Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana. Leo nimesimama hapa kuwasilisha sauti za vijana wote wa Kitanzania, vijana wanaotaka mabadiliko ya kweli. Hatma ya Taifa hili iko mikononi mwetu sisi vijana, na hii ni kwa sababu zaidi ya 76% ya nguvu kazi ya Taifa hili ni vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninukuu kauli ya Nelson Mandela ambaye aliwahi kusema, "The development of any nation cannot prosper if the generation of young people is left behind." Maendeleo ya nchi yoyote hayawezi kupiga hatua kama kundi kubwa la vijana litaachwa nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza, kwa mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa vijana wa Taifa hili na kwa kuona umuhimu kwenye historia ya nchi hii kwa mara ya kwanza kuanzisha Wizara mahususi inayohusu maendeleo ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameenda mbali zaidi kwa kutoa fedha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kwa niaba ya vijana wenzangu, tunataka kumhakikishia kwamba, sisi vijana hatutamwangusha. Tunatambua kwamba tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa tunalinda amani na utulivu wa Taifa letu ili nchi yetu iweze kupiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini, kama ambavyo nchi yetu imerithishwa hivi leo ikiwa kwenye mikono salama, sisi vijana tuna wajibu wa kuhakikisha tunaendeleza amani na utulivu wa Taifa hili ili nchi hii iendelee kubaki kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninampongeza sana Waziri wetu wa vijana Mheshimiwa Joel Nanauka, pamoja na menejimenti nzima ya Wizara, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya, na kwa ubunifu mkubwa ambao wameuonesha ndani ya muda mfupi tangu wamekabidhiwa jukumu hili na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi vijana tumeona uanzishwaji wa Vijana Platform, platform ambayo yeye binafsi, Mheshimiwa Waziri amezunguka mkoa kwa mkoa kwenda kusikiliza na kutatua kero za vijana. Pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza kwa kuanzisha vijana call centre, mfumo ambao unatoa uhuru wa vijana kuwasiliana moja kwa moja na watendaji wa Wizara, ikiwemo Mheshimiwa Waziri. Hili ni jambo la kupongezwa na la kuungwa mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza kwa kuja na Vijana Uchumi Challenge kwa ajili ya kuibua vipaji vya vijana wenye mawazo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ushauri wangu kwenye Wizara hii, moja, kwa kuwa tuko katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, na kwa kuwa malengo ya dira hii ni kwamba tuhakikishe sekta binafsi inachangia 70% ya uchumi wa Taifa letu, na kwa kuwa nguvu kazi ya Taifa hili ni 76% ambayo kundi kubwa ni vijana, ipo haja ya Serikali kuanza kupitia upya sheria, sera, na kanuni zetu ili kuhakikisha zinafungamanishwa na ushiriki wa sekta binafsi, pia kuhakikisha kuwa vijana wanapewa nafasi na kwamba wanatambulika katika kushiriki kwenye marekebisho ya sera, kanuni pamoja na sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo tuna Sheria ya Public Private Partnership ya Mwaka 2023, lakini ukiitazama ile PPP Act na ukija kutazama Sheria ya Procurement Act unaona kabisa hatuwezi kufungamanisha vitu hivi viwili na tukapata tija kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia PPP Act inatoa fursa kwa mwekezaji mwenye wazo la kuendeleza miradi kupata hiyo fursa ya kuweza kuendeleza miradi, lakini ukija kwenye Procurement Act inataka utaratibu na mmlolongo mzima wa Serikali uweze kufuatwa ili mtu aweze kupatikana wa kufanya shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta Procurement Act mchakato unaweza kuchukua zaidi ya siku 90, lakini mbaya zaidi waombaji wanakuwa wengi pengine hata yule ambaye alikuja na lile wazo asibahatike kuweza kushiriki kufanya lile wazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja ya sheria zetu kufanyiwa mapitio, na sheria ambazo zimekaa kwa zaidi ya miaka 10 zifanyiwe maboresho ili ziendane na masuala ya Public Private Partnership pamoja na ushirikishaji wa vijana. Hili ni jambo kubwa na ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, sasa hivi tuna Wizara hii, lakini tunahitaji instruments za kuweza kuisimamia Wizara hii. Leo hii maafisa vijana wapo chini ya halmashauri chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii. Ipo haja ya maafisa vijana kwenye halmashauri waripoti moja kwa moja Wizara ya vijana ili waweze kuwa na dhana ya uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mabadiliko hayo yamefanyika kwenye Wizara mbalimbali wakati halmashauri kipindi cha nyuma maafisa hawa, ma-engineer wa maji walikuwa chini ya halmashauri, lakini sasa hivi hawa Wakurugenzi, Maafisa wa Idara ya Maji wanaripoti moja kwa moja Wizara ya Maji na wanajibishwa na Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa maafisa wa vijana hawatakuwa chini ya Wizara ya Mheshimiwa Waziri, ni ngumu sana kuwawajibisha kwa sababu watakuwa chini ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maafisa vijana ambao ni wazee, uwezo wao wa kufanya kazi ni mdogo, uwezo wao wa kubuni ni mdogo. Hili jambo la kuwa na watendaji wanaoendana na kasi ya vijana ni muhimu sana kuzingatiwa katika kuwapata hawa watendaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi tuna Sera ya Maendeleo ya Vijana ambayo imekuwa reviewed 2024. Pia tuna mkakati wa utekelezaji wa sera hii wa miaka kumi, 2024 hadi 2034, lakini hatuna mpango kazi wa muda mfupi na muda mrefu ambao utatupatia majibu, mpango kazi kuhusiana na umuhimu wa kupata masoko ya uhakika kwa vijana, mpango kazi utakaoonyesha mkakati wa kupata elimu ya ujuzi kwa vijana, mpango kazi utakaoonyesha miundombinu wezeshi kwa ajili ya kukuza ujasiriamali na uwekezaji, mpango kazi ambao utaonyesha ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ipo haja ya kuwa na mpango kazi ambao utatupa direction kwa ndani ya miaka hii 10, nini tunaenda kukifanya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni hili la benki ya vijana. Ninapongeza kwa kuwa na wazo hili na kuanza kulichakata. Ipo haja ya kuwa na benki ya maendeleo ya vijana. Kama tumeweza kuwa na Benki ya Maendeleo ya ya Kilimo tunashindwaje kuwa na benki ya maendeleo ya vijana ilhali 76% ya nguvu kazi ya Taifa hili ni vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna programu na mifuko 74 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, lakini pengine vijana wanafahamu mifuko miwili tu. Wanafahamu mfuko wa 10% na wanafahamu na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, lakini leo tuna mfuko wa Small and Medium Enterprises Fund, tuna Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali, tuna Mfuko wa Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, tuna mifuko 74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani mifuko hii iratibiwe na benki ya maendeleo ya vijana ili vijana sehemu zote ndani ya nchi yetu waweze kupata fursa ya mitaji kwa sababu changamoto kubwa ya vijana ni suala zima la mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa 10% kipindi cha nyuma mchakato ulikuwa unawa-favour baadhi ya watu na kuwanyima baadhi ya watu nafasi. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisimamisha mchakato huu, na baadhi ya maeneo sasa hivi pilot imefanyika kwa ajili ya hizi fedha za 10% kupitia benki zetu. Hata hivyo taarifa iliyopo benki nyingi mpaka sasa hawajatoa fedha hizi za 10% kwa vijana, lakini pia kuna urasimu mkubwa wa utolewaji wa fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tangu maelekezo yametoka ni takribani mwaka mmoja sasa hivi. Tunatamani tupate tathmini ya uhakika, je, kupitia mfumo huu wa benki pilot study inakuja na majibu gani? Kuna haja ya kuendeleanao au hatuna haja ya kuendeleanao ili vijana huko kwenye halmashauri zetu waweze kupata fedha hizi?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, ninataka niwaambie vijana wenzangu, tumekuwa na ulalamikaji kwamba hatushikwi mikono. Serikali imeanza kutushika mikono, tuache kulalamika vijana wenzangu, tutumie fursa hizi zilizopo ili tuweze kujikwamua kiuchumi. Tanzania itajengwa na sisi sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ninakushukuru sana.