Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Saidi Salim Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ole

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SAIDI SALIM HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru nami kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi. Pia ninaishukuru Kamati za Siasa kwa ngazi zote zilizonipitisha kuanzia mkoa na wilaya. Kipekee kabisa ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Ole, hususan Wajumbe, wamekuwa wema kwangu, ni watu wazuri. Wajumbe hawa watakapokufa wote wataingia Peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa Wizara hii ya Vijana, ninatanguliza pongezi. Pongezi hizi ninazielekeza moja kwa moja kwa Wizara inayoongozwa na kaka yangu, Mheshimiwa Nanauka. Tarehe 4 Aprili, 2026 nilisimama ndani ya Bunge hili Tukufu kuchangia, nikauliza, kwa nini tusianzishe Benki ya Maendeleo ya Vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hilo leo katika wasilisho la Wizara hii, Mheshimiwa Waziri amesema sasa ni muda sahihi wa Serikali, kupitia Wizara ya Vijana, kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Vijana ili Vijana wa Kitanzania waende wakafungue akaunti zao, na wakafanye cash deposit hapo. Wakiwa wanahitaji kukopa, waende wakakope katika Benki yao ya Maendeleo ya Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipa pongezi Serikali kupitia Wizara hiyo. Nasi mnatupa imani ya kutafuta fikra mbalimbali kuja kuishauri Wizara, kwani tumeona mawazo ambayo tunayaleta, yanachukuliwa, yanachakatwa na wakiona yanafaa, basi wanakuja nayo kwenye mikakati yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Wizara ninaomba nichangie, kwa ruhusa yako, kuhusu fursa za vijana ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitengeneza kupitia Wizara mbalimbali. Tunajua tuna Wizara ya Vijana ambayo ni mpya, lakini kuna fursa za vijana za kiuchumi na za kiajira kupitia Wizara mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, Wizara ya Uchukuzi kwenye Taasisi yetu ya DMI pale, Wizara hii imefanya taasisi zake ziwe za kushikana na kusaidiana. DMI imewezeshwa na TPA chini ya mwekezaji wetu DP World kununua simulator ya kisasa, ambayo inaitwa Full Mission Desk and Engine Simulator. Unaposoma DMI sasa hivi, ndani ya miaka hii miwili iliyopita, unasoma kupitia simulator hii na unapotoka pale unakuwa umebobea. Mtambo huu ambao uko pale ni nchi siyo zaidi ya tatu Afrika nzima ambazo tunaumiliki, tukiwemo na sisi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya mtambo huu ambao umenunuliwa chini ya Profesa Tumaini pale, una thamani ya Dola za Kimarekani 2.8 million. Huu umesababisha vijana wetu wa Kitanzania kwenda DMI, wanapata fursa za kielimu za kisasa na wanapotoka pale wanapata fursa za kiajira, dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Taasisi ile ya DMI tulipokwenda kutembelea, Kamati ya Miundombinu, tumepata fursa za vijana zilizotengenezwa kupitia mtambo huu. Kuna meli za Kimataifa zimejikita sasa hivi kutaka kufunga mkataba na DMI kwamba, cabin crew yote na mabaharia wote wa meli hizo wawe ni vijana wa Kitanzania ambao wametoka pale DMI kupitia mtambo ule. Kwa hiyo, haya mambo hayatokei tu by nature, ni jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Serikali yake, ambayo imewezesha kupata fursa kama hizi za ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna fursa za vijana zilizoko katika Wizara ya Mawasiliano chini ya mama yetu Mheshimiwa Kairuki. Kuna huu Mfuko wa UCSAF, ambao unajenga minara, kama alivyozindua juzi pale Mheshimiwa Mama Samia. Mpaka sasa tumejenga takribani minara 2,151. Sisi tumebahatika kutembelea mnara mmoja tu, Kigamboni. Mnara huo umetengeneza fursa za vijana za ajira na kiuchumi, kama zifuatazo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnara ule wa pale Kigamboni ambao tumeenda kuutembelea umewezesha kuajiri au kujiajiri vijana 157 kama mawakala. Wamepata job opportunity kupitia mnara ule ambao umejengwa. Vilevile kuna vijana wa Bolt na Uber walikuwa pale hakuna network. Kwa hiyo, wanasema mtandao kulikuwa hakuna, walikuwa hawawezi kwenda kutoa service katika maeneo yale. Baada ya kujengwa mnara huu, vijana wetu wa Uber na Bolt wamejikuta wanaenda pale kupata riziki zao za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukakutana na vijana ambao wamejiajiri kupitia online shopping pamoja na delivery services za online pia, nao wamejiajiri baada ya mnara ule kufika pale. Vilevile, tukakutana na wanafunzi ambao wanasoma chuo kikuu. Vijana wetu hawa ambao ni wasomi walikuwa wanapata shida ya mawasiliano wakiwa wako pale Kigamboni, walikuwa hawana network, wakati wa usiku wanasumbuka. Baada ya Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, kupeleka mnara huu, vijana hawa wamepata ajira, mawakala 157, Bolt wanaenda pale kujiajiri, online shopping wanafanya kazi zao na vijana wetu ambao wanasoma, wamejipatia fursa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kutembelea TCAA, kuna fursa iko pale Chuo chetu cha Mamlaka ya Anga Tanzania, fursa ya kipekee kabisa. Kuna kozi inatolewa pale inaitwa ni Aircraft Controller. Hii Aircraft Controller ambayo inatolewa pale, vijana wanatoka Somalia, tumekuta zaidi ya wanafunzi 70 na wengine 34 kutoka Uganda wanasoma kozi ile kwa thamani ya shilingi milioni 70. Ni kozi ya wiki saba, lakini Mheshimiwa Mama Samia katoa maelekezo kwa Mheshimiwa Prof. Mbarawa, Kijana wa Kitanzania anayekwenda kusoma Aircraft Controller ndani ya chuo hiki alipie shilingi milioni 10 tu. Hizi ni fursa ambazo ziko katika Wizara nyingine, lakini zinatufaa sisi vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuchangia mchango wangu. Sisi vijana tulikuwa tunasikitika hapo zamani, zikitokea nafasi za jeshi tunatafutwa vijana; zikitokea nafasi za Polisi tunatafutwa vijana; zikitokea kazi ngumu za zege, tunawekwa vijana; lakini kazi za uongozi hatushirikishwi vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bunge hili ambalo tupo, tuna Wabunge wa Vijana ambao ni Viti Maalumu na tuna Wabunge wa Majimbo ambao ni vijana. Leo ndani ya Bunge hili tuna Mawaziri ambao ni vijana. Leo ndani ya Bunge hili kuna Makatibu Wakuu, kuna Maafisa Mezani pale wote ni vijana. Haya ni maono ya Mheshimiwa Mama Samia kupitia kuwajali vijana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kwa kusoma maneno matukufu kutoka katika Biblia. Methali 3:5-6 kuna maneno ya kumtia moyo Mheshimiwa Mama Samia, yanasema, “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atanyoosha mapito yako.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Kitabu Kitukufu cha Quran kuna aya inayosema, “Isubiru wa Swabiur”. Ee Mama Samia Quran inakwambia; subiria na uvute kwenye subira. Pia kuna aya inasema, “Wa Bashir As-Sabireen.” Nimpe ishara njema Mheshimiwa Mama Samia, kwa anayoyasubiria ndani ya nchi hii. Mama fanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)