Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BENG’I M. ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nami ninapenda nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama wengine walivyosema, kwa kuanzisha Wizara hii, limekuwa ni jambo la kimkakati, na kwa kweli litatusaidia sana kama nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ninapenda niwapongeze kwa dhati kabisa Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa hotuba nzuri na mikakati ambayo wameipanga ya kuendeleza masuala ya vijana hapa nchini. Ninampongeza sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Nanauka, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya tangu alipoteuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda sasa nichangie hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2026/2027. Ninapenda nijikite kwenye muundo wa utekelezaji. Unapokuwa na Wizara mpya kama hii ambayo imeanzishwa sasa hivi, na wakati tayari kulikuwa na Wizara nyingi zinafanya mambo ya vijana, mambo mengi yanakuwa ni magumu mara nyingine kuyatekeleza kwa sababu ni ngumu kumnyang’anya mtu mara moja kitu anachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu ni Wizara ambayo inalenga Kundi la wananchi fulani, ni ngumu pia kusema kwamba kazi zote zitafanywa na Wizara hii, kwa sababu tayari kuna Wizara zinafanya kazi na vijana na ni vizuri wao wakaangalia jinsi ambavyo wataji-network au watajipanga kufanya kazi na Wizara mbalimbali kwa kuzipa miongozo na kuhakikisha kwamba wao wanapata taarifa zote za utekelezaji na kuongoza vizuri masuala ya vijana ambayo yanafanywa na Wizara nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ambalo tumeliona muda mrefu katika masuala ya vijana, tumezungumza mambo mengi kwa kweli, masuala ya ajira ambazo hazina uhakika, ajira za informal sector, suala la uzoefu imekuwa ni tatizo kubwa. Mara nyingi vijana hawapati kazi kwa sababu hawana uzoefu, vilevile ujuzi na maarifa ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wa Kitanzania wanaweza kuwa na ujuzi, tunasema technical skill, lakini wakakosa soft skills. Hiki ni kitu ambacho ni muhimu sana Wizara ikakiangalia, kwa sababu unapokwenda kufanya kazi, unaweza kuwa unajua kazi, lakini usijue kujiongeza, usijue labda customer care na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo kwa sababu hawa ni vijana, na vijana ni wachanga, wanakuwa bado hawajawa exposed kwenye vitu vingi, na kuna vitu vingine hawavifahamu kabisa. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na programs ambazo zitasaidia kujenga tabia zao vizuri na kuongeza ujuzi ambao unahitajika ili wawe vizuri katika vitu ambavyo wanavifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo la upatikanaji wa taarifa ni tatizo kubwa. Hii siyo kwa vijana tu, ni kwa wananchi wengi tu ambao wanahitaji fursa zinazoletwa na Serikali. Kwa hiyo, nimefurahi kusikia kwamba kutakuwa na kanzidata vilevile kuwepo na utaratibu ambao utawafanya vijana wapate taarifa kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mikopo ambayo imetangazwa hivi sasa, na hata zabuni ambazo zinatolewa kwa vijana, sasa hivi bado hawajui wanazipata namna gani? Kwa hiyo, utaratibu wa upatikanaji wa taarifa, lazima utengenezwe na uwe rafiki kuwafikia vijana kwa utaratibu ambao unatakiwa, ambao utasaidia kuwaleta kwa wingi zaidi katika fursa ambazo zinatolewa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa vijana ndiyo ambao ni wabunifu kwa kiasi kikubwa. Tunao vijana wabunifu wengi sana hapa nchini, lakini kumekuwa hakuna utaratibu wa kuwatoa kwenye ubunifu kuwapeleka kwenye kufanya biashara. Mtu anaweza akabuni jambo lake zuri, lakini anakosa ujuzi kwa kutoa ule ubunifu kufanya ile product ikawa product na ikauzika kibiashara. Haya ni mambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulikuwa na tatizo kubwa la biashara zinazoanza (startups). Startups nyingi zilikuwa hazipati mitaji, kwa sababu kila anayetoa mtaji alikuwa anataka uzoefu na vijana wetu walikuwa hawana uzoefu, lakini kuanzishwa kwa Wizara hii kumeleta chachu ya kuangalia hili suala kwa upekee na tunafikiri kwamba kwenye startups tutaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalizo tu ni kwamba, katika utoaji mikopo na kum-finance mtu ambaye anaanza biashara kuna risk kubwa, kwamba unaweza ukatoa fedha na isirudi. Kwa hiyo, ni vizuri sana hawa vijana wakawa na programu za kuwasaidia kujenga tabia zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia tabia hapa, nina maana kwamba tuwe na programu za malezi kwa wale ambao wanafanya biashara ambao ni wazoefu, wawekwe na wafanyabiashara vijana ili kuwafundisha tabia nzuri za kufanya biashara ambayo kwa Kiingereza tunaita mentors.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na mentorship program kwa kushirikiana na taasisi kama hizi za biashara TWCC au TCCIA tutawapa vijana. Kila kijana atakuwa anapata mtu mzima ambaye anaweza kumlea katika shughuli ambazo anafanya za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni masuala ya uvumilivu. Vijana mara nyingi sio wavumilivu, na hili jambo ni lazima wafundishwe kwamba mafanikio hayaji kwa urahisi. Mafanikio yoyote yanahitaji struggle, upitie ugumu ili uweze kufanikiwa. Kama hawaambiwi, hawawezi kujua kwamba lazima upitie mambo magumu, uvumilie, mara nyingine ukae muda mrefu bila kukipata hicho ambacho unakitaka, lakini mwisho wake utakipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni nidhamu ya fedha. Nidhamu ya fedha ni tatizo kubwa sana. Watu wengi tunapenda fedha, tunataka mikopo, lakini hatuna nidhamu ya hizo fedha. Kwa hiyo, tufundishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna programu nyingi, ninakumbuka Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania ina programu kabisa ya elimu ya fedha. Kwa hiyo, ni vizuri sana vijana wetu wafundishwe nidhamu ya fedha, kuweka akiba, kuwekeza na fedha izae ilete matokeo chanya katika shughuli ambazo anazifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vitu muhimu sana tukiweza kufanya, hata Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao sasa umehuishwa vizuri na unatoa mikopo, utaendelea kushamiri kama vijana wetu watakuwa na nidhamu ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)