Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Kabla sijachangia ninaomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kurudi hapa Bungeni na niwashukuru sana wananchi wema wa Jimbo la Hai kwa kunipa heshima nyingine ya kuwa Mbunge wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kushukuru chama changu kuanzia ngazi ya Taifa, Mwenyeketi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mpaka ngazi ya Mwenyekiti wa Shina kwa kunipa hii heshima. Ninawaambia tu yale ambayo tulifanya miaka mitano iliyopita na sasa tunaenda kufanya zaidi ya hapo na wao ni mashahidi. Hivi ninavyoongea, kwa kipindi ambacho tumeingia, tayari mkandarasi yuko site anajenga Soko la Kwasadala, mkandarasi yuko site anajenga Soko la Mula, mkandarasi yuko site anajenga Ofisi ya Wilaya ya Hai, mkandarasi yuko site anajenga nyumba ya Mkurugenzi. Hii ni miradi mipya ambayo tumeanza nayo na hiyo ndio speed ya Mama Mheshimiwa, Dkt. Samia na tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuchangia hotuba hii, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waziri, hotuba imeandikwa vizuri, kitaalamu kabisa, hii inadhihirisha uprofesa wake. Ninampongeza sana na wasaidizi wake, pamoja na Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma mpango huu vizuri, umesheheni takwimu na unaonesha kweli dira. Nimesoma Mpango wetu wa Taifa wa Miaka 50 kweli, unawiana na takwimu zipo za kutosha kwa kweli, lakini Mheshimiwa Waziri nina jambo ninataka kushauri, namna ya kuweza kushusha mpango huu kuuleta chini na vitu viweze kuwa halisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kutambua uwezo wa Waziri na wasaidizi wake, lakini nimekuwa nikishauri hapa tutengeneze timu ya wataalam, watafute jina lolote watakaloita, hawa wataalam wakae chini wawe ndiyo watu wanaofanya tathmini ya mipango yetu na wanaojibu maswali magumu yanayohusu Taifa letu. Walipwe vizuri, wawe nje ya utumishi wa umma tuliouzoea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuanza kwa sababu, ninajua yanahitajika mabadiliko ya kisheria, tunaweza kuanza na lab za wataalam wakutane na jopo la wataalam kutoka sekta zote wakae watafute majawabu. Kwa nini tuna Ziwa Victoria, lakini ukienda watu wa Mwanza, watu wa Ilemela, bado wana shida ya maji? Hapa Dodoma tunaambiwa water table ipo kubwa na maji ya kututosheleza, kwa nini hatuna maji? Kwa nini, tukitoka hapa Dodoma kwenda kuikuta Singida mashamba yako ya kutosha, lakini ukiangalia takwimu zinaonesha hali ya ukosefu wa chakula, umaskini wa chakula ni asilimia nane?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa timu hii ikae vizuri tutafute mfumo wa kuajiri wataalam hawa. Ninaamini nchi hii bado ina vijana wengi wenye uwezo mkubwa, wachaguliwe kwa sifa zao, wapewe security of tenure ya kutosha, ikiwezekana twende Masaki pale tuwatafutie nyumba za kukaa tuwape magari mazuri, watoto wao tuwalipie ada, wakae wawe ni watu free from politics wawaze na watutafutia majibu. Waje na theories, wazipime, tuje kwenye utekelezaji, ndiyo mambo haya mazuri yanaweza kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa sababu, ukitazama mambo haya yalivyo mengi yanachangiwa, yana falsafa ya kwako wewe mwenyewe, kama Profesa kesho akiwa hayupo tunayawekaje? Tuna ya ring fence vipi, lakini, kukiwa na hiyo intellectual team itahakikisha haya mambo, tutawapa nguvu ya kisheria, watayasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nianze na hilo, lakini nimesoma taarifa hii, ninarudia tena, ukurasa wa sita umesema hali ya umaskini wa chakula ni asilimia nane. Sasa ninajiuliza mpaka leo tunahubiri hali ya umaskini wa chakula kwa nini? Taifa lenye watu wasomi namna hii!

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeonesha pale namna ambavyo wamekuza eneo la umwagiliaji. Ninaomba kama kuna eneo ambalo linaweza ku-capture Watanzania wengi ni kilimo. Tuondoke kwenye kilimo cha karatasi twende site tukalime kwelikweli, tuweke mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri tungeweza ku-site zone, labda tuseme Ukanda wa Kaskazini, mikoa hii izalishe mazao ya aina fulani twende tukuze umwagiliaji tuhakikishe maji ya kumwagilia yapo. Mle ndani tuweke viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na kila Mkuu wa Mkoa apewe jukumu kwamba, wewe tunahakikisha kwa mwaka huu tunataka tani kadhaa za mahindi, za maharage; tukienda hivyo itatusaidia. Tutaongeza uzalishaji na sisi tutauza mazao nje ya nchi, pato hili la Taifa tunalolizungumza litakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huohuo naomba kule Wilaya ya Hai, sisi ni wakulima, tuna eneo dogo, lakini tuko tayari kulima kisayansi. Ninaomba wekeni kwenye mpango, tunajua tuna skimu ambazo zimeshafanyiwa feasibility study; Metromu, Makeresho, Bwawa la Borutu na nyinginezo, tuleteeni fedha kwenye skimu hizi, ili sisi Wilaya ya Hai tuwaoneshe kilimo kinavyolimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tuna Soko la Kwasadala pale na ikumbukwe ardhi yetu ni ndogo. Kwa hiyo, hizi skimu zikijengwa pamoja na Skimu Ndogo ya Ngusero, Mkalama, Kilanya na pale Urara, tukipata sisi tutawaonesha kwa vitendo na mimi Mbunge nitatangulia mbele, namna ya kuongeza uzalishaji, lakini profesa anafahamu katika dhana hii hii, ili tuondokane na neno umaskini wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Prof. Mbarawa anajua tulimaliza mgogoro pale KIA, wananchi wameondolewa na tumekubali, lakini ndiko tulikokuwa tunalima. Kwa sasa hivi hawahitaji hekta zote 11,000, kule Chekimaji kuna maeneo ambayo wananchi walikuwa wanalima wameondolewa. Ninaomba turudi kwa mkataba maalum tulime, kama tunavyofanya kwenye mashamba ya NDC pale Kilimanjaro Machine Tools, ili tuondokane na hali hii ya chakula. Vinginevyo, Mheshimiwa Profesa Mbawara na Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, wajiandae tutakuja kuwaomba chakula. Hili jambo sidhani kama ni gumu kiasi hicho, tupo tayari, tunatambua ni maeneo ya KIA, watupe maeneo tukafuge, watupe maeneo pale tukalime kwa mkataba maalum na tuko tayari kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni sambamba na mpango wa maendeleo. Tumezungumza hapa na bahati nzuri Serikali imekubali, Kiwanda cha Kilimanajro Machine Tools, ninafahamu suala la makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma linaendelea vizuri, wakimaliza kile kiwanda wakifanye cha kuzalisha chuma. Waziri wa Viwanda anatikisa kichwa, ninamshukuru wa biashara pale. Maana yake ni hiki kitu na bahati nzuri ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kwamba, kile kiwanda kitahamishiwa mahali kwenye benki ya ushirika, ili kiweze kuzalisha. Wakati tukiwa mbioni kusubiri chuma tuanze sasa kile kiwanda kukitanua, ili kiweze kuzalisha chuma kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona kwenye mpango wamegusa eneo la vijana na wakatoa takwimu kwamba, kwa mwaka 2025 vijana 62,570 wanamaliza vyuo vikuu. Nikajaribu kutafuta, kwenye mpango, hawa vijana 62,000 wanaomaliza vyuo vikuu mpango wao uko wapi? Wanaenda kuishia wapi? Tunampongeza Mheshimiwa Rais ametengeneza Wizara ya Vijana, lakini ninaomba, waende wakakae tena, hawa 62,000 wakija mtaani wanaenda kufanya jambo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu pekee ambayo ninaiona kwa haraka haraka, pamoja na viwanda na vitu vingine, ni kwenye kilimo. Tuwahamasishe vijana wawekeze kwenye kilimo na kwamba, mkulima isionekane ni adhabu au ni mtu wa chini. Wale waliofanikiwa kwenye kilimo watumieni kuwashawishi na kuwahamasisha vijana wahamie kwenye sekta ya kilimo, ndiyo itakayotusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni pamoja na kurudisha vile vyuo vya kati vilivyokuwepo virudi kutoa elimu kwenye ngazi ya kati. Hii population ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu, kama hatutaiangalia vizuri, hili ni bomu lingine linalotujia. Hawa vijana wana maono yao, wasipopata majawabu sahihi, ndiyo maana tunasema, hiyo intellectual committee, hicho kikosi kazi kiende kikatafute majawabu. Hawa vijana wanaomaliza vyuo vikuu baada ya kumaliza wanaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa harakaharaka sana ninaomba ule mpango wa kuanzisha treni ya umeme kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha waukimbize. Wanajua mikoa hii ya kaskazini ni hub pia, ya uchumi wetu. Tuombe hilo na lenyewe walitazame liende kwa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana Serikali imefanya miradi mingi mikubwa, lakini kuna jambo ambalo sijaliona kwenye mpango vizuri, mpango wa matengenezo ukoje? Tumejenga shule nyingi, mpango wa matengenezo na ku-maintain? Tuna miradi mikubwa hapa, SGR, mpango wa matengenezo ukoje ili inapotokea kuna kitu kimeharibika kusiwe na fedha, tena tuanze kuhangaika. Hii miradi yote tunayoijenga, shule na nini, tuiweke kwenye mpango, kuwa na fedha ya matengenezo ili miradi yetu iweze kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunaelekea mwishoni, ninaomba sana Local Government Authority iacheni ifanye kazi yake, iacheni i-enjoy autonomy yake. Local Government inaingiliwa sana, tuwape nguvu Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Madiwani wafanye kazi yao kwenye jurisdiction yao. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaongezee nguvu tena ya fedha, kama posho yao. Ninafahamu ni jambo kubwa, lakini tufikirie namna ya kuongeza posho ya Madiwani, posho ya Wenyeviti wa Vijiji, posho ya Wenyeviti wa Vitongoji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwape wa-enjoy full autonomy, kama Local Government maana inaingiliwa sana na Central Government. Madiwani wanapanga hivi, anakuja mtu wa Central Government anapanga hivi, wakati wenye wananchi ni Madiwani.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha. Tunakushukuru kwa mchango wako.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)