Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Mhe. Dickson Nathan Lutevele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Mpango huu wa 2026 - 2050. Kwanza kabisa ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wetu Profesa kwa kutusomea Mpango ambao kimsingi tuliuelewa umechanganua mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nijikite kwenye eneo moja muhimu ambalo pengine linaweza likawa lina mchango mkubwa sana kwa Taifa letu kwenye Mpango huu ikiwa litafanyika kwa vitendo. Katika usomaji Mpango wa Mheshimiwa Waziri yapo maeneo ambayo yanawiana kabisa na Hotuba ya Mheshimiwa Rais. Eneo hilo mojawapo ni namna tutakavyoliendeleza Taifa letu kutoka kwenye uchumi tulionao hivi sasa kwenda kwenye uchumi wa kati na baadaye uchumi mkubwa zaidi. Katika kufanya hivyo tunajielekeza katika kujenga kongani za viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hilo ukisoma taarifa maeneo ya kongani za viwanda yameainishwa mle, lakini kwenye Mpango inasema tunafikiria kujenga katika kila wilaya. Sasa ninaomba nishauri kwamba mpango huu wa kongani za viwanda usiwe mpango wa maeneo fulani, halafu mawazo yakawa kwamba tunafikiria au tutafikiria kuweka katika kila wilaya. Kwa kuwa huu ni mpango ningeomba tujielekeze katika kuweka kongani za viwanda kwenye kila eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuweke kwenye kila eneo? Hapa kwenye viwanda kuna eneo pana sana ambalo limeajiri watu ambao hata sasa wanafanya kazi kubwa na pengine hatujawafikia. Kwa mfano, katika nchi yetu hata sasa hivi ukitoka hapo nje unakuta kila baada ya mtaa kuna gereji vijana wanatengeneza magari, vijana wako wanafanya kazi za kuchonga (mafundi seremala) wamo humo, lakini hawa vijana hatujawakusanya sehemu moja na kwa kufanya hivi tunaathiri mambo makubwa mawili. Kwanza, miji yetu inakuwa haina mpangilio mzuri, lakini jambo la pili tunashindwa kukusanya mapato kwa sababu hawa vijana hatujawaweka sehemu moja na hatujawawekea Mpango mzuri unaotufanya turudi kuangalia maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wasiwasi wangu ni nini, ukisoma taarifa ya CAG kwenye Mpango wa BBT inaonesha kabisa kwamba mpango huu ulikuwa umelenga kuajiri vijana 9,724 ulianza na vijana hao, lakini mpaka 2024 kwenye taarifa ya CAG ya 2024 inasema vijana waliokuwa wamebakia walikuwa ni vijana 514 tu. Maana yake mpango huu umefeli. Kwenye conclusion anasema Wizara ya Kilimo na Wizara ya Umwagiliaji walifeli kwenye mpango huu. Pia, Mpango huu ulikuwa unasema tunakwenda mbele kwa miaka nane target yake, lakini ndani ya miaka miwili tayari inaonesha Mpango ulikuwa umefeli kwa sababu vijana 900 na, kwa mwaka mmoja wakashuka mpaka vijana 500 na, hawa vijana 400 na kitu wamekwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba mpango huu ulikuwa umefeli na sehemu gani ninaweza kusema ulifeli? Kwenye Mpango wa BBT yalikuwa yameainishwa maeneo ambayo mpango huo unatekelezwa. Wewe unamtoa kijana Mbinga unamleta atekeleze Mpango wa BBT Dodoma, hata mazingira tu yanakataa. Namna ya ufanyaji kazi wa watu wa huku na watu wa kule hayashabihiani, lakini tukiweka kongani za viwanda tutakuwa na faida zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, maeneo mengi katika nchi yetu watu watajiajiri. Leo hii tunajenga vyuo vya VETA katika kila wilaya lakini je, tumeshajiuliza hawa vijana tunaowajengea VETA, hawa watu wanaoingia VETA baada ya kutoka hapo watafanya kazi wapi? Tunasema kwamba mtu akisoma VETA atajiajiri. Kujiajiri siyo jambo la kufikirika ni jambo linalotaka mtaji. Kujiajiri siyo jambo la kuamka asubuhi ukasema ninajiajiri ni jambo linalotaka mwendelezo. Hivyo basi, ninaomba kushauri Wizara pamoja na taasisi zinazohusika kwenye haya mambo kwanza kabisa Mpango huu uwe ni wa kila wilaya ili tuwafikie watu wote kwenye nchi nzima? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, twende tukajifunze kwa Mataifa yaliyofanikiwa. Nilikuwa ninasoma taarifa ya namna wenzetu walivyofanikiwa, kwa mfano China, 12% ya pato la Taifa la China wanategemea viwanda vidogovidogo ambapo viwanda vidogovidogo vimeajiri takribani watu milioni 60. Idadi ya Watanzania wote imeajiriwa kwenye sekta moja tu Nchini China. Sasa twende maeneo hayo tujifunze. Twende India tujifunze kwa wenzetu waliofanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo mamlaka kwa mfano TanTrade; jana mchangiaji mmoja alisema tuwe tunafanya check and balance tukipanga mpango hata kama wa mwaka mmoja, jamani tuliwakabidhi hiki mmefika wapi? TanTrade atuambie kwa mwaka amepeleka vijana wangapi kupata exposure? Ukifuatilia unakuta wanaokwenda huwa ni wale wale, ni wale wale, ni wale wale, vijana walioko kijijini hawana exposure. Nguvu wanayo, uwezo wa kufanya kazi wanao, lakini kwa sababu tunakwenda taratibu hawana exposure. TanTrade chukua vijana 100 peleka China wakajifunze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano, niliomba kwa TanTrade mara nyingi sana kwenda nikaangalie tu masuala ya machines, lakini nikakosa private sector ikanipeleka Dubai WoodShow. Wakati niko WoodShow nimekutana na masoko ya India, China na maeneo mengine niliporudi nimewapa Watanzania wenzangu masoko na wamefanya export. Kwa nini tusifanye haya? Kwa nini tusiwapeleke wale wanaolengwa na Serikali? Badala yake tunapeleka watu wale wale waliofanikiwa wenye viwanda vikubwa, tufikiri kuhusu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunafikiria Mpango wa Miaka 50 na kikubwa tunazungumzia viwanda. Tunapozungumzia hivyo viwanda, tuna viwanda ambavyo mpaka sasa vimeajiri watu wengi sana na havifanyi vizuri. Kwenye mpango havijaelezewa. Angalia Viwanda vya Chai kule Lupembe, angalia viwanda vya chai kule Mufindi. Angalia Viwanda vya Kahawa, kwenye Mpango huu tunasema tuna mpango gani wa kuhakikisha viwanda vile vinaendelea kufanya kazi. Kwa sababu katika viwanda vile wako babu zetu walitoa mashamba kwa ajili ya chai; walitoa mashamba kwa ajili ya kahawa; na walitoa mashamba kwa ajili ya Mikonge. Tunakuja na mpango gani wa kuhakikisha viwanda vile vinaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninaomba sana sana nisisitize kwamba katika mpango huu twende kwanza field twende tukawaone vijana. Sasa hivi Serikali imejenga shule kila eneo, imejenga sekondari kila eneo na vijana wanafaulu, lakini wapo ambao hawafaulu kwa syllabus na wale vijana wakiingia kwenye ufundi kwenye magereji mafundi wa umeme mafundi wa magari wanafanya vizuri sana kwa sababu ubongo wao bado uko mbichi. Wale vijana kwenye Mpango huu tunawazungumziaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoangalia tutajikuta tunakwenda na Taifa la wasomi watupu, lakini kuna kundi kubwa nyuma tunaliacha na kundi hilo ndilo linalozalisha. Kwa hiyo, kwenye Mpango usijilengeshe pekee yake kwa waliosoma, tuangalie na wale wanaofeli kwa sababu ni Watanzania na wanashiriki kwenye kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kushukuru sana. (Makofi)