Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, kwa mara yangu ya kwanza leo toka tuchaguliwe. Ninawashukuru wananchi wa jimbo langu kwa kuendelea kuniamini na mimi nitaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaomba nitoe mchango wangu kwa Mapendekezo ya Mpango tunaoujadili. Kwanza nina imani kubwa sana na Profesa kama msimamizi wa Mpango na Waziri. Tunamwelewa, lakini ninaoushauri ambao ninadhani ni vizuri nikatoa ushauri. Kwa muda mrefu nikiwa Bungeni, sisi Tanzania hatuna shida na mpango na mawazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo tunayo mengi sana, sana tu, mpaka na ziada na library tumeweka, tatizo ni utekelezaji wa Mpango wenyewe. Kila mwaka tunapanga vizuri, linapofika suala la utekelezaji tunatawanyika na mara nyingi Waziri wa Mpango anakuwa kivyake, Waziri wa Wizara nyingine hamzungumzi lugha moja kwenye kutekeleza huu Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka maandiko yanakuja yanasema tuwaimarishe wakandarasi wa ndani. Nyinyi wote humu ni mashahidi tunatoka kwenye jamii inayotuzunguka ya wakandarasi. Kama kuna watu wanaishi maisha ya vidonge vya presha kwenye mifuko ni wakandarasi. Tunazungumza tu kirahisi tuwaimarishe, lakini kazi zinapotoka wanapewa wageni na ukisoma mikataba ya wageni ina kikomo. Ukichelewesha kulipa, unapigwa penalty. Ukienda kwenye mikataba ya wazawa, unamcheleweshea hata miaka miwili kila siku wanajikomba maofisini. Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza mpango mzuri, lakini kuusimamia hatuwezi, na mimi nimwombe Profesa, nimeona amesema anataka kuwaimarisha wakandarasi wa ndani. Hivi kwa nini kuna kazi tunaweza tukasema kuanzia hata shilingi bilioni 50, hata shilingi bilioni 100 zote wapewe wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweka kazi, unawashindanisha na wageni. Wageni wanajua ku-lobby, wana-lobby, halafu wakandarasi wetu wanabaki kuhenyeka na vumbi na kulipa hatuwalipi. Hii siyo sawa. Kama kweli tunakubaliana kwamba tunataka kuimarisha wakandarasi wetu wa ndani, ni vizuri tukatenga kiasi cha fedha kama shilingi bilioni 50 au shilingi bilioni 100. Hizi zisishindaniwe na wageni, zishindaniwe na wazawa. Hapo ndipo tutakapoimarisha uchumi wa nchi yetu kwa sababu pesa yote itabaki huku kwetu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi sana kusikia Wenyeviti wa Bodi sasa wataingia kwa kushindana. Hili ni jambo zuri sana na mimi leo ni kama mara ya nne ninazungumza. Mwenyekiti wa Bodi ndiyo mbeba maono. Sasa mara nyingi imekuwa kama cheo cha shukurani. Mtu anastaafu na miaka 70, kashindwa kufanya kazi vizuri akiwa kazini, ameshakuwa mstaafu, maisha yamempiga kule, unamchagua tena unampa bodi, hana atakachopoteza na muda wake wa Mungu umeshafika miaka 70. Kwa hiyo, anaenda pale kukaa tu na kusinzia, matokeo yake tunaanza kusumbuana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Ninafurahi waingie kwa ushindani, lakini na umri pia. Mtu akishastaafu anatakiwa apumzike, mawazo mapya yaingie. Ninatoa mfano mmoja, tulipata Mwenyekiti kwenye Kamati yetu ya Nishati, Nyansaho ambaye sasa ni Waziri wa Ulinzi, ni kijana. Kapiga kazi vizuri, kapelekwa NSSF. Kapiga kazi vizuri, leo ni Waziri hapa. Sasa unachukua mtu amesha-expire, tena unamtundika kazi ya kuzurura, haiwezekani. Anataka kwenda akajiridhishe mradi, anataka kwenda sijui Liganga na Mchuchuma, ukiangalia hapa ana pingili zimechengana, basi anafanyia kazi kwenye simu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani hili wazo ni zuri kabisa kwamba ipatikane hiyo kazi kwa ushindani, lakini pia na umri uwepo kwamba tunashindana na watu wa design gani? Ukishindanisha watu