Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Jafari Wambura Chege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kutoka kwa Waziri Profesa Mkumbo, lakini pia nipate nafasi ya kuchangia mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya bajeti kutoka kwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kusema ninaunga mkono hoja zote mbili na ninakubaliana na maono yao mazuri yaliyopo kwenye taarifa zao zote mbili kwa Mawaziri hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia na kukubali kuanzishwa mchakato wa Dira mpya ya Taifa ya mwaka 2050. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mambo makuu matatu. Moja kwa kutekeleza maono ya Dkt. Samia, maono ya Watanzania na mwelekeo wao na dhamira waliyokuwa nayo juu ya kupatikana kwa dira mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kuandaa mpango elekezi na dira yenyewe, kiukweli amefanya kazi kubwa nzuri kama ambavyo tunatambua changamoto ya Dira ya mwaka 2025 ilikwenda kwa kusuasua kwa sababu ya kukosekana kwa mpango elekezi wenyewe ya namna dira inavyokwenda kutekelezwa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hilo. La pili, nimpongeze pia kwenye taarifa yake kwa kutambua umuhimu wa wawekezaji hasa wazawa na kurudi kuangalia namna ambavyo Serikali inapaswa kushirikiana na private sectors bila kuwaacha wazawa katika kuinua uchumi wetu kama watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili Mheshimiwa Waziri aende alitazame upya pamoja na kwamba wazawa wanaruhusiwa kufanya kutekeleza miradi iliyo chini ya bilioni 50, ninashauri Serikali ipanue wigo iende zaidi ya bilioni 100 mpaka bilioni 200 kwa sababu ninaamini tunao wazawa ambao wana uwezo mkubwa wa kufanya haya. Tatu, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwenye taarifa yake na ndiyo jambo muhimu sana la kuanza la kupendekeza walau Wakurugenzi wa Halmashauri kupata nafasi kulingana na uwezo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu nimeona kwenye Kamati pia wamekwenda mbali wameshauri Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali na Mashirika ya Umma nao waende watazamwe katika nyanda hiyo, wateuliwe kulingana na nafasi zao ili tuweze kuwapima kulingana na ukuaji wa taasisi zao na utendaji wao wa moja kwa moja. Kwa hiyo, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa hii. Nina maoni kadhaa kwa malengo mahususi katika dira. Yapo malengo mahususi manne, lakini nitajikita leo kwenye lengo moja tu la maisha bora na ustawi wake kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza dhana ya maisha bora, kama taifa linaloendelea tunatambua yapo maeneo kadhaa ambayo Serikali kwa ujumla wake inapaswa kujikita ili kuinua uchumi wa wananchi kwa ujumla wake. Wizara hii imeonesha mwelekeo na njia ya kupita, ni kazi sasa ya wizara za kisekta kuchukua maono ya wizara hii ya mipango na uwekezaji, kuyachakata na kuyaingiza kwenye mipango ya wizara za kisekta ili yaende yakashamiri na yasambae kwa wananchi kwenye maeneo yote kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo hayo nilitaka nijikite kwenye maeneo kadhaa. Mfano, tunapozungumzia maisha bora ni lazima uzungumze maisha bora kwa wananchi kwa kutazama miundombinu ya barabara inayozunguka wananchi wale. Katika miundombinu ya barabara lazima tuiangalie kwa nafasi mbili tofauti. Lazima tuangalie barabara zinazosimamiwa na TANROADS, lazima tuangalie barabara zinazosimamiwa na TARURA katika kutekeleza na kupunguza minong’ono na kuimarisha Maisha bora kwa ustawi wa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi, kuna baadhi ya meneo mengi sasa barabara imekuwa ni changamoto kubwa sana na Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa, zipo barabara ambazo zimetangazwa, wakandarasi wapo site, wanatekeleza, zipo barabara ambazo zimesaini mikataba, wakandarasi hawajaingia site na zipo barabara ambazo zipo kwenye procurement process kwenye maeneo mbalimbali. Lazima tukubaliane kwa kuwa Wizara ya Fedha imesema hapa imetoa mwelekeo wake wa uandaaji wa bajeti, watenge fedha ya namna ya ukamilishaji wa barabara hizi kwenye maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko barabara ambazo tunazungumzia maisha bora kwa wananchi zimetajwa kwa awamu nne, tano kwenye maeneo tofauti toka miaka ya 95 zinatajwa barabara zile, mpaka sasa tuko mwaka 2025 tunakwenda 2030. Mfano wa Barabara yangu ya Utegi - Shirati kwenda Kirongwe ni matarajio yangu sasa Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Fedha itatenga fedha kusaidia Wizara ya Ujenzi ili kuimarisha maisha bora kwenye maeneo yale, ili barabara zile ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inapokamilika ndiyo inakwenda kuinua uchumi wa eneo husika kwa sababu kuna barabara zinaunganisha kati ya mkoa na mkoa, wilaya na wilaya na zingine zinaunganisha nchi na nchi. Kwa hiyo, katika kuimarisha na kutengeneza maisha bora lazima uweke fedha ya kukamilika kwa barabara ile ili wananchi waweze kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni utekelezaji wa miradi ya maji nchini. Niombe sana Wizara husika ya sekta ya maji, ifanye tathmini ijiridhishe badala ya kuwa na tathmini ya namna tumetatua maji kwa asilimia ngapi