Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Tinnar Andrew Chenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Wizara ya Maendeleo ya Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumrudishia sifa na utukufu kwa kunipa uhai wa kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kwa kuanzisha rasmi Wizara ya Maendeleo ya Vijana na kumteua kijana msikivu Mheshimiwa Joel Arthur Nanauka kuongaza Wizara hii ambayo imebeba changamoto, maono na matarajio ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, na kama ilivyowasilishwa kwenye taarifa yetu, tulipata bahati ya kutembelea kikundi cha vijana ambacho kipo pale Muheza Tanga. Kikundi hiki ni moja ya vikundi vya vijana ambavyo vinafanya vizuri sana. Ninaiomba kabisa Wizara iendelee kukilea kikundi hiki lakini pia kutumia kikundi hiki kama balozi wa mafanikio kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikundi hiki kinafanya shughuli zake pembezoni mwa barabara. Ninaomba sana uongozi wa Mkoa wa Tanga uone namna ya kuwatafutia eneo la kudumu vijana hawa ili waweze kufanya kazi zao kwa tija. Kikundi hiki pia kinazalisha bidhaa za ujenzi. Ninaomba sana uongozi wa Mkoa wa Tanga uone namna ya kuwasapoti vijana hawa kwa kutumia bidhaa zao kwenye miradi ya ujenzi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, vijana hawa waliomba mkopo kwa ajili ya kutafuta usafiri, kuweza kusafirisha bidhaa zao kuzipeleka kwa wateja. Ninaiomba sana Wizara ione namna ya kuwapatia mkopo huu ili waweze kufanya kazi zao na kuwapunguzia gharama za kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Wizara hii imetenga bajeti ya shilingi 35,957,298,000. Kati ya hizo, zilizotengwa kwa miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni tano plus. Kwangu mimi ninaona fedha hizi bado ni kidogo ukilinganisha na mahitaji makubwa ya kundi hili maalumu la vijana ambalo ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Serikali ione namna ya kuongeza bajeti kwenye eneo hili. Ninaungana na Wabunge wenzangu kusisitiza kwamba zile shilingi bilioni 200 za vijana zirudi kwenye Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba niendelee kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kuwainua kiuchumi siyo vijana tu, bali wanawake na watu wenye ulemavu. Ninaomba sasa nichangie katika maeneo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ni kuhusu mitaji kwa vijana. Vijana wengi wana nia na ari ya kufanya kazi, lakini wanakosa mitaji au wakati mwingine wanakutana na masharti magumu ya mitaji au mikopo hii, kiasi ambacho wanashindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba hapa Serikali iongeze juhudi katika kuhakikisha kwamba inapunguza urasimu wa upatikanaji wa mikopo hii. Hapa ninaomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kauli yake ya kusema kwamba, tutumie NIDA badala ya kuomba barua. Kwa hiyo, kama mtu ana NIDA, hakuna sababu ya kupewa barua ya utambulisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni changamoto ya ujuzi usioendana na soko halisi la ajira kwa sasa. Ni dhahiri kwamba, bado kuna pengo kati ya elimu ambayo tunaitoa kwa wahitimu wetu na soko la ajira. Ninaiomba Serikali iendelee kuboresha mitaala, hasa kwenye eneo la mafunzo kwa vitendo, teknolojia na ubunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ajira zisizo na uhakika wa kipato kwa vijana wetu. Vijana wetu wengi wanafanya kazi katika sekta ambayo siyo rasmi, ambayo haina uhakika wa kipato cha kudumu, lakini pia, haina uhakika wa hifadhi ya jamii. Hapa ninaiomba Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi iongeze rasilimali zaidi kwenye sekta zenye kutoa ajira nyingi, kwa mfano, kwenye Sekta ya Viwanda pamoja na Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la afya ya akili. Kutokana na matatizo na changamoto, vijana wetu wengi wanakumbwa na tatizo la msongo wa mawazo. Kwa ajili hiyo, wengine wamefikia hatua wanakata tamaa, na wengine wanaingia kwenye vitendo ambavyo havina tija, kwa mfano kucheza kamari kupita kiasi. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iwekeze zaidi kwenye eneo la afya ya jamii kwa kuongeza wataalamu wa kutoa ushauri nahasa kwa vijana wetu, ili kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni matumizi yasiyo na tija ya mitandao ya jamii. Ni ukweli usiopingika kwamba, mitandao ya jamii ni fursa na ni uchumi kama ikitumika vizuri, lakini bado vijana wetu wengi wanatumia mitandao hii vibaya. Ninaiomba Wizara, ikishirikiana na wadau wa vijana, ione namna ya kuwaelimisha vijana wetu juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya jamii, ili waweze kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mifano mingi ya ambao wanatumia mitandao ya jamii na wanaishi maisha yao vizuri kama akina Shilole, Niffa, na Kelvin. Ninaomba tujifunze kutoka kwa vijana hao. Ninaiomba Wizara iendelee kuwafikia vijana, hasa wale walioko katika maeneo ya vijijini, ili na wenyewe waweze kupata fursa kama vijana wa mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ukosefu wa mwongozo au mentorship kwa vijana wetu. Vijana wetu hawajapata watu wa kuweza kuwasaida katika safari zao za kiuchumi au kitaaluma. Ninaomba tuwekeze sana kwenye eneo hili, ili tupate washauri watakaoweza kuwasaidia katika kuwapa mwongozo wa namna gani hasa kwenye eneo la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, japo siyo kwa umuhimu, ni kitu ambacho mimi ninakiita after care, hata sisi wazazi tukishajifungua kuna kitu kinaitwa postnatal. Sasa, ni kweli tunawapa vijana mikopo, lakini mara nyingi hatuwafuatilii kwamba wanaendeleaje? Ninaomba tuweke mkazo kwenye ufuatiliaji, ili kuweza kubaini changamoto za vijana hao. Siyo changamoto tu, na maendeleo yao pia, ili tuweze kuwapa ushauri wa namna gani ya kutunza fedha, kwa sababu, hapa ndiyo kwenye tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. Ninaomba kuwasilisha. (Makofi)