Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii adhimu nami kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Maendeleo ya Vijana. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai nami kuweza kusimama leo katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na pongezi kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mheshimiwa Emmanuel John Nchimbi, na Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Lameck Nchemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zinaenda sambamba na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Tumeona Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu anahangaika kila mikoa kutafuta kero, kutafuta changamoto na kuzipatia majawabu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Kaka Joel Nanauka, akifuatana na Katibu wake Mkuu Mama Jenifa Omolo pamoja na wasaidizi wao wote, kwani wanafanya kazi nzuri na pia wameanza vizuri katika utekelezaji wa kazi za Wizara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapongeza kwa taarifa yao nzuri, kwa kweli taarifa yao imewasilishwa kwa kina, imeeleweka na imegusa maeneo mbalimbali ambayo ni kero kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini ya kwamba, kuanzishwa kwa Wizara hii ni kuhakikisha kwamba tunainua uchumi wa vijana wetu. Ili tuweze kuwafikia vijana hawa, ni lazima wataalamu wetu wa Wizara hii wafike ngazi za chini (Local Government) kwenye ngazi ya kata, kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa ili waweze kuwasaidia vijana wetu hata katika kuandika maandiko ambayo yanatakiwa kwenye matangazo ya uombaji wa shilingi bilioni 200 ambalo tangazo lake lilisema, limetolewa tarehe hiyo, ambalo lilihusu fursa za mkopo za Mfuko wa Maendeleo kwa Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mambo yaliyokuwa yanahitajika ni pamoja na kuwa na eneo la sifa za mwombaji, namna ya kuomba mkopo, wametoa maelekezo, na pia wamesema mwombaji anatakiwa aambatanishe nyaraka zifuatazo: ikiwemo na andiko la mradi lisilopungua kurasa tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kule kwetu Mandepwende mtu anajua hata hilo andiko la mradi wenye kurasa tano? Hapana, tusifanye hivyo, turahisishe haya masharti, tuendane na maeneo. Kama kule wananchi wa kwetu wengi wao hawaelewi haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba wataalamu wa Wizara washuke chini kwa ajili ya kufanya usaidizi kwa vijana wetu hawa, ikiwezekana waweke hata kliniki waweze kuwasaidia waandike andiko wawakague kwamba andiko linaandikwa hivi. Vinginevyo patayarishwe fomu zenye maelekezo yote, yeye awe anajaza pale sehemu za wazi tu. Hiyo itakuwa imemsaidia kijana kuepuka na kujua hilo andiko la mradi ni kitu gani? Kwa hiyo, tuboreshe baadhi ya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, tumeona Mheshimiwa Waziri amefanya ziara kwenye baadhi ya mikoa ikiwemo na Mkoa wa Ruvuma. Kwenye ukurasa wake wa saba ameeleza ya kwamba amekutana na hoja 186 ikiwemo hoja ya mikopo ya 10% ile ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza, huu mkopo wa 10% upo kwenye wanawake, vijana, wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na makundi maalum, yaani wenye ulemavu asilimia mbili. Huu mkopo nilikuwa napendekeza uhame kutoka kwenye halmashauri uende kwenye Wizara yake ili iwe rahisi hata kwenye kufanya ufuatiliaji na tathmini wa mkopo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vijana wengi wanahangaika wanatoka huko, wanaenda kwa Mwenyekiti wa Mtaa, mara halmashauri, mara kwa Mbunge, wanaenda kuulizia tunapataje huu mkopo? Ni kweli mkopo huu una urasimu mkubwa. Ili kuondokana na dhana hii, tunaomba huu mkopo uhamie kwenye Wizara ambayo imeweza kuwekwa peke yake, Wizara inayohusiana na maendeleo ya vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, ili tuweze kuwafikia vijana wetu, lazima elimu itolewe kwenye redio na siyo redio hizi za Tanzania tu, hapana kwenye local radio kulingana na maeneo yetu. Kwa mfano, eneo letu la Mkoa wa Ruvuma tunazo redio nyingi tu kulingana na wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Tunduru iko Wapo Redio, vijana kule wanapenda kusikiliza hiyo redio. Ukiwawekea vipindi pale ukatenga muda wa saa moja au mbili huku wanasikiliza muziki, huku wanasikiliza vipindi hivyo vya maendeleo kwa vijana, tutakuwa tumewapa elimu tena kwa gharama nafuu, kuliko kusubiri unawakusanya vijana wengi kwenye ukumbi eti unawapa elimu. Watapatikana vijana wachache tu. Hawawezi kufikia vijana wote wa lile eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Ruvuma ukienda Namtumbo unakuta kuna redio inaitwa Site FM, Songea Mjini local radio iko Redio Jogoo, Redio Selous, Majimaji, Mbinga na Nyasa unakuta redio inaitwa Salvation Radio na Hekima Radio. Hizi zote tukiwapa matangazo haya wataweza kuelewa badala ya kusubiri uwakusanye kwenye mkutano maalumu ndiyo unatoa elimu, hapana. Elimu hizi ziende kwenye redio zetu za kule maeneo ambako tunatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda pia kwenye eneo la urejeshaji wa mkopo hasa huu wa shilingi bilioni 200, tumeona muda wa marejesho ni kuanzia miezi mitatu hadi sita. Hii siyo sawa. Huyu kijana aliyekopa, ukimpa miezi mitatu atakuwa hata biashara yake hajaizungusha. Naomba tuongeze muda, badala ya kuanzia hii miezi mitatu, twende miezi sita. Tuanze na miezi sita angalau awe amefanya hiyo biashara yake. Tukifanya hivi hawa vijana wetu tutakuwa tumewasaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, pia liko eneo ambalo tunasema vijana wetu wana ukosefu wa ajira. Tunaamini ya kwamba tukiwawezesha hawa vijana, ajira yao itakuwa inatokana na hii mikopo na hawataweza kujiajiri wao wenyewe tu, wataweza kuajiri na vijana wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria, yako maeneo ambapo mikopo hii sidhani kama itawafikia kwa sababu naona kwenye hizi shughuli ambazo zimeainishwa hapa, wengine hawazifanyi kabisa na au wanafanya kwa kiasi kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, afanye maboresho kwenye baadhi ya maeneo ili vijana wengi waweze kujiajiri wenyewe kuliko wanavyohangaika hivi sasa wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaendesha bodaboda siyo kama wanapenda. Anachukua bodaboda ya tajiri, anaendesha, anafanya marejesho pale ya shilingi 8,000 ili mradi na yeye abakiwe na fedha kidogo, lakini kama tutawawezesha kwa utaratibu ambao tutakuwa tumeuboresha, ninaamini vijana wengi tutakuwa tumewafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ninaamini ni Wizara mtambuka na inafanya mambo mengi makubwa na mazuri. Ninaomba tuendelee kushirikiana na vijana, na watendaji wale wa kutoka kwenye halmashauri ili tuweze kuboresha Wizara hii na iweze kusonga mbele, na vijana wasiwe na maswali kwa wataalamu wa ngazi za chini. Watoke wale wa juu wa halmashauri waende wakaelekeze ngazi za chini, waandae; hata hiyo kliniki kwa ajili ya kuboresha maslahi ya vijana wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, ninakushukuru. (Makofi)