Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia mpango wa maendeleo wa nchi yetu. Ninampongeza Rais, kulikuwa na malalamiko namna ya kupanga mipango yetu, ameshaunda Wizara na amempa Profesa Kitila Alexander Mkumbo na Naibu wake pia ameweka Waziri wa Fedha, Balozi mzoefu kwa muda mrefu, pamoja na Watendaji wa Wizara tunawatakia kila la kheri katika kazi hii kubwa ambayo wamepewa ambayo kwa kweli inahitaji kila mtu ashiriki katika mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu haijawahi kuwa na upungufu wa mipango, ninachomwambia Profesa Kitila Mkumbo yeye ni Profesa, ni mtafiti na Maprofesa wengine waliomo humu na Madaktari na wasomi mbalimbali kuwa, nchi hii haina upungufu wa mipango, shida tuliyonayo ni namna ya kutekeleza mipango tuliyonayo. Ningeshauri Waheshimiwa Wabunge tujielekeze katika maeneo hayo, ukirudi nyuma mipango iliyopangwa katika nchi hii ma-shelf huko yamejaa, sasa Bunge hili Rais mwenyewe ana utashi amelileta jambo hili, ameshaunda Wizara, amewapa watu nafasi, tuwasaidia kuwashauri namna ya kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza vilevile Mheshimiwa Rais kwamba mipango ile ambayo ilikuwa kizungumkuti kwa muda mrefu, Liganga na Mchuchuma, gesi, SGR na vitu vingine vingi na viwanja mbalimbali vya ndege ameshatekeleza na vingine vimeanza kufanya kazi. Tunampongeza kwa jambo hilo kubwa sana kwa kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine niwaambie Watanzania na Wabunge tunapokuwa tunampongeza Rais sisi wengine wanasayansi ni lazima uwe na facts, ukiangalia mambo yaliyofanyika, hivi kwa mfano, wenzangu walipata Ubunge, mimi niliutafuta. Nilikatwakatwa huko kote na viongozi wangu wa Wilaya hawanitaki hata bure, Mwenyekiti wa Mkoa na Kamati ya Siasa na Kamati Kuu wakaniteua, nikarudi nikashinda kura za maoni. Nikarudi tena wakanikata tena kule yale majamaa, nimekuja Mkoa na Mama Samia amenirudisha, hivi wanataka nisimpongeze kweli? Haiwezekani! Ukinizuia nisimpongeze Rais utakuwa hunitendei haki, halafu usisahau kwamba nilikuwa Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, Rais akiwa Makamu wa Rais amenituma kazi, kwa hiyo ninamjua vizuri kwa utendaji wake wa kazi na uthubutu. Yapo mambo mazito Mama ameamua ameyafanya hapa, kabisa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo haya ambayo vilikuwa ni viporo vya muda mrefu aliwaambia kazi itaendelea na imeendelea. Hivi sasa tuchambue mambo haya namna ya kuzungumza, kama kuna ukweli tuuseme na ukweli utatuweka huru, kama kuna mahali tukosoe na watu wapokee hivyo, twende na Taifa la namna hiyo. Pia msisahau kwamba mimi ni Mjukuu wa Baba wa Taifa, kwa hiyo hilo ni muhimu sana kuliweka. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitila Mkumbo amesema atawezesha makandarasi wa ndani, hili ni donda ndugu. Pale kutoka Mjini Tarime mpaka Mogabiri, nimewaambia wakakwangue ile inayoitwa lami ubaki udongo watu wajue hakuna lami, kuna udongo pale. Barabara ya kutoka Mogabiri - Nyamwaga - Nyamongo ni kizungumkuti, miaka saba kilomita 25 anadai mpaka leo bilioni 4.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale Musoma kwa Profesa Muhongo, Makojo – Busekela, ukizungumza habari ya mpango watakuambia barabara. Ukienda Busigwe - Kitaramo - Butiama kama hukutaja barabara hii na fedha ulipe mkandarasi, utaimba hawatakupigia makofi. Ukienda Tarime Mjini nimetaja Mogabiri mpaka kule Tarime Mjini, mkandarasi yupo mpaka mabati yamedondoka, hawatakuelewa na mpango wanataka barabara ilimwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mwibara, Busambara Mugara wanataka barabara ilimwe. Ukienda Rorya – Utege - Shirati, Chege hawezi kukuelewa bila kuzungumza habari hii. Kwa hiyo Profesa ametaja, nimwambie sasa mwezi wa 11 ukija hapa, pamoja