Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hii mipango ya muda wa kati, muda mfupi, na muda mrefu. Nami nianze kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa wasilisho zuri sana ambalo lina takwimu za kutosha. Vilevile ninampongeza Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa uwasilishaji mzuri sana wa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwa kuchangia sehemu ambayo Kamati ya Bajeti imependekeza kwamba Serikali ione uwezekano wa kuanzisha sera na sheria ya tathmini na ufuatiliaji (Monitoring and Evaluation). Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu ukiangalia fedha ambayo Serikali inaelekeza kwenye maendeleo ni fedha nyingi sana. Ni kiasi kikubwa cha fedha ambayo inatoka kwenye vyanzo mbalimbali, ambavyo vingine ni mikopo. Mikopo, mapato yanayotokana na kodi na vyanzo vingine mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana kukawa na sera ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kusimamia mambo ya tathmini na ufuatiliaji, kukatungwa na sheria, ikapitishwa na Bunge kwa ajili ya kuelekeza mambo mbalimbali. Hii ni muhimu sana kwa sababu fedha ambayo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunacho kitengo katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambacho kinafanya Monitoring and Evaluation. Vilevile kwenye Wizara ya Mipango na Uwekezaji nako ninaamini kuna kitengo ambacho kinafanya kazi hiyo. Hata hivyo, tungekwenda mbali zaidi. Hiyo ingejichukulia kama ni vitengo tu kwa ajili ya kuishauri Serikali upande wa ndani, lakini tukija na sera na sheria ikaundwa na taasisi maalumu ya kusimamia, kwa sababu hata kwenye maeneo ya ukaguzi kuna ukaguzi wa ndani, (internal auditors) na vilevile kuna external auditors.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile inasaidia sana mtu asiweze kujichunguza mwenyewe. Yaani Serikali hiyo hiyo inafanya miradi, lakini inajichunguza yenyewe. Kwa hiyo, ili tupate maoni yenye uhuru, ni vizuri tukawa na taasisi ambayo ni independent kabisa, ikiwezekana kama ilivyo taasisi ya CAG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine ukiangalia, unaona hadi wa Wizara kabisa ambayo inasimamia mambo ya tathmini na ufuatiliaji. Ikiwa taasisi, kwa kweli itakuwa na uhuru mkubwa zaidi na itaweza kutushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukua mikopo kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo. Unakuta mradi umechelewa kutekelezwa, lakini muda wa mkopo kuanza kulipwa tayari umeshafika. Kwa hiyo, tunampa kazi Waziri wa Fedha kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya kurejesha ule mkopo. Kumbe mradi ule ambao umechukua mkopo ungekuwa umesimamiwa vizuri, ungekamilika kwa wakati, ungelipa deni wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa, mambo haya ili tuweze kuyafanya vizuri, ninapendekeza kwamba hili suala ambalo Kamati ya Bunge ya Bajeti imeweza kushauri ya kutungwa kwa sera, sheria, na kanuni ikiwezekana kwa ajili ya tathmini na ufuatiliaji, vilevile twende mbali zaidi tuunde na taasisi ambayo itakuwa huru na ambayo haitaingiliwa na chombo chochote kama alivyokuwa CAG ili waweze kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia sana tunavyozungumzia hii Dira ya Maendeleo ya Taifa, na haya mageuzi ya kimifumo na kubadili mindset ambapo Mheshimiwa Waziri ameelezea kwenye ripoti yake tutaweza kwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imesisitiza, na siyo mara ya kwanza kuzungumzia umuhimu wa Serikali kutenga angalau asilimia moja ya pato la Taifa kwa ajili ajili ya tafiti. Tukitenga asilimia moja kwa ajili ya tafiti, tukavishirikisha vyuo vyetu vikuu, tuna Chuo Kikuu cha Sokoine, tuna Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine, Chuo Kikuu cha Dodoma, hizi fedha wakashirikishwa ili ziweze kuelekezwa katika tafiti, tafiti zitatusaida kuwa na sera ambazo zimefanyiwa tafiti nzuri, ambazo zitakuwa zinajibu changamoto halisi za kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana kwenye pato letu la Taifa Serikali ikafuata ushauri wa Bunge ambao unaielekeza kutenga asilimia moja kwa ajili ya kuelekeza kwenye tafiti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lina umuhimu mkubwa sana lakini