Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edibily Kinyoma Kazala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya maendeleo ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na uhai. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona ipo haja ya kuanzisha Wizara hii ya Vijana. Nchi hii zaidi ya 70% ni vijana na nikinukuu maandiko ya Biblia kwenye Mithali 20:29 inasema; “Fahari ya vijana ni nguvu zao.” Pia, inasema; “uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi.” (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fahari yetu sisi vijana ni nguvu na huwezi ukaendesha Taifa au tukafanya lolote bila kuwa na nguvu. Ikitokea vita kwenye nchi hii tutawahitaji sana vijana ili wawe mstari wa mbele kulitetea Taifa lao kuhakikisha amani inaendelea kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini wazee pia wana mchango wao, ndiyo maana nimesema kwamba uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi, kwa hiyo, watatusaidia busara na kutu-control, kutushauri kuhakikisha mambo yanaenda vizuri, lakini mambo yanayohitaji nguvu na usasa na mambo yale yanayohitaji innovation na mambo mengine mapya mengi sana vijana ndiyo wanaokuwa na mawazo chanya kwa kuibua vitu vipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia duniani waliofanya vitu vikubwa, mawazo mengi waliyapata wakiwa vijana. Kwa hiyo, ndiyo maana ninasema kwamba vijana ndio wenye nguvu na ndio tumaini na engine ya Taifa letu. Nimeona dira ya vijana, miongoni mwa vitu walivyozungumza kwenye dira yao, wanataka kuwa na Taifa la vijana wenye ujuzi, ufahamu, vijana waliowezeshwa kama walivyotaja pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaangalia kwenye bajeti yao, 14% ndiyo inazungumzia kuhusiana na uwezeshaji wa vijana. 86% kwenye bajeti yao ni matumizi ya kawaida na mishahara. Kwa kweli mimi kwenye hili nimesikitika kidogo. Kama tuna dhamira ya dhati kama Taifa na tunataka Taifa letu liende mbele na lifikie dira 2020 - 2050 sidhani kama hii shilingi bilioni tano inaweza ikaleta mabadiliko ya kutisha kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningetarajia pengine Wizara hii, yale matrilioni tunayoyasoma kwenye Wizara nyingine yangekuwa yako kwenye Wizara ya vijana. Maana tukizungumzia kilimo, tunahitaji vijana waende kule wakalime. Tukizungumzia viwanda, tunahitaji vijana kule waende wakafanye kazi. Sasa, shilingi bilioni tano hizi zinaenda kufanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna shilingi bilioni 200, ninamshukuru Mheshimiwa Rais. Hizi shilingi bilioni 200 zimetengwa kwa ajili ya vijana, na Waziri wetu sisi vijana, yule amekaa pale lakini ukimwuliza hizi fedha ziko wapi? Anakwambia, ziko kwenye kilimo, ziko sekta ya viwanda na biashara au ziko kule sijui kwenye Wizara ya Utamaduni na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, mifuko yote, fedha zote zinazohusu maendeleo ya vijana ziwe kwenye Wizara husika, ya Vijana. Hata tukija tukimwuliza kwamba hizi fedha zimefanya nini? Awe na majibu kwamba hizi shilingi bilioni 200 zimefanya moja, mbili, tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nizungumzie kwenye ajira. Zaidi ya vijana 700,000 mpaka 900,000 kwa mujibu wa World Bank, wana-graduate kuingia kwenye soko la ajira. 10% ndiyo vijana wanaoingia kwenye formal sector, ila 90% wengine wanazurura kule au wanafanya vitu ambavyo Serikali hatutambui, wanaenda kwenye informal sector. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, tuwe na mfumo ambao una-track vijana wetu. Tuwe na Youth Tracking System ambayo itawatambua vijana wetu waliomaliza vyuo, wanaohitimu masomo. Tujue vijana wetu wamehitimu na ujuzi gani? Pia, tujue vijana hawa wanajishughulisha na nini, na wako wapi ili tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninashauri, kwa mfano kwenye force account. Mwaka 2025 tulikuwa na miradi zaidi ya 29,000. Miradi hii iko kule kwenye halmashauri na kule ambako wanasimamia mpaka walimu wa shule ya msingi, sekondari, na madaktari, lakini huku tuna vijana ambao hawana kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miradi hii tusii-group vijana hata watano watano basi, tuwape hii miradi ya force account waende kule vijijini watekeleze kuliko kumpa Mwalimu ambaye tayari ana ajira, unampa tena akasimamie mradi wa force account. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)