Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Muhsin Haji Ussi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MUHSIN HAJI USSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ametupa afya njema, na leo tupo katika Bunge hili Tukufu kujadili mambo mtambuka yenye maslahi mapana kwa vijana wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vilevile, kumpongeza pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa dhamira zao za dhati za kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusema kwamba nimefanya tafiti na nimejiridhisha kwa Afrika, sisi Tanzania ni nchi ya kwanza kuwa Wizara pekee ambayo ina mamlaka ya wazi na ya moja kwa moja juu ya uratibu madhubuti wa sera na programu zote za vijana. Nchi nyingine zote zinatumia Mfumo wa Integrated Ministry, yaani Wizara ya Vijana imeunganishwa na michezo ama sanaa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea jembe Mheshimiwa Waziri Joel Nanauka, kijana mzalendo, mchapakazi ambaye mimi binafsi nimemfahamu kabla hajawa Mbunge wala Waziri. Amekuwa akishajihisha na kutoa elimu kwa vijana juu ya namna bora ya matumizi sahihi ya fedha (financial literacy) na namna ya kubadilisha maisha yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninataka kuchangia niungane na Wabunge wengi ambao wameshangaa kwamba, Mheshimiwa huyu ana Wizara inayohusiana na vijana na maendeleo yake, lakini hana fedha; na kwa namna anavyofanya kazi mara nyingi yupo site, anakutana na makundi ya vijana na amekuwa maarufu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unampa kazi ya kumchonganisha na vijana wa Kitanzania, watamkimbia huko site wataona Waziri amekuja kupiga soga na sisi, lakini hana fedha. Kwa hiyo, ninaomba zile fedha mahsusi ambazo zimetengwa ikiwemo shilingi bilioni 200 kwa ajili ya vijana zipelekwe moja kwa moja kwenye Wizara hiyo ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwa umakini sana hotuba yake, ukurasa wa 10, Mheshimiwa Waziri anakiri ukosefu wa ajira Tanzania na hasa kwa vijana. Ukosefu wa ajira siyo Tanzania tu, tukubaliane; duniani kote kuna changamoto hii ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, pamoja na utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2023/2024 (Integrated Labor Force Survey) inaonesha zaidi ya 60% ya Watanzania ni vijana ambao wana range kwenye umri wa miaka 15 na 35. Kila mwaka, zaidi wa vijana 1,000,000 huwa wanaingia kwenye soko la kutafuta ajira, wanaofanikiwa ni vijana wasiozidi 300,000, wasiofanikiwa ni vijana wanaozidi zaidi ya 700,000 kwa mwaka. Ni kusema kwamba zaidi ya 12.12% ni vijana ambao wana ukosefu wa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limezidi hata lengo la Taifa ambalo tulijiwekea walau kwa asilimia nane ya ukosefu wa ajira. Hata hivyo, inaonesha vijijini kuna unafuu zaidi kuliko mijini, vijana wengi wa mijini wanahangaika na ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata maandiko Matakifu ya Biblia yanasema, “Mtu yeyote asiyefanya kazi basi na asile.” Hata Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, miongoni mwa masharti ya uanachama, sharti nambari tatu inasema, “Ukiwa mwanachama uwe ni mtu mwenye kuamini ya kwamba kazi ni kipimo cha utu na kuitekeleza imani hiyo kwa vitendo.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za mwaka 2024 zimeonesha, Tanzania ina watumiaji zaidi milioni 30 wa internet. Sasa ninataka kuja hapa kumsadia Mheshimiwa Waziri, anawezaje kutatua changamoto ya vijana wa mijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumiaji wa laini za simu zilizosajiliwa ni milioni 60. Katika hizo, laini milioni 35 zinatumia mfumo wa mobile money, yaani mfumo wa kutumia simu kwa ajili ya kufanya miamala ya kifedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe ushauri kwa Wizara, ili kuondoa changamoto hii Mijini, kwanza kwa upande wa sera, kuanzishwe vituo vya TEHAMA vya Kitaifa katika miji mikubwa. Kwa mfano, tunaweza tukawa na kituo pale Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule India mwaka 2015 walianzisha kituo kinaitwa Digital India ambacho kilikuwa kinafundisha vijana mambo mbalimbali ikiwemo artificial intelligence, freelancing, digital economy na kadhalika. Vijana wetu wengi sasa hivi wanatumia mitandao, wanatumia internet, hii itasaidia kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Zanzibar, ukienda Jimboni kwangu Malindi kuna eneo linaitwa Forodhani, kuna vijana wa Makachu wanatumia internet, na mitandao ya kijamii kuonesha namna gani Zanzibar na Tanzania ilivyo nzuri na kuvutia uwekezaji na watalii wengi. Vilevile, Serikali itoe motisha za kikodi kwa kampuni ambazo zinaajiri vijana na hasa katika eneo hili la teknolojia na mitandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mchango wangu wa mwisho. Ukurasa wa 10 huo huo, Mheshimiwa Waziri amekiri ya kwamba vijana wanakosa ujuzi na utaalamu ambao unaendana na mahitaji ya soko. Nimezungumzia vijana wa mjini, sasa wataniuliza wa kule vijijini inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna kitu cha kujivunia Tanzania, tuna ardhi nzuri yenye rutuba kwa ajili ya kilimo. Inaonesha zaidi ya 60% ya Watanzania wamejiwekeza kwenye kilimo. Niliwahi kusema hapa kwamba vijana tunakimbia kilimo, na sababu ziko wazi. Moja, kilimo hakina teknolojia ya kisasa; pili, hakina faida ya haraka; tatu, hakina mfumo mzuri wa soko. Kijana yuko tayari awe na bodaboda apate shilingi 10,000 kwa siku kuliko kuwekeza kwenye kilimo kitakachomtajirisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema hivi, “Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi.” Uti huu wa mgongo unahitaji kuimarishwa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiulimwengu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii kuishauri Serikali, kwanza, kuanzisha agri-business parts (kilimo biashara). Nitatoa mfano, kule Brazil wamefanikiwa sana kwa sababu, kilimo kimeunganishwa moja kwa moja na usindikaji na masoko. Kwa hiyo, vijana wanalima, wanapata fedha, na Serikali inakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuwe na mfumo wa mkataba unaitwa contract farming. Kule China wakulima wadogo wadogo wameunganishwa na kampuni kubwa za kilimo. Tunaacha udalali hapa katikati, vijana wanapata fedha, Serikali inapata uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, kuna kitu kinaitwa agritech. Kuna siku nilikuwa ninamtembelea, rafiki yangu kule Songea akaniambia siwezi kupata mazao kwa sababu ya mvua. Ninaishauri Serikali, tuwekeze katika irrigation, tuangalie namna bora ya kuwa na drones ambazo zitaweza kusaidia hususan kwenye umwagialiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)