Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia huu Mpango wa Professor Kitila, ninampongeza sana. Ninamshukuru Waziri wa Fedha, ni mtendaji mzuri, ametuonyesha mambo mengi katika taarifa zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwateua kwa sababu ameona vipaji vyenu vinatumika vizuri kwenye hali hii. Kwa hiyo, tunamshukuru sana kwa kuendelea kuwateua kuwepo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia mpango huu ulivyo na hakuna chochote kitakachozungumzwa katika mpango kama hatutengenezi maisha bora kwa Watanzania. Nianze tu mimi na jimbo langu. Leo nikienda jimboni hata nikihubiri kilimo bora chenye ufanisi watu hawatanisikia. Nikihubiri ufugaji bora wenye ufanisi watu hawatanisikia; kwa nini? Kwa sababu toka mwaka 2021 mpaka leo kila kinachofanyika kwenye Jimbo la Bunda, tembo wanakula. Yaani leo badala ya kuchunga ng’ombe tunachunga makundi ya tembo, kila kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo hata ningehubiria watu kiasi gani, mpango mzuri, mpango nini na uchumi mkubwa wa Jimbo la Bunda ni mazao ya kilimo na mazao ya kibiashara. Tembo anakula yote, anakula mpaka katani, anaangusha na maghala anakula. Sasa wale wa Zanzibar niseme ndovu basi ndiyo tusikie vizuri kwa sababu inawezekana nikisema tembo nisieleweke vizuri. Ndovu wanakula mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa upande wangu, nini kifanyike watu wa Bunda waishi kwenye maisha bora? Ni kuruhusu mpango wa VIP wa Grumeti waweke uzio (fence) kama ilivyowekwa Serengeti, kama ilivyo Botswana na South Africa. Tukiwekewa fence tutaishi. Maana yake ni kwamba leo, jana na hata juzi nilikuwa ninahangaika na watu wa wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii walipe fidia. Kila mwaka ni mamilioni ya hela yanalipwa, siyo kwangu tu na maeneo yote. Sasa, kwa nini kama kuna mpango maalum ambao umefanyiwa utafiti wa kuweka fence kwa nini tusikubali huo mpango? Maana yake sisi hatutumii hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Grumeti Fund wale wa VIP wamekubali kuweka fence ili kuzuia pamoja na ng’ombe kwenda huko, lakini tembo kuja huku. Wameweka Serengeti ikaleta tatizo la Kiserikali. Mimi kwangu hoja kubwa ni kwamba Serikali ikubali kuweka fence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kabla ya fence nini kifanyike? Tunaomba sasa TANAPA, TAWA na TFS waendelee kulinda kwa sababu toka tumeanza kuchukua hizi hela za TANAPA, TAWA na TFS kuzileta Serikalini hali ni mbaya sana. Eti, TANAPA wakusanye hela, wawape TRA halafu TRA wakae huko na Serikali warudishe TANAPA. Hivi tembo anasubiri huo mchakato kweli hapo? Tuwe wawazi, TANAPA na TAWA wanalinda Hifadhi ya Taifa na hifadhi zinazotoa mazao mazuri kwa Tanzania ni tano tu, nyingine 22 hazitoi mazao. Bunge lilishaazimia hapa, tuliazimia, tuwape 51% ya kwao halafu 49% ibaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichopo ni kwamba Serikali imetii Azimio la Bunge, lakini badala yake ni kwamba hela zinaenda Serikalini ndiyo zirudi, aah aah! Kwani sisi si wataalam wa fedha? Kwa nini tusiweke mkataba kwenye benki kwamba shilingi milioni moja ikiingia, shilingi 510,000 itakuwa ya TANAPA, TAWA na TFS na shilingi 490,000 iende Serikalini ili moja kwa moja kila mtu anapata chake, kwa nini tunasubiri kurudishwa? Kwa hiyo, kwangu ninataka haya mambo yafanyike ili watu wangu wapate amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimeona mpango wako, lakini ninajiuliza, hivi Januari, 2027 kutatokea nini? Kama tukio la kwanza kwa Tanzania watoto wa mwaka 2021 darasa la kwanza na watoto wa mwaka 2022 waliokuja kuingia darasa la kwanza, wale wa darasa la sita. Mwaka 2027 Januari, watoto wa darasa la saba na wa darasa la sita wanaingia kwa pamoja; almost 3,000,000 na kitu wanaingia kwa pamoja. Ukigawa hapo tunahitaji karibu madarasa 69,000 na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua wanafunzi walioingia mwaka huu kwa kutolea mfano, 937,000 maana yake madarasa yanayobaki ni mengi. Tumejiandaa vipi kukabiliana na upungufu wa madarasa na shule za sekondari kwenye mpango huo ambao ni sera mpya? Kwa hiyo, hapo napo tuangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, utekelezaji wa miradi…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Taarifa wapi, Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru. Ninataka tu kumpa taarifa kaka yangu kwa mchango wake mzuri. Alionyesha kuwa bitter kwamba TANAPA na Ngorongoro wakikusanya fedha zinaenda. Ninampa taarifa tu kwamba, Bunge la Kumi na Mbili tulifanya marekebisho, sasa hivi TANAPA…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere, kaa chini wakati unapokea taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakusanya na kuchukua through retention. Kwa hiyo siyo kwamba fedha zote zinaenda, wanakusanya na kutumia. Kwa hiyo, kama kuna kero zozote zile za tembo na nini wao watu wana fedha wanaweza wakawa wanalipa on time. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unapokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa si dada utaikataaje hata kama iko vibaya sawa tu, naipokea tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, utekelezaji wa miradi…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere kuna taarifa ya pili kutoka kwa Mheshimiwa Profesa Shemdoe

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la darasa la sita na la saba kukutana mwaka 2028 Januari, sisi kama Wizara tumeshatoa maelekezo kwenye bajeti ambayo italetwa kwenye Bunge lako. Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wahakikishe kwenye mafungu yao wanaweka ujenzi wa madarasa ambayo yatatusaidia ku-accommodate wale wanafunzi mwaka 2028. Ninashukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unaipokea hiyo taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa ya Profesa, lakini sina hakika kama mkoa na halmashauri zinaweza kuwa na fedha za kujenga haya madarasa. Sasa kama zinashindwa kulipa 10% ya wanawake ndiyo zitajenga madarasa? Ninadhani tujiandae upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kazi ya kumaliza viporo, niombe Serikali iwe kali kidogo, hamna kitu kinanichukiza kama mradi umepewa fedha halafu haukamiliki na mbaya zaidi sasa akienda Waziri kwenye halmashauri fulani au kwenye mkoa anakutana na mkuu wa mkoa anakutana na mkuu wa wilaya. Wanaenda kwenye Kituo cha Afya Unyari, tumepelekewa milioni 500, hakina jengo la upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anaona kabisa hapa kuna tatizo anaanza kuna nini, kuna nini, utasikia sasa minong’ono. mkuu wa mkoa anasema mkuu niachie, mkuu wa wilaya anasema mkuu niachie. Hivi wakuachie ulikuwa wapi? Yaani miaka mitano mradi umekufa wewe waziri anaenda niachie, niachie, tutaachiwa mpaka lini? Ninaomba Mawaziri, sehemu hii ninaona wamekuja kivingine, ninawashukuru sana Mungu awasaidie waendelee kubadilika hivyo hivyo.? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kuachiwa, kama wewe ulikuwepo mradi umeharibika, chukua action hapo hapo. Hii Tanzania tumebaki na maneno mengi mno, kusameheana ni kwingi mno, hakuna hiyo. Sasa hivi ni kupambana na tumeambiwa huko Ulaya, wenzetu walikuwa wanatufadhili fedha hapa nimeona Waziri wa Fedha amesema hapa bilioni 39 haziji, kipindi hiki lazima tuangaliane na hata yale makongamano sijui mihadhara sijui nini ipunguzwe. Sasa leo kila siku Mkuu wa Wilaya yuko Dodoma, Mkurugenzi yuko Dodoma, Mkuu wa Mkoa yuko Dodoma. Wanatumia hela zipi au ni hizi ambazo wananchi wanakusanya kwa viazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiwe online meeting, kwa nini tusifanye hivyo. Lazima tujibane kipindi hiki, Tanzania ionekane kwamba tunafanya kazi ya maana. Kwa hiyo niombe, kwenye Mradi wa Kituo cha Afya Unyali, kwenye Mradi wa Sekondari ya Tirina, kwenye Mradi wa Sekondari ya Sanzati, kwenye Mradi wa Kituo cha Afya Mihingo Bunda, ile miradi ambayo inakuwepo inakuwepo, tukamalize hiyo miradi ambayo inakuwepo na Barabara ya Sanzati inakwenda Nata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, nimeuliza swali siku moja hapa la barabara, Spika aliyekuwepo akaniambia muone, Waziri hapa na Naibu Waziri wamalize. Nikaenda kwa Waziri wa Fedha tukaongea, akasema kwamba miezi hii miwili tutapewa bilioni mbili kwa hiyo barabara, mpaka leo. Hivi sasa kwa nini sisi Wabunge tukisema jambo haliheshimiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambie Wabunge nchi hii tunajenga sisi, Watanzania wametuamini sisi, tukiendelea na hayo mauoga mauoga hapa, tutashindwa kufanya miradi ya wananchi, pale ambapo mama ametoa hela zake zimekwenda kwenye site, tusimamie kikamilifu. Sasa tukijifanya waungwana na kila mwaka tunakuja nusu nusu inasaidia nini sasa. Tunajifanya watakatifu, tukirudi humu tuko 30%, inasaidia nini. Tupambane hela zilizoko huko zifanye kazi. Ninakushukuru. (Makofi)