na Mawaziri wengine watueleze hao makandarasi ambao wanadai fedha na miradi ambayo wameshasaini wanalipaje kabla ya kuweka miradi mingine mipya, asiweke kiporo juu ya kiporo, tuambie hizi barabara zingine na miradi mingine ya maji wanaweka mpango gani wa kulipa ndiyo ulete mipango mingine hapa mipya ya kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu tuwekeze kwenye elimu ya amali. Iwe shule ya msingi akimaliza darasa la saba ana jambo la kufanya, iwe sekondari ana jambo la kufanya, iwe ngazi yoyote ya chuo ana jambo la kufanya, tufanye kama Wachina. Mchina ukimwita aje kufanya kazi ya umeme, akiona shughuli imeisha anakuwa fundi bomba, hujakaa sawa anakuwa fundi cherehani. Tufanye namna hiyo ili tusaidie vinginevyo tutakuwa tunapata lawama kila siku, kwa sababu hatuwezi kuajiri vijana wote, lakini tuna vyuo, kwa hiyo, tuwekeze maana yake twende kwenye teknolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetajwa habari ya ajira, nikawa ninajiuliza pamoja na Wizara ya mdogo wangu pale wa vijana. Kwanza juzi wamewaajiri watu hapa, ukiangalia Wabunge walivyokaa humu Bungeni, kila Mkoa una wawakilishi vijana, akinamama na majimbo, kila Mkoa hapa umewakilishwa, tunataka ajira nchi hii iwe na msawazo huu. Wakitoa ajira tuone watu wetu wamepata ajira, wafanye kazi hiyo, ukipitia watu walioajiriwa pale ni kama hatumo maeneo fulani fulani hivi wanasababisha watu kuanza kujadili huyu kapataje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, alete mpango, wanawezaje kutangaza ajira 10,000, twende kwenye uwakilishi wa Majimbo, Mikoa na makabila yote yapo humu ndani, tuombe hilo walifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amefanya uthubutu mkubwa, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, ameshaelekeza walete sheria ya namna ya kupata Watendaji Wakuu wa Taasisi na haya Mashirika ya Umma na kupata Wajumbe wa Bodi, wameleta mapendekezo Kamati ya Bajeti kwamba hata Wakurugenzi kama wanatangaza ajira Mtendaji wa Kata nafasi mbili, wanatangaza watu wanaenda 200 mpaka 500. Kwa nini hizi Halmashauri wasitangaze, 180 ni nyingi sana. Kwa hiyo Wakurugenzi wale wafanye vetting, wapewe vigezo, wapewe kazi, hata Makatibu Tawala wale (DAS) mpaka (RAS), hizi ni taasisi kuna miradi mikubwa ya kiuchumi, kuna viwanda pale, hawa watu wapewe malengo wafanye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watenganishe siasa na utumishi wa umma ili twende mbele Profesa anafahamu ninachokizungumza. Walifanya hivyo London - England tangu miaka ya 1940, walifanya hivyo Singapore twende kuweka watu kwa vigezo, kwa uwezo, tusiweke mtu kwa sababu ni ndugu yake na Waitara, tulisoma darasa moja, tupimane na wakifanya hivyo hawa vijana ambao wanalalamika wazee kupata uteuzi, hawatalalamika kwa sababu wameweka mambo wazi, wameenda kwenye ushindani na mtu amekosa nafasi kwa vigezo, hawezi kulaumu. Yule ambaye amepata nafasi tunavyo vigezo kwamba baada ya miezi sita ama mwaka mzima hujafanya kazi ambayo tumeitarajia utaondoka atakuja mtu mwingine, watafanya kazi kwa ushindani na kazi itakuwa nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa hapa tusiongee jambo la utawala bora kwa kujifichaficha, tuongee jambo la utawala bora hadharani na kuna vigezo, watu wameenda shule kuona nini maana ya utawala bora, kwa hiyo tukitaja mambo haya tutaje kwa upana wake na watu wajue tunataka utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hapa, Profesa amesema kutakuwa na uwazi, kutakuwa na uwajibikaji, hili jambo ni kubwa, kuna utawala wa kisheria, mambo ya demokrasia na vitu vingine. Ushauri wangu hapa ninataka niseme, mpango huu ukiangalia mawazo yaliyokuja ni makubwa yanahitaji kila Waziri aje hapa atuambie yeye anakwama wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ambaye