Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata hii nafasi, pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai na kunijalia siku ya leo kusimama katika Bunge hili Tukufu kuweza kuandika mipango au kutoa ushauri na maoni juu ya uandikaji wa mipango ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge aliyesimama hapa, wengi miongoni mwao walikuwa wanaonesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mipango hii au mpango huu, mwisho amesimama Mheshimiwa Waitara naye pia ameonesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mpango huu. Kamati ilishauri na mimi ninaongezea kushauri, kwa nini tusiweke sheria ya kutekeleza huu mpango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunapopitisha bajeti tunakuwa tuna The Appropriation Act na tunakuja tunaihoji Serikali juu ya utekelezaji, tunakuja hapa baada ya miezi sita kwa mujibu wa sheria ya bajeti tunakuja kufanya, kama kunafanyika mid-review basi Serikali inatupa habari kwamba kitu gani kimefanyika. Kwa hiyo, ninaunga mkono kwanza wazo hilo la Kamati, lakini ninatia mkono zaidi kwamba huu mpango basi tugeuze iwe sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie katika ugharamiaji wa mpango, katika ugharamiaji huo tumesema kwamba sekta binafsi itachangia 70%, nilitamani zaidi Wabunge tungejadili huko kwenye hizo 70%, niseme tu Serikali wajiandae kuwa na vivutio vizuri kwa sekta binafsi za ndani na nje ili mpango huu utekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri huo tu sitaki kwenda mbali katika hizi 70%, sekta ya umma ambapo Serikali yenyewe itagharamia mpango huu kwa 22%, lakini ugharamiaji mzima wa mpango ni sawasawa na dola trilioni 3.6 approximately. Sasa nitachangia juu ya uchangiaji wa Serikali katika mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu Waziri amesema kuwa Tanzania kupitia Benki Kuu tutaendelea kununua dhahabu, sasa nami hapa hapa katika kugharamia mpango huu tunaweza kupitia hii kwenye kugharamia dhahabu tukapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu huwa tunaitumia kuweka reserve (federal reserve) ya nchi, kwa hiyo inatusaidia sometimes percentages tunayoamua kuiweka inatusaidia kuingiza katika reserve kwa sababu Serikali yetu au Benki Kuu huwa inafanya portfolio ambayo wenyewe wanaita strategic reserve allocation. Inawezekana wakaweka katika Dola asilimia fulani, katika Euro asilimia fulani, katika Yuan asilimia fulani na katika dhahabu tumeweka asilimia fulani. Tumeanza kuweka kwenye dhahabu ambayo ndiyo ninaizungumzia asilimia tano, lakini tukawa tunaendelea tunaanza kuweka 10% na huenda tukazidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoweka vizuri tukizidi kwenye reserve, yale matumizi yetu ya miezi minne ambayo sasa hivi tuna miezi 4.9 tunapata kuwa na special drawing rise kubwa ambayo supplementary au ziada ya kile kilichowekwa tunapata kukopa kitu ambacho kinaitwa concessional loans. Mikopo ambayo pengine unaweza ukaipata hata chini ya asilimia moja hiyo ni financing ya kwanza, ni kwa sababu tumeweka dhahabu, hiyo ni financing ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Financing ya pili, tunaweza tukaweka hiyo dhahabu ambayo ziada yake dhahabu hiyo ambayo tukiisha kuweka tunaweza ikiwa nyingi, tunaweza tu tukasema kwamba tuweke dhamana tukapata fedha kwa kuweka ile dhamana, fedha zile zinaweza zikaja kwenye miradi na huu utaratibu siyo wa kigeni, siyo mgeni duniani utaratibu huu, utaratibu huu upo na uko katika mfumo wa international bullion system.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaojua waangalie wataona, sasa tukiweka dhamana dhahabu zetu katika kiwango ambacho kinakubalika tutapata fedha. Jambo la tatu, tunaweza tukaweka dhahabu nyingi na kiwango kile ambacho kitakachozidi tunao uwezo wa kuziuza dhahabu zile, au tunao uwezo wa kuweka dhamana tukanunua bond ya Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bond ya Marekani sasa hivi ya miaka miwili, sasa imefikia asilimia 3.5. Asilimia 3.5 ni kiwango kikubwa wakati fedha zako ziko palepale zitakuja kutekeleza hii miradi. Pia katika kuweka dhamana wanaku-charge asilimia mbili, utakapokuwa-charged asilimia mbili kwa dhamana ina maana ukipata 3.5, 1.5 ni faida na fedha zako ziko palepale, lakini umepata faida. Kwa hiyo, kila tukiweka dhahabu kwa wingi tunapata faida zaidi pia kiwango cha dhahabu kinachozidi tunaweza hata tukauza halafu tukanunua tena, si tunayo wenyewe hii? Kwa kuwa, tunayo wenyewe leo kitu chako kikikusaidia inakuwa nongwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze ndugu zangu, kuna mtu mmoja kule kwetu, jina lake anaitwa Mbu, Baba yake anaitwa Mbu na Babu yake Mbu, kiufupi ukimtaja majina yake yote anaitwa Mbu Mbu Mbu, alijaribu kujadili mambo haya! Huyo