itaendelea kuhitajika na tutahitaji uwekezaji mkubwa. Kwa hiyo, hapa tutahitaji kuleta uwiano mzuri baina ya uwekezaji pamoja na vivutio ambavyo tunavitumia kwenye uvutiaji wa misamaha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kulikuwa na swali moja ambalo lilijitokeza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge liliulizwa kwamba, ni kwa nini upande wa Zanzibar haikujitokeza kabisa katika Mwongozo wala katika Mpango wa Maendeleo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme tu, kwa mujibu wa utaratibu kwa mujibu wa Katiba na Muungano wetu, masuala yote yasiyo ya Muungano yanayohusu upande wa Zanzibar haya yako moja kwa moja chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia mamlaka ya kutunga sheria ambayo inasimamia na kupitisha bajeti zake ni Baraza za Wawakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunathamini kazi kubwa ambayo imefanyika katika miaka yote, lakini hasa katika kipindi hiki. Kwa upande Zanzibar, miradi ya kimkakati ambayo ilitakiwa ionekane humu, haiwezi kuonekana kwa sababu ya kikatiba na itaonekana katika mapendekezo ambayo yataanzishwa na SMZ kwa upande wa Baraza la Wawakilishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme kwamba Serikali imepokea maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na tutayazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)