wameshastaafu, ana uwezo hawezi ku-compete na kijana wa miaka 45 katoka Chuo Kikuu, lakini ana mawazo mazuri. Kwa hiyo, ninaomba sana, hilo tuliweke kama ninavyoshauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni utekelezaji wetu wa mipango. Mipango inakuwa mizuri, lakini kama Serikali inakuwa haiongei lugha moja, ni tatizo. Ninatoa mfano wale mnaotoka Dar es Salaam, sisi tulipanga vizuri, tutajenga barabara za mwendo kasi; na tutajenga barabara za njia nne. Ninyi mnaopita ile barabara, ukishuka Airport niambieni mmefananisha na nchi gani ile barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazunguka wote huko duniani. Nchi gani unatoka Airport vizuri, ukishaingia hiyo barabara ya kwenda Posta, yaani gari inaenda hautulii, inazunguka hivi, inazunguka hivi, wakati huku mliacha eneo? Ramani mliitoa wapi hiyo ya njonginjongi, hizo kona kuanzia mwanzo mpaka mwisho, eeh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunatengeneza Barabara kwenda mpaka Tegeta. Kwa hiyo, chukua mfano mtu anayeishi Tegeta, akitoka Airport ya Dar es Salaam zile kona unahesabu moja mpaka utafika Tegeta kona 100 concentration ya kustarehe kwenye gari hamna. Huo Mpango ulitengenezwa na nani? Mlijifunza wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwashauri sana ndugu zangu, kwa kweli tunafika mahali tunaona sasa kama Serikali haizungumzi lugha moja. Ni vizuri ikawa na lugha moja, wanapotengeneza Mpango washirikiane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga barabara, baada ya miezi miwili au mitatu unaona tena wengine wanakata barabara, wanapitisha waya wa umeme; wanakata barabara wanaweka mabomba; jamani eeh! Kwani kwenye mipango yao hawajui kama huku kuna watu, huku hakuna watu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani hiki kitu tunafika mahali kushauri kwa kweli mtaona kama tunawapinga, lakini ndugu zangu hasa waliobahatika, ma-engineer na wasomi tuliowaamini kwenye Wizara, watengeneze mpango wa pamoja, washirikiane. Wanapotengeneza, kila mtu alete hitaji lake, wanapotaka kutengeneza kitu kimoja, lakini siyo tunatupa fedha leo, baada ya wiki moja tena, unakuta grader zinalia, tunapitisha bomba la maji kupeleka kulia. Hili ni Taifa la wasomi, na sisi tunawaamini. Tengenezeni vitu vya kisomiki, msitengeneze vitu vya blah blah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa kwenye Kamati ya Nishati muda mrefu, tumeshauri kwenye Madini. Mwaka 2017 ukiangalia makusanyo yaliyokuwa yanakusanywa kwenye dhahabu, leo tunachangia 10%, lakini kuna vitu tunazungumza leo mwaka wa tatu tupo humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Waziri Mavunde hapa akasema Vision 2025/2030 tunanunua ndege tupime. Eneo letu limepimwa 16%. Tunaimba kila siku, leo mwaka wa tatu bado tuna-order ndege. Hii ndege inatengenezwa wapi? Tununue ndege ili tupime, tukusanye dhahabu. Ninyi wenyewe mmeona mafanikio kutoka sifuri; leo tuna tani 17 ndani ya miezi 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona ng’ombe anatoa maziwa, mlishe na majani ili maziwa yatoke mengi. Sasa tunakuwa tunapanga vitu halafu kukamilisha hatukamilishi, sasa hii inakuwa kiukweli siyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Profesa, mimi ninamwamini sana. Profesa, nina imani atasimamia vizuri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninaomba nizungumze. Mimi ni Mbunge wa awamu ya tatu na nilikuwa ninafuatilia sana Bunge…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: …hasa Wabunge wanaotokea Kanda ya Ziwa. Wabunge, wanaotokea kanda ya ziwa tumezungumza suala la Airport…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, kuna Taarifa.