iangalie upatikanaji wa maji kwenye maeneo yale. Yako maeneo ambayo yana miundombinu ya maji, tunayahesabu kama asilimia katika kutekeleza mpango kazi wa maji, lakini maji hayatoki kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wito wangu ni nini, Wizara ya Maji, kwanza ihakikishe miradi ya maji iliyoanzishwa inakamilika, inakwenda, inafika mwisho na inatoa maji. Mbili, wafanye tathmini kwenye miradi ambayo tayari walipeleka miundombinu badala ya kuihesabu kwenye asilimia ya utekelezaji wa maji wajiridhishe kama miradi hiyo kweli inatoa maji na wananchi wananufaika kwenye yale maeneo. Wakifanya hivyo, maana yake watakuwa wanakwenda kwenye ile itifaki ya maisha bora na ustawi wa wananchi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni sekta ya ardhi, hili eneo tumekuwa tukilisahau sana. Kipanga, kupima na kumilikisha tumezungumza kwa mda mrefu sana. Niombe Waziri wa Sekta kwenye awamu hii ya bajeti inayokuja, hili jambo liende lipewe msukumo mkubwa kwa sababu ardhi isiyopangwa na kupimwa kwani ndiyo chanzo cha migogoro ya ardhi kwenye maeneo yetu, maana yake kunakuwa hakuna amani kwenye maeneo yetu. Ardhi yetu inakosa thamani halisi pale inapokuwa haijapangwa, kupimwa na kumilikishwa kwenye maeneo yao. Niombe sana Mheshimiwa Waziri husika, aende alione hili tunapokwenda kuchakata bajeti yake ili waweze kulipa nguvu ili waweze kupata ustawi ulio mzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa jambo la soko la vijana, ajira kwa vijana na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Wizara husika ya Vijana, lakini ningeomba sana Waziri husika pamoja na michakato mbalimbali inayoendelea kwenye Wizara hii, lazima waende wakawa-group vijana, tujue hawa vijana wanaowazungumzia ni kuanzia umri upi mpaka umri gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende pia tukazungumze fursa sawa kwa hawa vijana kwa kutazama mazingira ya vijana wanayotoka. Kijana wa Rorya mazingira yake kwenye fursa hayawezi kuwa sana na kijana anayeishi Dar es Salaam. Kwa hiyo, Wizara iende ikajikite itazame kama inakwenda kusaidia vijana, isaidie vijana kulingana na mazingira ya maeneo yao wanayotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, itazame fursa za kimaeneo hayo wanayotoka hao vijana. Tusizungumze general moja kwa moja kwa kuwa-generalize vijana wote kama vile ni sawa kutokana na fursa wanakotoka. Kijana wa Rorya inawezekana fursa yake isiwe sawa na kijana wa Tandahimba, haiwezi kuwa sawa na kijana wa Kinondoni. Kwa hiyo, ni lazima Mheshimiwa Waziri, aende alione hili namna ambavyo anaweza akaliweka ili litengeneze ustawi ulio mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye mpango, ni kuhusiana na kilimo. Sisi tunazungumza Mkoa wa Mara, leo hii hatuna zao kuu la kibiashara tunalojivunia, tunazo skim mbalimbali za umwagiliaji pamoja na kuzunguka Ziwa Victoria zaidi ya 70%, hatuna skim kubwa ya kuzungumza leo kama kielelezo cha ukuaji wa kilimo kwenye Mkoa wa Mara. Tunatamani Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na mpango huu umekwishaonesha ili waende wakatengeneze upembuzi yakinifu kwenye maeneo yale na sisi tunatamani kupitia mkoa ule tuwe tuna skim ambazo zinawainua wananchi kwenye uchumi na zinaleta manufaa kwenye Wizara hii na kwenye sekta ya kilimo kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri alitazame hili. Mfano, mimi Rorya nimezungukwa na maji 77% lakini ninavyozungumza na wewe hatuna skim yoyote tunayojivunia pamoja na kuzungukwa na maji 77%. Tazama katika 100%, ni 23% peke yake nchi kavu, lakini sina skim yoyote ya umwagiliaji. Kwa hiyo, nikatamani pamoja na kusema, wenzangu wameshauri hapa kuwe na timu ya monitoring and evaluation lakini Wizara ione namna bora ya kusaidia maeneo haya ili waweze kuwasaidia kwenye kilimo, badala ya kubaki na kuzungumza kilimo kwa ujumla wake, lakini maeneo ambayo yana fursa hayanufaiki na kilimo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningetamani nizungumzie juu ya uchumi wa kimaeneo na Mheshimiwa Waziri amelizungumza sana hapa kwamba, pamoja na kwamba tunakwenda kuunda timu ya monitoring and evaluation lazima tuangalie maeneo hasa ya kimkoa namna yalivyokaa, ni fursa zipi za kiuchumi ambazo zinaweza zikaanzishwa zikawanufaisha mikoa husika. Mkoa wa Mara hatuna mradi mkubwa kama kielelezo kinavyozungumza, hatuna mradi wa skim ya umwagiliaji lakini viwanda tulivyokuwanavyo vyote vimekufa. Matarajio yetu ni nini kutoka kwa Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, Serikali ione namna ambavyo kama fursa yetu ni kufufua viwanda vilivyokuwepo vikiwemo viwanda vya nguo, kiwanda cha maziwa na fursa zingine ambazo zinaweza zikainua uchumi wa maeneo yale. Ningetamani sana nione Wizara hii na Serikali ikiona namna ya kuweka fedha kuinua mkoa ule. Kwa sababu, ukifanya hivyo kwanza unainua ajira kwa wale vijana, lakini pia watatengeneza uchumi wa mkoa wenyewe husika, kuliko namna inavyokwenda kwa ujumla wake na sisi kama mkoa tunabaki tukiwa bado hatujapata kitu ambacho tunaweza tukasema tunajivunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninasema tena kwa mara nyingine kwamba, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)