Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimesoma randama vizuri, nimesoma sheria zinazoendana na jambo hili, na nimesoma matoleo tofauti tofauti na nimeona sasa niishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika randama ya Fungu 104 katika page ya nne ambayo wameelezea dira na dhima; dira inasema kuwa na vijana wenye ujuzi, halafu yanaendelea mengine. Dhima inasema, kuweka mfumo wa ufanisi wa kitaasisi, lakini mwisho wakataja kwamba, kuwapa vijana ujuzi husika. Sasa lengo langu mimi nililokusudia kuzungumza, ninataka kuzungumzia kukuza ujuzi wa vijana kwa ajili ya kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vitu vyote, pamoja na ile ya Waziri Mkuu ambayo inashughulikia kazi, ajira na mahusiano, nimeona kwamba kuna upungufu katika Wizara hii. Upungufu wenyewe Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameutambua na ameutaja page ambayo ameeleza katika hotuba yake. Tukiacha idara au kitengo cha kukuza ujuzi kwa ajili ya kupata ajira, hapo ndipo tumewaacha vijana, maana hakimo katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama, utakuja kukuta katika core functions zake ni uratibu na uhamasishaji wa vijana, elimu ya uraia na uzalendo na uratibu wa mwenge, ukuzaji biashara na uwezeshaji vijana kiuchumi; na nyingine ustawi wa makuzi ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lalamiko letu kubwa lilikuwa ni ajira kwa vijana, na ajira huwezi kupata bila ujuzi. Kama huna ujuzi, ajira huna, na hiyo amesema mwenyewe Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 10 paragraph ya 13 alipotoa takwimu za kwamba vijana ni milioni 20.6 kati ya waajiriwa walioajriwa milioni 26. Vijana wa kutoka miaka 15 mpaka 35 wako milioni 20.6, ukitazama, wengine ni milioni sita. Maana yake ni kwamba vijana wanahitaji wawezeshwe zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisema kwamba kuna ukosefu mkubwa wa ujuzi kwa vijana, kwamba hii ni changamoto. Pia akesema kwamba ujuzi wenyewe ni ambao unaendana na soko. Kwa maana hiyo, kazi ya Wizara hii sasa watuletee ujuzi unaoendana na soko, hatutaki waratibu wafanye wao. Kwa nini wasifanye wao? Farasi huyu ni wake mwenyewe Mheshimiwa Waziri, anakaaje mkiani? Vijana na ajira ni wake. Hilo ndilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama changu kimeahidi katika Ilani kuwapatia ajira watu 8,500,000. Kutoa ajira hizo anafanya kama anamnyooshea kidole mtu yuko Uingereza, yeye yuko Tanzania. Anampandisha mtu shetani wa Uingereza kwa kunyoosha kidole, anampataje? Achukue hiki kitengo kiwepo kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo hiki ni muhimu, kwa sababu ukitazama hivi vitengo vyote nilivyovitaja, investment yake ni shilingi 5,383,000,000, kitu kama hicho; lakini akichukua hiki cha kukuza ujuzi kwa vijana investment yake ni shilingi bilioni 9.7, takriban mara mbili zaidi; ni zaidi ya 200%. Kitengo hiki akikiacha ina maana kwamba tutakwenda tofauti na dira. Dira yetu inatutaka kuwafanya vijana wawe na ujuzi ili uchumi tuliou-target tuweze kuufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nizungumzie kitu kimoja. Ni kwa nini kukawekwa programu ya kukuza ujuzi? ATE (Association of Tanzania Employers) walikaa wakakubaliana na Serikali, kwamba iwepo Skills Development Levy, ichajiwe kwa ajili ya kukuza ujuzi, na hii one third itakwenda kwenye kukuza ujuzi na vingine vitakwenda katika elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa makubaliano hayo ATE wao watapewa gap ya skills ambayo ipo na Serikali i-finance kupitia Skills Development Levy kuwasomesha watu ili tupate ujuzi unaotakiwa, maana kama kiwanda kimekosa ujuzi, ina maana tuna-import labour. Sasa ili tusi-import labou,r tuwape ujuzi vijana wetu. Tutakapowapa ujuzi, hapo ndipo tutakapozifanya hizi kazi wenyewe. Vinginevyo hatutaweza kupata ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, page number 15 ametaja hapa programu ya kukuza ujuzi ambayo inafanyika kule katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, kwamba, ukijumlisha namba zote tatu unapata; kwa mwaka 2025 waliofanyiwa huo ujuzi ni watu 16,000. Hii ni namba ndogo sana. Kwa nini, hili jambo asiwe nalo yeye? Akiwa nalo yeye anaweza akalifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa rai, kwa kuwa tozo hii imewekwa, tuipeleke. Kama hatujaipeleka, ina maana kwamba tutakosa kuwapatia vijana wetu ujuzi na tutakosa kuwapa vijana ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza kitu kimoja, nini maana ya kukuza ujuzi? Kukuza ujuzi maana yake ni kwamba vile gap zilizokuwa zimepatikana viwandani wapatikane wataalamu wasomeshwe. Wakishasomeshwa, zile kazi tunakaa sisi wenyewe. Kama kazi hizi hatujakaa sisi wenyewe, ina maana moja kwa moja tunapoteza, na ajira hizo tunazipeleka kwa watu wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie juu ya vijana. Watu wengi wanazungumza falsafa za kuhusiana na vijana. Kuhusiana na vijana, mimi nina falsafa moja. Nabii Musa, watu wote wanamjua; katika Biblia, ni Musa. Katika Quran, Mungu anasema, “Famaaa aamana li-Moosaaa illaa zurriyyatum”, hawajamwamini watu wote Musa isipokuwa vijana ndio walimwamini. Musa alishinda na vijana, na nchi hii tutashinda tukiwakamata vijana, maana kila mwenye lake analitupa kwa vijana, lakini sisi tunaweza tukawatumia vijana wetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kitu kimoja kwa kumalizia ili niweze kuunga mkono hoja. Mimi ninasema, “Tanzania ndipo kwetu, hatuna kwingine katu, Asitudanganye mtu, kujenga wajibu wetu, kwa nguvu na jasho letu, tuishi kama wenzetu.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kitengo cha kukuza ujuzi kiwepo kwa Mheshimiwa Waziri wa Vijana, hapo ndiyo atakuwa ana Wizara kamili. Kama anaratibu, akiratibu kwa mbali hawezi kuratibu hivyo. Wengine wanaweza wakaratibu, na wana sekta. Kilimo wana sekta, uvuvi wana sekta, sasa wanaenda kumratibu Waziri Mkuu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tutizame, unaenda kumratibu Waziri Mkuu? Sasa hili ninaona halijakaa vizuri. Hiki kitengo kichukuliwe, kwa sababu Wizara zote hata kama TAMISEMI, whether itawekwa Ofisi ya Rais au itawekwa kwa Waziri Mkuu. Sasa hii ipo kwa Waziri Mkuu, unaenda kuiratibu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda Mheshimiwa Waziri atoe ufafanuzi juu ya hili. Ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja.