Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Mpango huu wa Serikali. Nitakuwa na mambo machache ya kuzungumza. La kwanza, ninaipongeza Serikali kwa Mpango wao mzuri na hususan Mwalimu wangu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mheshimiwa Prof. Kitila kwa uwasilishaji mzuri wa Mpango pamoja na Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuzungumza. La kwanza, ninalotaka kuzungumza ni kushauri. Kwanza kushauri kwenye utekelezaji wa Mpango, tunapokwenda kutekeleza Mpango huu, ni vyema tukaangalia wapi ambapo tumekwama? Moja kati ya maoni ya Kamati wanayoyazungumzia kwenye utekelezaji wa Mpango ni kwamba kuna mambo mengi hayajamalizika, na tunaenda kuanzisha mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hoja kubwa sana kwenye Kamati wamelizungumza na hii inaendana na kwamba kukosekana kwa kitengo cha tathmini (Monitoring and Evaluation) ndicho kinacholeta haya ambayo yanaoonekana tunaanzisha mambo mengi katika Taifa na mengine hayajakamilika kiasi kwamba wananchi wanakuwa hawaoni tija ya utekelezaji wa Mpango husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Waziri, na Serikali. Cha kwanza ni kufanya tathmini, ni miradi ipi imekamilika na miradi ipi bado haijakamilika? For instance, kwenye miradi ya barabara, kila Mbunge akisimama hapa ndani anazungumza kwamba tumefanya sherehe kwenye kusaini mikataba, lakini barabara hizi hazijatekelezwa na hazijaanza kujengwa. Ukienda kwenye miradi ya maji, ukienda kwenye miradi mingine mbalimbali, sasa ni vyema Serikali ikafanya tathmini ya miradi yote ambayo haijakamilika, tukamilishe ili tulete tija kwa wananchi waone kwamba Serikali imefanya kazi. Kuwa na viporo vingi vinaisababishia Serikali iwe na mzigo mkubwa inaopoenda kuanzisha na miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais, amejikita kwenye kuongeza ajira, tafsiri yake ni kwamba, wage bill inaenda kuongezeka. Mkienda kuanzisha pia miradi mingine, mnakuwa na mzigo mkubwa sana wa kutafuta fedha kiasi kwamba hiyo mingine inaenda kukwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashauri kwenye utekelezaji wa mipango, tufanye tathmini ya hii miradi ya kimakakati ambapo tumeona kabisa kwamba Serikali inaenda kujikita kwenye sekta ya uzalishaji. Hatuwezi kwenda kwenye uzalishaji kama barabara hazijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwenda kwenye uzalishaji kama miradi ya maji kwenye umwagiliaji haijakamilika. Hatuwezi kwenda kwenye uzalishaji kama sekta ya afya na huduma bora kwa wananchi hazijakamilika. Kwa hiyo, ni lazima kitengo cha tathmini na ufuatiliaji kiwekewe mkazo na kitungiwe sheria kiwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Mheshimiwa Rais ya kuanzisha Wizara ya Mipango ilikuwa ni kuona haya mambo yanaenda kufanikiwa. Sasa haiwezekani tukawa na Wizara ya Mipango na bado kwenye utekelezaji wa mipango tunakwama kwa sababu hakuna tathmini. Kwa hiyo, ninashauri ni muhimu tuwe na hicho kitengo cha tathmini na ufuatiliaji ili kuangalia jinsi gani miradi yetu inaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza, kwa mfano tu Wilaya ya Makete, barabara ya kutoka Makete kuelekea Mbeya, yenye takribani miaka minne toka tumesaini mkataba, centimeter moja ya lami haipo hadi leo. Sasa huu ni mfano tu, lakini barabara ya kutoka Njombe kuelekea Ludewa ni same case, barabara kutoka Lupembe kuelekea Morogoro ni same case. Barabara ya Mbeya Mjini pale kwa muda mrefu ime-stuck. Sasa ni vyema Serikali ikafanya tathmini kwenye hii miradi, ikakamilisha ili tuweze kwenda kwenye hatua nyingine ili miradi iweze kuwa na tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ni kwenye vyanzo vya mapato. Hii mipango tunaizungumza kwenye utekelezaji wa mipango hii. Mipango hii haiwezi kukamilika kama hatuna fedha. Serikali yoyote duniani, cha kwanza lazima tujikite kwenye ukusanyaji wa fedha. Ukiangalia kwenye Mpango wetu, tunakiri kabisa na Kamati imekiri, 70% ya Mpango inaenda kutekelezwa na sekta binafsi. Sekta binafsi ndiyo inaenda kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Rais, kwa sababu ni maono makubwa kwenda kuibeba sekta binafsi. Sekta binafsi ni engine ya uchumi popote pale. Nyinyi kama Serikali hamwezi kufanikiwa kutekeleza miradi hii yote bila kutegemea sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye utekelezaji wa mpango huu lazima tuangalie vyanzo vya mapato. Mheshimiwa Waziri hatuwezi kuepuka kabisa kutafuta namna ya kupata fedha kupitia kwenye e-economy, kwenye digital economy, hii ni mifumo ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kuhusu Serikali kuwa na mifumo inayosomana, lakini kuachana na utaratibu wa kukusanya fedha kwa taslimu. Niipongeze Kamati ya Bajeti wameandika kabisa, kukusanya fedha kwa mfumo wa taslimu ni upotevu wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima twende kwenye mfumo wa kukusanya mapato kupitia mifumo na zaidi tupunguze idadi ya mifumo kuwa mingi Serikalini. Mifumo lazima isomane, ili mapato yaweze kutekelezeka. Ninampa tu mfano Mheshimiwa Waziri, ukusanyaji wa fedha kwenye Daraja la Mwalimu Nyerere; wakati wanakusanya fedha kwa taslimu walikuwa wanakusanya shilingi milioni 150, milioni 600, lakini kwa kukukusanya kupitia mfumo wanakusanya zaidi ya 1.5 billion ndani ya mwaka mmoja. Maana yake ni kuna fedha nyingi zilikuwa zinapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwenye Hospitali ya Tumbi pale, Dar es Salaam, walivyokuwa wanakusanya kwa taslimu walikusanya shilingi milioni 30, milioni 40, lakini sasa hivi kwa mwaka ni shilingi milioni 600, baada ya kufungiwa mfumo wa GoTHOMIS kuhakikisha kwamba, wanakusanya fedha kupitia kwenye mfumo. Sasa ni hospitali ngapi, ni maeneo mangapi, ambayo fedha hazikusanywi kwenye mfumo, zinakusanywa kwa taslimu na zinapotea? Kwa hiyo, Serikali ni lazima iangalie ni namna gani ya kuhama kabisa kuachana na ukusanyaji wa fedha kupitia kwenye hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia TEHAMA, Mheshimiwa Waziri, ni lazima iendane na speed ya internet. Sisi hapa tumekuwa ni mashahidi tunaenda kwenye kulipia hati unaambiwa mfumo uko chini, unaenda kulipia TRA unaambiwa mfumo uko chini. Taifa letu, kama dunia inakimbizana na ukusanyaji wa mapato kupitia mifumo, ni vyema tukaangalia kuboresha upatikanaji wa internet nchini yenye speed, yenye standard, ili hii mifumo iweze kukusanya fedha kwa uhakika na mapato yasiweze kupotea. Kwa hiyo, hilo ninaomba sana lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia TCRA wanahitaji kama shilingi bilioni 480 ninadhani, ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kufanikisha hili jambo. Ninatumia nafasi hii kuwaomba kuimarisha TCRA, ili mifumo iweze kukusanya mapato na pia, kuweza kuboresha internet kwenye Taifa letu. Tunapozungumza, Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la ukusanyaji wa mapato kupitia mifumo kuna namna nyingine ya kuangalia kupitia madini, kama ambavyo Serikali tumeona inafanya kazi ya kununua gold na kuhifadhi kwenye BOT. Bado wachimbaji hapa wamekuwa wanaomba pia, benki zitengenezewe wigo kuhakikisha kwamba, wao pia, wanakuwa na uhifadhi wa madini kwenye benki, kama wanavyohifadhi fedha. Hii yote ni kuhakikisha kwamba, uchumi unaendelea kuimarika na mipango yetu inaenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni ambalo linahusisha upotevu wa mapato. Hatuwezi kutekeleza miradi hii kama rushwa itaendelea kushamiri kwenye Taifa letu. Mikataba mingi inaigharimu fedha. Ukiangalia Mheshimiwa Waziri tunatumia fedha nyingi kwenda kulipa watu ambao wameingia mikataba, ambayo baadaye imegeuka kuwa mizigo kwenye Taifa kutokana na kwamba, tumeshindwa kuitekeleza kwa wakati na zaidi rushwa kushamiri kwenye kusaini mikataba na kuliumiza Taifa. Tutakwamisha utekelezaji wa mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, accountability kama haiwezi kuchukua nafasi kwa Watumishi wa Serikali hatuwezi kufanikiwa kutekeleza kwenye hii miradi, lazima watu wawe accountable. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kuja na mfumo wa kushindanisha watu kupata watu bora kwenye usimamizi wa wakurugenzi wa hizi taasisi na mambo mbalimbali. Kwa sababu, kati ya eneo ambalo Serikali imekuwa iki-inject fedha ni kuwekeza hizi taasisi mbalimbali ziweze kujiendesha, lakini tuna-inject fedha mwisho wa siku zinaliwa na mafisadi. Sasa ni lazima Serikali iangalie ni namna gani ya kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa accountable na tunasimamia suala la upotevu wa mapato kupitia rushwa na kutokukusanya fedha kupitia mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kushauri ni kuhakikisha kwamba, ndani ya Serikali tuna Wizara ya Vijana, ile pale, hakuna mpango unaweza kufanikiwa dunia hii, kwenye nchi yoyote, bila kuangalia Wizara ya Vijana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, cha kwanza, ndiye champion kuelekea mipango ijayo ya miaka 50 kwa kuanzisha Wizara ya Vijana. Sasa ukisoma kwenye ripoti mbalimbali inaonesha Tanzania tuna Mifuko zaidi ya 70 kwenye Wizara mbalimbali inayohusika na Wizara ya Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatuwezi kuwa na Wizara ya Vijana, lakini kuna Wizara nyingine huko zimekaa na mifuko ambayo inasimamia Wizara ya Vijana. Ni wajibu na ni muhimu kwa kipindi hiki Wizara zote ambazo zina mifuko mbalimbali ambayo inahusisha vijana mifuko hiyo ielekezwe kwenye kapu moja isimamiwe chini ya Wizara ya Mheshimiwa Joel Nanauka, Wizara ya Vijana na Maendeleo, ili angalau kwenye hili kapu tukisimamia tuwe tuna uwezo wa kufanya monitoring kwamba, ni Mfuko gani na Mfuko gani haujafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye hii mifuko 70, kwenye ripoti, inaonesha tumekopesha zaidi ya shilingi trilioni 3.5 kwa vijana zaidi ya 24,000,000. Sasa kama tumekopesha hizo pesa na vijana nje wanalalamika ajira hazijapatikana, ni nani anayekula hizo fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na kapu moja ambalo linaweza lika-control Mifuko yote, ambayo inaweza ku-support vijana kwenye nchi yetu. Tofauti na hapo kufanya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa na Mfuko wa Vijana, Wizara nyingine tena ina Mfuko wa Vijana, hii mifuko ilivyosambaa kwenda huku ndipo tunaruhusu kuonekana ule utendaji kazi wa hii mifuko usiwe na tija. Kwa hiyo, ni lazima Wizara ya Vijana iwezeshwe iweze kupewa hiyo Mifuko yote isimamiwe ndani ya kapu moja, ili Waziri wa Vijana awe na nguvu ya kufanya hiyo kazi. Hayo ni maoni yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ninaendelea kushauri kwamba, sekta ya kilimo ni vyema pia ikaendelea kuwezeshwa kwa sababu, ni eneo ambalo katika nchi yetu linaongeza sana kwenye suala la uzalishaji. Mvua imeanza kuwa inakata kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, kwa hiyo, tumejikita kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunatamani sana tuendelee kuweka fedha nyingi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ili wakulima wetu waweze kubadilisha mazingira ya kutegemea mvua, sasa wawe na uwezo wa kutegemea maji kwa msimu mzima tuweze kulima kwa sababu, bila kilimo Taifa letu litapata wakati mgumu na pia, sekta nyingine zitakwama. Kwa hiyo, ninaendelea kuhamasisha kwamba, tunavyohamasisha kilimo, tuhamasishe pamoja na barabara za TARURA.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani dakika zimeisha?

MWENYEKITI: Ndyio, muda wako umekwisha Mheshimiwa. Ninakushukuru.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah! Sijaanza hata kuchangia. Ahsante. (Makofi/Kicheko)