Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. ABDALLAH S. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyopo Mezani. Kipekee nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kuzifanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninachukua nafasi hii kuwapongeza watoa hoja: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na msaidizi wake Mheshimiwa DKt. Chaya kwa wasilisho zuri. Pili, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Balozi Khamis Omar pamoja na Manaibu wake, Mheshimiwa Eng. Mshamu Munde na Mheshimiwa Luswetula. Ninawapongeza kwa kazi nzuri, wameanza kazi zao vizuri. Ni Mawaziri ambao wanafikika, wanasikiliza, na wanashaurika. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasilishiwa hapa nyenzo tatu na Waziri wa Mipango kwa ajili ya utekelezaji wa Dira 2020 – 2050. Ninanukuu maneno yake katika wasilisho lake amesema: “Kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira 2020 – 2050, nyenzo tatu zimeandaliwa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Ukiangalia wasilisho la Mheshimiwa Waziri na ukurasa wa 86 wa huu mpango wa nne unaelezea kinagaubaga kwamba, ili kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio wa mpango wetu, imebainika mambo manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita katika jambo moja tu la msingi. Utawala bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, na zimeainishwa changamoto hapa, kwamba Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, asilimia 85 ya bajeti yake inategemea Serikali Kuu. Changamoto ya pili ni kwamba, kuna mwingiliano wa majukumu kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile imeelezewa vizuri kwamba, kuna upungufu mkubwa wa watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na ikaja na suluhisho kusema, “hapa ili tuziwezeshe Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa lazima tuzingatie ugatuaji, D by D (Decentralization by Devolution).” Mimi nitajikita hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu hakiwezi kutekelezeka kama hakutakuwa na Sheria ya Ugatuaji. Ugatuaji Tanzania bado tunatekeleza kwa tamko la kisera tu, hata sera bado haipo. Maelezo ya Wizara kwamba sasa hivi wamekamilisha sera, basi sheria ya ugatuaji ije ili yawekwe wazi majukumu ya Serikali Kuu na majukumu ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. La sivyo, tutakuwa tunachanganyana kila siku na kutakuwa na mabadiliko kila siku. Akija huyu, anasema watumishi wa kilimo wahamie Serikali Kuu, mwingine anasema watumishi wa kilimo wabaki Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, ni lazima ije sheria ya ugatuaji ambayo itaelezea vizuri majukumu ya Serikali Kuu na majukumu ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, itaainisha vyanzo vya fedha kwa Serikali Kuu na vyanzo vya fedha kwa Serikali za Mitaa. Sasa hivi kuna kuchanganyana. Vyanzo vyote vya fedha vya kuaminika vipo Serikali Kuu. Vyanzo vya fedha vya Serikali za Mitaa siyo vya kuaminika, havitabiriki, na siyo vya kuleta mapato kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, huu mpango unaelezea vizuri kwamba lazima kuwe na maboresho katika uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, na kukawa na wazo kwamba hata Wakurugenzi sasa wapatikane kwa njia ya uwazi, wasailiwe na nafasi ziwe za ushindani. Mimi ninashauri tusiishie tu kwa Wakurugenzi, twende mpaka kwa Wakuu wa Idara, nao wapatikane kwa ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapofanya hayo tusiangalie upande mmoja wa management, tuangalie na hadhi ya Madiwani katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kama Diwani tunampa kutunza shilingi bilioni 100 kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, inakuwaje Diwani yule anakwenda kule kwa posho ya shilingi 300,000/=? Kwa hiyo, ni muda muafaka sasa hivi tuangalie hata hadhi ya Diwani, tuangalie sifa ya Diwani, tuangalie majukumu ya Diwani ili waweze kuzisimamia vizuri Serikali zetu za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, ili kweli tuboreshe utawala kwenye ngazi ya chini, twende mpaka kwa wenyeviti wa Serikali za Vijiji, mpaka na Wenyeviti wa Mitaa. Majukumu yao sasa yameongezeka. Majukumu ya Mwenyekiti wa Mtaa leo siyo yale ya mwaka 1971. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie zile hadhi zao, tupandishe hadhi zao, na tuhakikishe kwamba tunawatengenezea mazingira wezeshi ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa halmashauri una changamoto. Sisi wakati wa bajeti hapa tunakaa miezi mitatu kujadili bajeti. Hivi inawezekanaje Madiwani wanakwenda halmashauri kwa masaa matatu wanapitisha bajeti ya mwaka mzima, tena kwa idara zote nne kwa masaa tu? Hicho kitu hakiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanakwenda pale wanaweka makabrasha yao, na ukikuta Mkurugenzi ambaye yuko smart, anamwambia karani wagawie posho sasa hivi. Akianza kuzungusha karatasi ya posho tu basi, wote wanaangalia saa, wanaangalia wakapande magari, wanatawanyika. Hatuwezi kuendesha hivyo Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Lazima tuwape siku za ku-debate hiyo halmashauri yao. Tuwape siku tatu siku nne wajadili bajeti ya halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tuangalie hata uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Je, kwa muda tulionao huu, hivi bado kweli Baraza la Madiwani liendelee kuwa Mamlaka ya Nidhamu kwa watumishi wa halmashauri? Mamlaka ya Nidhamu ambayo Mkuu wa Idara anaweza akasema Kamati ile ya Fedha ina Madiwani wakorofi watatu. Kesho akaenda kuwarubuni, amefanya ubadhirifu inaonekana kwamba tumwachie tu tumsamehe. Kwa hiyo, vitu kama hivi inabidi vibadilishwe katika Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengi ya kuelezea kwenye Serikali za Mitaa, lakini ninaomba niishie hapo. Lazima tufanye mabadiliko ya kweli ili kweli tupeleke nguvu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Kamati ya Bajeti, kwanza niwapongeze sana, wamefanya uchambuzi mkubwa sana. Wao vilevile wanampongeza Rais kwa kuongeza bajeti. Walipopitia pale Mwongozo wa Mpango wa Maandalizi ya Bajeti wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu. Nami pia ninaungana nao kwa sababu sasa hivi bajeti ijayo itatoka shilingi trilioni 7.3 kwenda shilingi trilioni 8.19, sawa na ongezeko la 10.4%. Hili ni ongezeko kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, hizi fedha ambazo zinaongezeka zisiende kwenye miundombinu tu, tumwangalie na mwalimu mwenyewe ambaye anafanya mabadiliko katika sekta ya elimu. Hakuna elimu pasipokuwa na mwalimu mahiri. Ni lazima tumwezeshe mwalimu kwa in-service training, tumwezeshe mwalimu kwa maslahi yake, walimu wapate stahili zao kwa wakati ili waweze kuchapa kazi vizuri. Tukiwawezesha walimu kama anavyowekeza Mheshimiwa Mama Samia, matokeo yanaonekana. Sasa hivi Division One zimejaa kwenye shule za kata na matokeo mmeyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti tukiendelea kumthamini mwalimu, tukiendelea kuwekeza kwa walimu, matunda yataonekana vizuri katika shule zetu za kata. Kwa hiyo, zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa motisha kwa walimu, zitolewe fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo kazini kwa walimu, na pia stahili zao zilipwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mtindo wa baada ya miaka minne inaundwa timu ya kushughulikia madeni ya walimu, hapana. Walimu walipwe kwa wakati. Hakuna sababu ya kuunda Tume ya Kushughulikia Madeni ya Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwenye Mapendekezo ya Mwongozo wa Utayarishaji wa Bajeti nichangie mambo mawili. Suala la kwanza ninashauri kwamba, kwenye mwongozo yatolewe maelekezo mahsusi kwa Maafisa Masuuli katika bajeti ijayo kwa mambo mawili. Jambo la kwanza ni kwamba wasianze miradi mipya, tukamilishe viporo vya zamani. Hakuna haja ya kuanza miradi mipya wakati tuna viporo hatujakamilisha. Pili, zitengwe fedha za kutosha kulipa madeni ya wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)