Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asma Ali Mwinyi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASMA ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kusimama, nami nichangie hoja katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunipendekeza kugombea Jimbo la Welezo. Pia ninaomba kumshukuru pia Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, kwa kazi nzuri anayoifanya na pia kwa maendeleo mazuri anayotuletea, na hususan katika Jimbo letu la Welezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Katibu wetu, Mheshimiwa Mary Chatanda, kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya. Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipowashukuru wananchi wa Jimbo la Welezo kwa kunichagua kuwa Mbunge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hii ya leo ninaomba kuunga mkono jambo la ajira ambalo tayari limeshaongelewa, na ni jambo linalowagusa wananchi wangu moja kwa moja, na sisi wengine ni vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi, takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya 50% ni vijana nchini kwetu, lakini pia ni asilimia kubwa ambayo pia Jimbo la Welezo, bado vijana wanakosa ajira. Hili la ajira siyo kwa Jimbo la Welezo tu, lakini nchi nzima. Ninavyosema vijana, ninaongelea vijana wa miaka 15 mpaka 35, na hawa takwimu inaonesha ni milioni 33.16 ya Tanzania Bara, na ni 53.7% ya Watanzania wote; na kwa upande wa Visiwani ni milioni 1.08 ambayo ni sawa na 57.4%. Vijana hawa wote bado wana changamoto kubwa ya ajira inayowakabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongelea ajira, siongelei tu ajira yoyote, ninaongelea ajira zenye staha, yenye heshima, ajira ambayo inawawezesha vijana hawa wakaishi, wakanyanyuka kiuchumi wakaishi kwa heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona Mheshimiwa Waziri Mkuu aliongelea vitu vikuu vitatu kuhusu bajeti yake ya 2026/2027. Cha kwanza, aliongelea kuimarisha sekta binafsi ili iwe engine ya ajira kwa vijana; pili, ni kuwekeza zaidi katika ujuzi na mafunzo; na tatu, aliongelea kuhusu kuboresha mazingira ya biashara na upatikanaji wa mahitaji kwa vijana. Namuunga mkono kwa asilimia mia moja kwa haya ambayo aliyoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuongea kuhusu hii mikopo ambayo inaongelewa ya 10%. Mikopo hii ambayo imewekwa ni mizuri, lakini bado imekuwa ni changamoto kwa vijana wetu kupata stahiki hii moja kwa moja. Hii ni kutokana na urasimu uliowekwa katika upatakanaji wa mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba kutoa mapendekezo machache kwa Serikali. Kwanza kabisa, Serikali iboreshe mfumo wa utoaji mikopo kwa vijana kwa kuondoa urasimu usio wa lazima, kuweka mifumo ya kidijiti ili kurahisisha uwazi, na hii iende moja kwa moja kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali ianzishe Skills Development Sector ambazo zitawasaidia vijana kupata zile skills ambazo wanahitaji ili waweze kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. Hii itasaidia sana katika upatikanaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba Serikali itoe kipaumbele mahususi kwa vijana katika zabuni za miradi ya kimaendeleo. Hii itawasaidia vijana kuweza kujiwekeza wao wenyewe na kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Vijana, nayo pia naipongeza. Ni jambo zuri ambalo wanalifanya na litawasaidia na litaweka uwazi jinsi gani vijana hawa wanaweza kupata hii mikopo na wakajiwezesha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kuongelea kuhusu hii kodi ambayo iliwekwa tax code kwa vijana ambayo inaonekana kwa sasa ni jambo ambalo haliwasaidii kutokana na urasimu uliokuwepo kule. Wanatakiwa watoe angalau fedha mwanzoni, ndiyo wapate. Sasa ndiyo kwanza wanaanza, hii fedha hawana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASMA ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imelia. Katika kuhitimisha kwangu nimeona Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa shilingi bilioni 200 kwa vijana. Ningependa hii pia ingeletwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili vijana wa Welezo na pia wengine wote nao wapate kunufaika. Nasi tunakuahidi tutakuwa mfano wa kwanza Jimbo la Welezo kuonesha jinsi gani tutaweza kutumia na kurejesha hii mifuko, na kufuata masharti kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namaliza kwa kusema kwamba ajira kwa vijana siyo chaguo, ni lazima kwao. Kwa hiyo, tunaomba kwamba sisi tuko tayari, na ninaahidi vijana wa Jimbo la Welezo kwamba niko nao bega kwa bega kuhakikisha kwamba ajira ipo katika ajenda yangu, ili angalau nao wapate, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)