Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yumna Mmanga Omar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YUMNA MMANGA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima na kutujaalia sote tukiwa hapa leo tukiendelea na majukumu yetu ya kikatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na vijana wenzangu kwa kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuanzisha Wizara hizi ambazo zinagusa mahsusi maendeleo ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, na mimi niende moja kwa moja katika hoja iliyopo Mezani. Wakati ninasoma hotuba hii ya Waziri, nimeona kwamba ameomba shilingi milioni 35 kwa ajili ya utekelezaji wake wa mwaka 2026/2027, lakini 83% ya fedha hizi zinakwenda kwenye uendeshaji ikiwemo mishahara na OC na 17% zinakwenda kwenye uwezeshaji wa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu ni kwamba, kama Wabunge wenzangu waliotangulia kusema, fedha hizi shilingi bilioni 200 ambazo zimetolewa kwa maendeleo ya vijana zingeletwa kwenye Wizara hii zikaweza kuratibiwa vizuri. Kuzipeleka kwenye Wizara nyingine, inasababisha fragmentation ya activities, ujasiriamali na kupelekea kutokupimwa, ufanisi wa upimaji wa matokeo wa hizi fedha kuwa ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia inclusivity ya uwezeshaji inaweza kupungua kwa sababu tunatambua Wizara hizi za sekta ziko zaidi katika uzalishaji, siyo uwezeshaji wa vijana, na sisi vijana wa Kitanzania tunataka kuwezeshwa na siyo kuendeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, niseme tu kwamba, moja ya malengo la Wizara hii ni kuongeza kuhamasisha vijana kushiriki kwenye nafasi za uongozi kuanzia ngazi za Taifa hadi kata. Hii ameanza kumdhihirisha Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia Baraza lake la Mawaziri, humu ndani ya Bunge, pamoja na maeneo mengine ndani ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu hii imezindua kamati ya utekelezaji wa kusimamia programu za uwezeshaji wa vijana ikiwemo Hub Challenge na Idea Kitaa. Kamati ile haina uwakilishi wa vijana wenye ulemavu. Hatulilii uwakilishi, tunalilia meaningful participation, kwa sababu ni sisi ndio tunatambua pilipili inatuwasha kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sisi ndio tunatambua kiatu kinatubana kwa namna gani? Ni sisi tunatambua changamoto zetu na namna gani ya kwenda kuzitatua. Kwa maana hiyo, basi hata ile fomu ya maombi ya kwenye programu hii, inapokosa kipengele cha ulemavu, ni kipengele kidogo, lakini impact yake ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kukosekana kwa kipengele hiki, tunaweza kukosa takwimu sahihi ni vijana wangapi wenye ulemavu wamefikiwa na taarifa ya fursa hii? Ni vijana wangapi wenye ulemavu ambao wameomba fursa hii? Ni vijana wangapi wenye ulemavu wamepatiwa fursa hii? ni vijana wenye ulemavu wa aina gani wamepata fursa hii? Vivyo hivyo, kutokana na ukosefu wa takwimu hizi tunashindwa kupima matokeo halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ulimwengu wa sasa ambao ni data driven decision making, ukitutoa kwenye nafasi ya maamuzi, maana yake umekusudia kwa madhumuni mazima kutoa kwenye matokeo. Hivyo basi, ninaiomba Wizara ikaangalie namna inavyokwenda kutushirikisha sisi vijana wenye ulemavu kwenye nafasi hizi, na pia nafasi ya kurekebisha ile fomu kwa matokeo mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara imeanzisha makongamano mbalimbali ambayo yanakutanisha vijana sehemu mbalimbali kujadili fursa na changamoto. Makongamano haya ni kwa namna gani yanajumuisha vijana wenye ulemavu in terms of miundombinu na kufikiwa na taarifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya makongamano mijini na vijijini, ni lazima tuhakikishe tunaweka mazingira ya kwenye kivuli, yaani miundombinu rafiki ili vijana wenye ulemavu wa viungo waweze kufika, na pia wakalimani wa lugha ya alama ili ndugu zetu wenye ulemavu wa uziwi waweze kupata taarifa na kunufaika na fursa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni mapendekezo yangu kwa Wizara kuona ni namna gani wanaweka jitihada za makusudi za kuweza kuhakikisha kuwa nasi vijana wenye ulemavu tunatufaika kwa 100% kwenye fursa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukaweka specific intervention. Kama ni mashindano, tunaweka mahususi kwa vijana wenye ulemavu; na yapo yanaendelea. Tarehe 7 Machi, nimehudhuria Programu ya Wazo Bora, Pitch Programme, ambayo vijana wenye ulemavu wameshindanishwa mawazo yao, ideas zao za ubunifu na washindi watatu walipewa zawadi. Shindano hili lilianzishwa na Standard Chartered Bank wakishirikiana na Side Saver Organization. Taasisi hizi zipo, na sisi kama Serikali tuna nafasi kubwa ya kutekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawasilisha hoja na ninakubaliana nayo. (Makofi)