Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi niweze kujadili mpango huu wa maendeleo ulioletwa mbele yetu. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi na wananchi wangu wa Wilaya ya Chunya na Jimbo la Lupa kwa kuweza kunichagua na kunirudisha tena niweze kuwawakilisha. Ninawaambia kwamba tunaendelea pale tulipoishia kuhakikisha kwamba mipango ya Serikali inakwenda vizuri na wao wanaendelea kupata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mpango huu mzuri ambao ametuletea hapa mezani, mpango ambao umesheheni vizuri. Hakika tunaona kwamba PhD yake inafanya kazi vizuri, yeye pamoja na wasaidizi wake, lakini pia na Waziri wa Fedha. Hakika tupo sehemu salama zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu mpango huu ni mpango ambao unaenda kuakisi yale ambayo mipango ya Serikali kwa miaka mitano lakini kwa miaka 50 inayokuja. Hata hivyo, kwenye mipango hii ambayo inaendelea imeweza kueleza mambo kadha wa kadha, imeweza kugusa vizuri kila sekta na wananchi huko nje kila mmoja ameweza kuisifia hii hotuba. Jambo kubwa ambalo liko mbele yetu waweze kuona matokeo ya hii mipango ambayo imeelezwa kwenye hii hotuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona namna ambavyo ukitaka kuhakikisha kwamba uchumi unaendelea kuwa vizuri zaidi na kwenye mpango imeeleza namna ambavyo kwenda kuiwezesha sekta binafsi. Sekta binafsi ukuaji wake ambao tunategemea kwamba, zaidi ya 70% tunaweza kupata mapato kutoka kwenye sekta binafsi hasa kwenye upande wa ajira, lakini kwenye upande wa kodi na mambo mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kwenda vizuri zaidi lazima mazingira mazuri hasa kwenye sekta binafsi yatengenezwe. Tumeona kwenye mipango ya Serikali namna ambavyo kwenye upande wa nishati leo tuna uhakika wa kuwa na umeme wa kutosha, tuna Bwawa la Mwalimu Nyerere na tunazo megawati za ziada. Je, hizi megawati ambazo tunasema tunazo za ziada huko chini kwa wananchi wetu wanaufurahia huu umeme? Huko chini kwenye viwanda vyetu wanaufurahia huo umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri kwenye upande huu. Lazima tuwekeze nguvu kubwa kwenye usafirishaji wa huu umeme kwa maana miundombinu tuliyokuwa nayo ilikuwa ni ya zamani ambayo sasa imechakaa, pamoja na kwenye usambazaji wa huu umeme. Tukiweza kuwekeza kwenye usafirishaji na usambazaji tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, juzi tarehe 17 Januari, tumeona kwenye usambazaji tumeweza kusaini kwenye vijiji zaidi ya 9,000 na mimi kwa Wilaya yangu ya Chunya tumepata zaidi ya vitongoji 31. Hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ili tuweze kwenda vizuri zaidi tuhakikishe kwamba njia ya usafirishaji inakwenda vizuri. Mathalani leo kwenye Wilaya yangu ya Chunya, tuna umeme umesambaa kwenye vijiji vyote, lakini umeme huu tunaoupata ni mdogo ambao haujitoshelezi na haujitoshelezi kwa sababu miundombinu imeshakuwa ni chakavu ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nishauri namna ya kuweza kukabiliana na hii changamoto. Tuweze kujenga substation ya kutosha pale kwenye Wilaya yetu ya Chunya ili tuwe tuna umeme wa kutosha ambao utaweza kulisha viwanda vyetu, utaweza kulisha kwenye maeneo ya wachimbaji na wao waweze kunufaika na huu umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tu wachimbaji wengi wa kutosha wanashindwa kunufaika na huu umeme, kwa sababu ni mdogo matokeo yake wanatumia majenereta hivyo gharama za uendeshaji zinazidi kwenda juu zaidi. Hivyo nishauri kwenye hili, tukifanya hivyo tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, sisi watu wa Chunya maeneo mengi sana ni wachimbaji, tunapeleka umeme kwenye vitongoji, lakini maeneo ya wachimbaji kasi ya kupeleka umeme ni ndogo sana. Niombe ili mpango huu uweze kwenda vizuri na uwaguse wananchi wengi, twende tuhakikishe tuwe na mpango mahususi wa kupeleka umeme maeneo ya wachimbaji, ili kuweza kwenda kule kuongeza uzalishaji ambapo pamoja na kwamba umeme ni huduma, lakini umeme pia ni biashara. Wataweza kununua kwa gharama, lakini pia tutapunguza uendeshaji kwenye migodi ya wachimbaji wetu wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kwamba tunaenda kuwagusa hawa wachimbaji wetu, tunaona namna ambavyo Sekta ya Madini imezidi kuchechemuka. Leo hii kila mchimbaji wa madini anafurahia hasa kwenye uchimbaji wa madini ya dhahabu namna ambavyo mazingira ya uchimbaji yametengenezwa yamekuwa mazuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mazingira ya uchimbaji kuwa mazuri zaidi, bei ya soko la dunia na soko la ndani kwa mara ya kwanza tumeweza kufikia kwa gramu moja zaidi ya shilingi 400,000. Haijawahi kutokea, lakini kwenye Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan kutokana na sera nzuri na mambo mazuri huko duniani leo tunaona namna ambavyo bei imekuwa nzuri na wachimbaji wetu wananufaika, hivyo tukiwekeza zaidi hapa, tutaweza kupata na kuwapata wachimbaji wakubwa zaidi. Ili tuweze kuwafikia wachimbaji wengi na wakubwa zaidi lazima tuwekeze kwenye utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunaliimba jambo la utafiti kila siku. Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri amekuwa anazungumza kwamba utafiti unafanyika, vifaa vinanunuliwa lakini pamoja na kwamba vifaa vinanunuliwa bado hatujaweza kuwafikia wachimbaji wengi. Tukifanya utafiti wa kina tukaupeleka maeneo hizi taarifa kwa wachimbaji wetu wadogo tutaweza kuongeza uzalishaji wa dhahabu, lakini tutaweza kuwainua wachimbaji wetu kutoka kuwa chini kwenda kuwa wa kati, uchumi wa nchi utaendelea kukua, lakini siyo kukua tu tutaendelea kuwatengeneza mabilionea wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kupitia Sekta ya Madini peke yake kwenye mchango wa pato la Taifa tunachangia zaidi ya 10%; siyo kiasi kidogo na tukiendelea hivi tutazidi zaidi ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, Mheshimiwa Waziri yuko hapa na Naibu Waziri wa Madini yuko hapa; tuendelee kuweka nguvu kubwa sana kwenye Sekta ya Madini. Tukiwekeza nguvu kwenye Sekta ya Madini kwenye utafiti tuna uhakika tutapata fedha nyingi hasa fedha za kigeni na nchi yetu itazidi kwenda mbele na tutaweza kupiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tulikuwa tuna mpango wa kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kupitia Mradi wa MBT (Mining for Brighter Tomorrow). Mradi huu unazungumzwa, lakini utekelezaji wake bado haujaanza mpaka leo. Niombe tuweze kuwatengeneza vijana. Tumeunda Wizara ya Vijana; namna gani tutaweza kuwasaidia hawa kupitia MBT maeneo ya wachimbaji wadogo tutengeneze rush.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu tuna baadhi ya maeneo ambayo tumeyaweka kama hifadhi kuna Hifadhi ya Mbiwe, kuna hifadhi ya kule Gepu kuna watu walitolewa kule. Tuone namna ambavyo kule Gepu tutengeneze tuwapatie leseni hata mbili au tatu kwa wachimbaji wadogo ambao tuwaweke kwenye mpango wa MBT ili wao waweze kuchimba pale. Hivi ndivyo tutakavyoweza kuwasaidia vijana na Wizara yako Mheshimiwa Nanauka itaonekana inafanya kazi vizuri na wananchi wetu wataweza kupiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pia kwenye upande wa Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo kazi kubwa imefanyika na zaidi ya 65% – 70% ya Watanzania tunategemea kilimo kuendesha maisha yetu ya kila siku, lakini na uchumi wetu kwa ujumla. Tumeona Serikali imeweka ruzuku ya kutosha leo wananchi wananufaika wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mbolea hii ambayo leo wananchi wananufaika, kule kwangu tuna wakulima wa mazao ya chakula na wakulima wa zao la tumbaku. Mpaka kwenye zao la tumbaku tumeweza kuweka ruzuku na wananchi hawa wanaweza kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mazao ya chakula, wale mawakala ambao wanapata hii mbolea kwa ruzuku na bei elekezi, wanashindwa kwenda kuifikisha mbolea hii maeneo yote kwa sababu usafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine gharama zinatofautiana. Leo wakala anachukua mbolea anaambiwa atauza mfuko kwa 75,000 kwa Wilaya ya Chunya, kutoka Mbeya mpaka Chunya ni 75,000, lakini kutoka Chunya Mjini mpaka Kambikatoto ni kilometa 240, huwezi kwenda kuuza kwa shilingi 75,000. Kwa hiyo, leo mwananchi huyu tunamuadhibu, kwa sababu ya bei elekezi na yule supplier anashindwa kuifikisha kule kwa bei ile ambayo ilitakiwa iweze kumfikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, Wizara ziko hapa, ziangalie namna ya kuangalia hizi bei kutoka eneo moja hadi lingine ili wananchi wetu hawa waweze kufikiwa bei ikiwa nzuri kwenye ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango huu imeeleza pia, namna ambavyo kwenye kilimo tunaendelea kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tumeona kutoka mwaka 2021/2022 tumetoka kutoka hekta 690,000 na mwaka 2024/2025 tumefika zaidi ya hekta 983,000. Zaidi ya miaka mitatu tumeongeza zaidi ya hekta 300,000 kwenye upande wa umwagiliaji, hii ni hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado tuna maeneo mengi makubwa na mazuri ambayo yanatufaa kwa ajili ya umwagiliaji. Kule kwangu Chunya tuna maeneo makubwa na mazuri. Walishakuja kufanya utafiti, tunaomba fedha zije ili hawa wananchi waweze kunufaika na maeneo ya umwagiliaji haya ili tuweze kuzalisha chakula kingi cha kutosha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)