vilevile hata kwenye upande wa hizi sera, sheria; tulikuwa na ile Tume ya Kurekebisha Sheria na yenyewe ikipewa fedha iweze kufanya tafiti kuona sheria ambazo zinaweza zikawa kikwazo katika kufikia malengo ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana, kwa sababu unaweza kukuta kuna gaps nyingi sana katika mipango yetu, katika sera zetu. Kwa hiyo, hao watafiti mbalimbali watatusaidia kuonesha maeneo yenye upungufu ili tuweze kuyafanyia marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Serikali ipokee ushauri wa Bunge, asilimia moja ya pato la Taifa liweze kutengwa kwa ajili ya tafiti. Tafiti hizi zifanywe na taasisi mbalimbali za Serikali. Kwenye kilimo kuna taasisi nyingi sana ambazo zinahusika na tafiti za mbegu; na tafiti za mambo ya uongezaji thamani wa mazao na vitu vingine. Kwa hiyo, ziweze kupewa fedha kwa ajili ya kufanya tafiti ili sera zetu na mipango yetu iweze kuwa na uhalisia isiwe na pungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwenye taarifa hizi kuna hoja ya ugharamiaji wa mpango. Serikali imetuletea taarifa kwamba mpango elekezi wa muda mrefu unagharimu Dola za Marekani bilioni 3,582 na katika hizo, 70% Serikali inatarajia kuzipata kwenye sekta binafsi wakati 30% zitagharamiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tukiangalia mazingira ya sekta binafsi hapa nchini katika eneo la ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, maeneo mengi ambayo ukuaji wake unaenda vizuri yametegemea zaidi uwekezaji ambao umefanywa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sekta binafsi bado zina changamoto nyingi. Kwa upande wa mikopo, sekta binafsi bado wana changamoto ya kupata mikopo ambayo ina riba nzuri, ambayo itapatikana kirahisi ili wakienda kuwekeza waweze kufanya biashara na Serikali iweze kupata kodi za kutosha na ukuaji wa uchumi uweze kwenda kwa kasi. Kwa hiyo, mazingira ya ufanyaji biashara bado ni changamoto. Pia hilo suala la mindset za watumishi bado ni changamoto kwenye baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikutana na mtu mmoja analalamika kwamba yeye ana biashara, ana TIN number, sasa kutokana na shughuli zake kuwa nyingi alikosa muda wa kwenda kufuatilia leseni ya biashara. Kwa hiyo, alimtuma mtu mwingine ili anavyopata ile leseni ya biashara maana yake analipa mapato Serikalini. Alipofika kule kwenye halmashauri (ninaomba niihifadhi) akaambiwa hii TIN haina majina yako. Kwa hiyo, uje na kiapo kutoka kwa mwanasheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa mindset kama hizi, kwa sababu mtu anakuletea fedha, unamwambia alete kiapo kutoka kwa mwanasheria kwa ajili ya kupeleka kwenda kufanya assessment ya kodi. Kwa hiyo, vitu kama hivi ninafikiri mindset za aina hii tuweze kuziepusha na urasimu ili tuweze kufikia malengo haya ya hii mipango ya maendeleo ni muhimu sana tukaangalia hili eneo la sekta binafsi tukapunguza urasimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tukahakikisha kwamba sekta binafsi zinapata mikopo ambayo ina riba nafuu, kwa sababu ukiangalia mikopo mingi ambayo wanachukua sekta binafsi, riba zake zinaanzia 15% mpaka 24%. Kwa hiyo, sasa hii ni riba kubwa sana na inaweza ikawa ni kikwazo kikubwa sana kwa sekta binafsi kuchangia kwenye utekelezaji wa hii mipango ya muda wa kati na muda mrefu ambayo tunaielezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anajibu swali la Mheshimiwa Sanga Nyakisa, ameeleza kwamba mambo ya mikopo yanategemea zaidi nguvu ya soko, lakini ninadhani kuna haja ya kuangalia vizuri hapa ili sekta binafsi iweze kupata mitaji ya kutosha kwenda kuwekeza na itakayosaidia kwenye utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kama ambavyo tumezungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia sekta binafsi zinakabiliwa na changamoto ya utitiri wa kodi. Kwa hiyo, tuangalie kodi zetu zile za Serikali Kuu na kodi zinazotozwa na halmashauri zetu, Serikali za Mitaa tuone zile kodi ambazo ni kikwazo katika maendeleo ya nchi yetu katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa ili tuweze kuziweka sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, eneo la mwisho ni eneo la miundombinu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)