Mbu Mbu Mbu alitaka kujaribu mambo haya, kwa hiyo hawezi kuelewa. Huu utaratibu upo duniani unatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika ushauri wangu katika sehemu nyingine, ushauri wa Kamati page namba 13 walisema kwamba Serikali iimarishe matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi; lakini wakaeleza kwamba TRA aliomba bilioni 480 kwa ajili ya kuimarisha mifumo. TRA amepewa bilioni 120 ambayo ni sawa 25% kwa ajili ya kuimarisha mifumo. Ina maana hii mifumo inayotumika imeboreshwa kwa 25% bado kwa 75%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kwamba hebu watoe na hizo shilingi bilioni 360 ili tupate mfumo kamili; kwa sababu kati ya mifumo ilipoimarishwa mfumo mmoja ulioimarishwa ulikuwa huu ni wa IDRAS ambao unashughulikia mapato ya ndani. Mfumo huu umerekebishwa kwa 25% bado ziko modules ambazo zinatakiwa ziingizwe katika mfumo huu ili uweze kufanya kazi kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipotumia fedha hizo 25% pia walirekebisha mfumo ya TANCIS, lakini bado ziko modules zinahitajika ndani ya mfumo huu ili mfumo huu uweze kwenda sawa; na kwa sababu inashindikana hata kufanya comparability, kwa sababu Mfumo wa TANCIS tunatumia kwa East Africa. Sisi hatuwezi kuona ule ulinganifu kama wanavyofanya watu wetu wengine. Huwezi kujua kama umepigwa au umepiga wewe. Tukiuboresha mfumo huu unaweza ukaja ukatufanyia mambo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna mfumo hapa unaitwa ETS (Electronic Tax Stamps) ambao ulikuwa vender wake ni SICPA. Mfumo huu ilikuwa tayari uwe umekwishakabidhiwa Serikalini. Mwaka 2017 wakati mfumo huu anapewa SCPA ilikuwa a-run kwa muda wa miaka mitatu arithishe elimu kwa watu wetu ili uweze kufanya kazi. Sasa hivi bado tunahangaika na kumlipa vender, bado mfumo huu sisi hatujauchukua tunaanzisha na mifumo mingine. Kwa nini mfumo huu usije huku? Ambapo serving yake tutatekelezea miradi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe tunakosa mapato kutokana na maeneo tofauti katika nchi katika mipaka. Upande wa nchi jirani wanazo scanners, lakini ukija kwa upande wetu hakuna scanners. Watu wamefanya research wamepita Horohoro hakuna scanners, wamepita Holili hakuna scanner, Tunduma ipo lakini foleni kubwa. Kwa hiyo, inahitajika scanner ziwe nyingi. Pia Namanga kulikuwa bado hakuna scanner na kama itakuwa imechukuliwa ni ndani ya wiki mbili hizi. Niiombe Serikali iangalie utaratibu wa kukusanya mapato. Tukiweka scanners ina maana kwamba mapato yetu hayataweza kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tupime ardhi. Tunayo ardhi nzuri sana. Tutakapopima na kutoa hati tutapokea pango la ardhi. Makisio yanasema tuna uwezo wa kupata trilioni mbili kwa mwaka kwa sababu ya kodi ya ardhi tu. Sasa kwa nini hili Serikali hatuingii tukafanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ardhi peke yake; tumetoa mfano, Mji wa Mtumba ule pale. Ninauchukulia ule ni mji wa mfano. Kila kitu chake kimepimwa. Barabara ziko pale. Kila kitu kiko pale majengo yamekaa ukipita unaona raha. Hivyo katika mpango wetu huu wa miaka 25 kutoka 2025 mpaka 2050 tutakaa kwenye makazi hayahaya Mbagala na kwingine huko? Tutakuwa hivi hivi? Ninaomba Mheshimiwa Waziri atuelezee na mpango wa makazi. Tupime ardhi lakini na mpango wa makazi uwepo. Kama hatutakuwa na mpango wa makazi kwamba hii itakuwa siyo nchi inayokua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilizungumzie, tunakua kwa kasi kiteknolojia na kila sekta imetajwa huku inatakiwa ikue; na kwa kuwa kila sekta inatakiwa ikue ina maana tunahitaji elimu ya ufundi. Tunahitaji kuwa na skills ili tuwe na kilimo kizuri. Kila mmoja aliyelalamika hapa kuhusiana na mbegu zile ni skills. Watu waliolalamika hapa kutokana na viwanda, tunakosa skills. Tumesema kwamba foreign direct investment itakuwa 57%. Watakuja watu wa nje lakini je; raw materials tutakuwa nayo, sawa; lakini watakaoajiriwa pale ni akina nani? Kama wasipoajiriwa watu wenye skills ina maana kwamba tutapoteza na huu uchumi wetu pato lile tutaingia wasiwasi kulipata. Ninazungumzia kwenye skills, mfano China watu wanafuata skills, raw materials zipo, ukitaka za viwanda zipo, ukitaka za kilimo zipo, lakini wanafuata skills. Skills zinazopatikana pale ndiyo maana wanakuwa wako competitive katika dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechukua muda wako mwingi unisamehe, lakini huu ni ushauri. Huu mpango unawezekana kabisa kutekelezeka na unatekelezeka, GDP iliyokusudiwa inapatikana, per capita inapatikana. Ikiwa tutawekeza kwenye ujuzi tuwekeze mapema maana ni wa miaka 25. Kwa hiyo, tusije kuwekeza mwaka wa mwisho. Tuwekeze mwanzo; tukiwekeza mwanzo productivity itakuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)