Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niwe miongoni mwa wachangiaji wa hotuba hii ya Ofisi ya Rais, (Maendeleo ya Vijana).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu kwa uwasilishaji mzuri, na kwa kweli hotuba iliyowasilishwa hapa inaendelea kuonesha dira na matumaini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umaalum sana, kwa dhati ya moyo wangu, ninaomba nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na mapenzi, lakini kiukweli Mheshimiwa Rais anawapenda sana vijana wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais mapenzi yake ameyadhihirisha katika nyanja mbalimbali, lakini kubwa zaidi ya yote kwa kutuletea hii Wizara ya Vijana. Ameenda kuwagusa vijana wa nchi hii na kuona kwamba changamoto za vijana sasa zinaenda kuwa historia katika nchi ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, ninaomba nitoe rai. Mheshimiwa Waziri imani aliyopewa na Mheshimiwa Rais ni kubwa na sisi wasaidizi wa vijana wa nchi hii tunamtegemea sana. Ninataka nimwambie, ameanza vizuri, amechaguliwa, unatushirikisha sisi wasemaji wa vijana, tunapanga na tunajadiliana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutachoka, tutaendelea kuleta maoni ya vijana, tutaishauri Serikali kwa hekima, na pia tutakapoona kuna changamoto kwa maslahi ya vijana, tutaendelea kuzisema ili ziweze kupatiwa ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wanasema, kushukuru ni kuomba tena. Kwa niaba ya vijana wa nchi hii, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kututengea na kutupatia zaidi ya shilingi bilioni 200 ili ziweze kuwanufaisha vijana wa nchi hii. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais na tunampongeza kwa ujasiri mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri nilipata nafasi kushuhudia tukio hili ambapo hizi shilingi bilioni 200 zilipotolewa nilikuwepo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, na vijana wamefarijika sana. Kabla sijaelekea kwenye mchango wangu, ninataka nitoe ushauri mdogo kwenye hizi shilingi bilioni 200. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lililofanywa na Serikali siyo baya, ni jema. Fedha hizi kugawanywa katika Wizara za Kisekta, tunaona kwamba fedha hizi zimekwenda katika Sekta ya Kilimo, Sekta ya Uvuvi, Sekta ya Madini, na Wizara ya Michezo. Tunaishukuru Serikali kwa mgawanyo wa fedha hizi, lakini bado vijana wana maswali wanatuuliza. Hivi ni nani coordinator wa hizi fedha? Nani anazisimamia hizi fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Vijana amepewa mandate ya kupokea tu, lakini coordinator wa hizi fedha ni nani? Sisi tukiwa na maswali yetu tumwulize nani kwenye Wizara za Kisekta? Vijana wakitupigia simu, tunakwenda kwa Waziri wa Vijana; kwa Waziri wa Vijana zime-shift, zimekwenda kwenye Wizara za Kisekta. Hatukatai kwamba kwenye Wizara za Kisekta hakuna vijana, wapo, lakini bado Wizara hizi wanatakiwa waanzishe mfumo maalum wa kuwasaidia vijana wetu hasa huku maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, wanatakiwa wapate taarifa za kutosha. Vijana hawana taarifa za kutosha kuhusiana na hii mikopo, lakini hata masharti ambayo yametolewa, sisi sote tunafahamu. Waheshimiwa Wabunge tulipochangia katika Ofisi ya Waziri Mkuu tulisema kwamba katika ngazi za halmashauri watendaji au watumishi wanao-deal na masuala ya vijana huko chini hawapo, na mikopo hii baadhi ya hizo Wizara ambao wame-highlight tangazo lao, wamesema kwamba matangazo haya yanatoka katika halmashauri. Huko katika halmashauri ni nani ambaye anamfundisha kijana kuandika hilo andiko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vijana wote wana utaalamu wa kuandika maandiko. Tunaomba sana, bado kuna haja ya kutosha ya kuwasaidia vijana. Fedha zilizotoka ni nyingi sana. Mheshimiwa Rais ameshatekeleza ahadi yake, bado tuna nafasi na muda upo, Mheshimiwa Waziri a-coordinate na hizi Wizara nyingine ili tuweze kuwasaidia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana bado wana malalamiko makubwa, na kiukweli wanahaitaji kusaidiwa kwa sababu tusipowasaidia vijana hawa, fedha hizi watazipata majujarei. Fedha hizi lengo lake ni kuwasaidia hata vijana hawa maskini, vijana wa vijijini na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niliombe hilo, nitoe angalizo. Mheshimiwa Waziri tunakuamini na tunatamani hili tuendelee kulisimamia ili vijana wetu waweze kupata matokeo chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba niende kwenye mchango wangu. Wote mtaungana na mimi kwamba zaidi ya 76% ya vijana wa nchi hii ndio wanaojishirikisha katika shughuli za kiuchumi. Kwa mantiki hiyo, hatuwezi kumtenganisha kijana wa Tanzania na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, hilo jambo haliwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunatakiwa tubadilishe mindset za vijana. Tuzibadilishe kwa kufanya mambo yafuatayo ili tuweze kuifikia hiyo Dira ya 2050. Wizara ya Vijana lazima tujipambanue, na kujipambanua kwetu sasa tuwaandae vijana ili waweze kupigania fursa ambazo siyo ajira rasmi, kwa sababu sasa hivi ajira zinapotangazwa vijana wanahisi ndiyo kipaumbele, lakini kumbe zipo ajira ambazo siyo rasmi zinazoweza kuwasaidia vijana wa nchi hii, lakini lazima tuweke miundombinu mizuri na rahisi kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii itafanywa na Serikali, lakini pia Mheshimiwa Waziri ndio ambaye tunamtegemea. Jambo la kwanza kwa Mheshimiwa Waziri tunaomba sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, jambo la kwanza na wakati muda umeisha!
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Eeeh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie.
MWENYEKITI: Malizia kidogo.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri tujikite katika mambo makuu manne. Jambo la kwanza, elimu ya ujuzi wa kisasa; jambo la pili, kilimo cha kisasa, tuwawezeshe vijana katika masuala ya kilimo; jambo la tatu, tuzirasimishe sekta ambazo siyo rasmi kuja kuwa sekta rasmi ili kuweza kuwasaidia vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, siyo kwa umuhimu, uwezeshaji wa kiuchumi na ujasiriamali kwa vijana. Hapa ndipo kwenye fursa za vijana, ninaomba sana tuyazingatie haya ili kuweza kuwasaidia vijana wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)