Bunge linatakiwa limhoji limwajibishe atoe majibu sahihi hawezi kuja kuninong’oneza mimi, inatakiwa ikiwezekana Serikali ifanye kazi yake, Bunge lifanye kazi yake, ndiyo utaratibu wa Bunge hili. Kwa hiyo, lazima Wabunge tuzungumze na Mawaziri wa upande wa Serikali, kila mtu afanye kazi iende vizuri, ndiyo mambo ya utawala bora. Tukitaka hoja imekuja hapa iandaliwe vizuri tupate majibu, Mama Samia amejipanga vizuri, ukimsikiliza, mawazo yake, maamuzi yake, viongozi wangeelewa Rais anachokitaka, anataka matokeo, hizi changamoto ziishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi Mbunge kipindi cha tatu humu, nilikuwa ninaangalia hapa kwenye Kanuni za Bunge Kanuni ya 57, 58, 61 - Haki na Madaraka ya Bunge. Nikaangalia mwongozo nikikosea hapa nitaenda kwenye Kamati ya Maadili, ukisoma Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, nikasoma Ibara ya 100 humu. Sasa kama leo nitazungumza humu Mbunge ninatakiwa nimhoji Waziri, halafu nikimaliza ninaambiwa nitaenda kuhojiwa sehemu nyingine ninataka niseme kwa mazingira ambayo Bunge letu tumeingia, kwa changamoto tulizopata kwa wananchi wetu, watu wa Tarime Vijijini, wapigakura wangu wanamjua Waitara yukoje, hakuna Waitara wa Jumapili wala Jumatatu wala Jumanne, Waitara ni mmoja siku zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Bunge hili na Wabunge wameangalia sura za watu waliopo humu ndani, tulikuwa wengi, tupo sasa 30%. Wenzetu wamekuja, kikulacho kinguoni mwako. Kila mtu afanye kazi ya wananchi kwenye Bunge hili na Serikali iende ijipange vizuri, wakiwasilisha hoja wafanye kama anavyofanya Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo! Mbona Waziri Kitila watu hawalalamiki? Analeta hoja za kitaalam ameenda amejifungia, sasa mpango huu tungetamani, watu wanasema ni Mpango wa Maji, Maji, Maji, Waziri kijana Aweso aje atuambie yeye anakwama wapi katika Wizara yake tumsaidie kama ni kubadilisha sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa kilimo aje atuambie malalamiko ya wafugaji na wakulima kila mwaka tunazungumza hapa, watu wanauana, leo hii unaleta mpango wa Serikali tuoneshe namna ambavyo wakulima watalima kwa mpango, namna ambavyo wafugaji watafuga kwa mpango na bila ugomvi kuwe na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge wa Tarime vijijini nina shida ninapiga hapa mwaka huu ni awamu ya pili kwa Jimbo la Tarime Vijijini, Jimbo la Ukonga ilikuwa awamu ya kwanza, ninazungumza malalamiko ya Hifadhi ya Serengeti kuhusu habari ya mipaka tu! Ng’ombe wanatekwa, watu wanapotea pale. Ndugu zangu! hapa ninapozungumza Karakatonga kuna watu watano hawapo. Sasa ukiniambia mambo mengine!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda Bunge lifanye kazi yake, Serikali ifanye kazi yake na Mahakama ifanye kazi yake, kama ambavyo tukienda Mahakamani tunanyenyekea na Serikali wakija hapa tuzungumze kama Mhimili, tufanye kazi ya wananchi. Rais atalindwa kwa wivu mkubwa, yeye ameshamaliza kazi yake kama kuna mtu amepata fursa ya kumsaidia na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba tunajua anaweza kazi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninasoma watu wa Singapore walifanikiwa kwa namna gani, ni meritocracy, tufanye kazi kwa uwezo wa mtu, tufanye proper placement kwenye maeneo, tufanye kazi ya mapinduzi, huu mpango huu ukiusoma vizuri ni mpango wa kimapinduzi. Hatuwezi kujadili mzaha mzaha hapa, hatuwezi kupiga piga makofi, tumuunge mkono Rais, tutunge sheria za kufunga watu, ukienda ukaiba tukwambie umeiba, you are in for it, ukidanganya tukwambie umedanganya you are in for it, tusilete blaa blaa, hili Bunge Watanzania wanatutegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ahsante kwa hayo. (Makofi)