TAARIFA

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpa taarifa kaka yangu Musukuma, mtu bingwa wa Jimbo la Geita. Nimpe tu taarifa kwenye kile alichokuwa anazungumza kuhusu madini, mimi ndio mchimbaji mdogo katika nchi hii. Ninapenda kumpa tu Taarifa kwamba juzi Mheshimiwa Mavunde, Waziri Makini wa Wizara ya Madini, amerusha ndege ya Barrick kwa ajili ya uanzishwaji wa kupima maeneo kwa ajili ya madini, alikuwa hajapata hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamkaribisha Bungeni. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, mimi sizungumzii ndege ya Barrick, nazungumzia ndege ya Serikali, ya kwetu wenyewe. Hatuwezi kutumia ndege za kuazima watu. Kwa hiyo, karibu na ninakushukuru sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kushauri. Kwa kweli, tufike mwisho. Hebu oneni aibu. Mimi nimekuja hapa mwaka wa 15, kulikuwa na Wabunge, na Wabunge, na Wabunge tunazungumza Mwanza International Airport. Kwani hamwoni aibu! Yaani kila mwaka mnatuambia tunakarabati. Profesa Mbarawa yupo hapa, alinialika kwenda kutia saini, tukazungusha na mabati, tukafanya na sherehe, tukapiga na ving’ora, sasa hivi mmeng’oa tena na mabati na mkandarasi hayumo. Hivi jamani mnatuonaje eh? Mpaka tuongee nini sasa ili mjue kama mnatukera eeh?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli sisi Mwanza ni watu wa kuzidiwa na Airport ya Arusha Mjini ndogo ile? Airport ndogo, mnaweka mavioo, mnaweka manini, sisi mnatuzungushia mabati! Hapana. Profesa niwaombe tufike mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sehemu yenye uchumi mkubwa kwenye mambo ya ndege ni Mwanza, lakini tunakuwa wa mwisho, tunazidiwa mpaka na Ibadakuli. Mpaka tuongee nini sasa? Tuongee nini? Sehemu ambayo mnapeleka ndege moja kwa wiki, tunajenga majengo mazuri, tumejenga runway kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ambayo tunapeleka ndege mpaka dreamliner, tunakaa tunaongea kitu hakifiki mwisho. Mnapanga mipango mwaka huu, tunakuja tunapangua tena, tunaweka mwingine, tunapangua. Ni nini kimetokea mpaka mmemwondoa mkandarasi aliyekuwa pale? Ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlizungusha mabati, tumeshindilia, tukaanza kung’oa vioo. Sasa hivi vioo vinaanguka, mkandarasi naye ametoa vitu. Jamani, fikeni mahali mwone huruma. Nasi ni kipande cha hii Serikali, na tunauchangiaji mkubwa sana kwenye mapato ya hii nchi, na sisi ndio tunaongoza kusafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa ndio tunaongoza kusafiri. Tumejenga mpaka Uwanja wa Musoma, tunauzindua; wa Mwanza ni stori, ni swagger. Tukishuka pale na Dreamliner, hamna hata pa kujikinga, wageni wanaloa na mvua. Au nani ameturoga kwenye huu uwanja wetu wa Kanda ya Ziwa? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana tufikie mwisho. Tunapopanga mipango ifike mwisho. Profesa kama na mwakani tena tukiwa hai, akija tena na Mpango wa 2027/2026, tunaupiga chini. Mimi nikueleze ukweli.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ahsante, muda wako umekwisha…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ahsante. (Makofi)