Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa heshima ya kuwa mchangiaji wa Wizara hii muhimu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitaanza kwa kusoma Kitabu cha Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro, mstari wa tano anasema: “Vivyo hivyo ninyi vijana watiini wazee, naam ninyi nyote jifungeni unyenyekevu mpate kuhudumia kwa sababu Mungu huwapinga wote wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyevu neema yake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu niseme nimesoma fungu hili nikiwa nimeanza na neno la bwana nikiamini kabisa ya kwamba kwanza Mungu wetu ni Mungu wa Majeshi, Mungu wetu ni Mungu wa Majeshi na nimesoma fungu hili kwanza nikimtanguliza Mungu katika bajeti hii muhimu sana katika masuala mazima ya ulinzi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba mimi nimekuwa Serikalini maisha yangu yote toka nimemaliza chuo, nimefanya kazi Serikalini na Mheshimiwa Jafo ametoka kuzungumza hapa ni Mjumbe mwenzangu kwenye Kamati hii na uzuri Mheshimiwa Jafo pia nimefanyanae kazi nikiwa kama Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe miaka hiyo ya nyuma kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa dhati ya moyo wangu Jeshi letu la Wananchi kwa kiwango kikubwa tungeweza kusema katika bajeti hii Wabunge wote kwa uzalendo ambao Jeshi letu limeendelea kuonesha kwa nchi yetu ninaweza nikasema kabisa na wanajeshi wote wanaotusikiliza sisi Wabunge na viongozi wa Jeshi wote walioko hapa wakiongozwa na Waziri wetu kaka yangu mnyenyekevu sana ambaye fungu hili pia linamuhusu, kitendo cha kuona Wabunge, Bunge hili wanawasemea vizuri wanajeshi ni kwa sababu kubwa moja na ninaomba m-note na siku mkiondoka kwenye misingi hiyo mnaweza msizione sauti za Wabunge na Watanzania wakionesha mapenzi mema kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka niwaambie mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Nimemfahamu Waziri huyu Mheshimiwa Dkt. Nyansaho toka akiwa mtumishi wa umma pale Benki ya Azania, nataka tuweke rekodi sawa na fungu la unyenyevu nililolisoma linabeba maudhui ya Waziri wetu huyu wa Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna jambo ambalo Mungu analithamini sana katika leadership ya mwanadamu, cha kwanza Mungu anachokithamini sana kwa binadamu it’s humbleness, unyenyekevu na unyenyekevu huu wa Waziri wetu ameurithi kutoka kwa unyenyevu wa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamsema Waziri huyu utakumbuka mimi nimefanya kazi katika shirika la umma linaitwa Fair Competition Commission nikiwa kama inspector, lakini nikiwa kama Senior Human Resource Officer. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie wakati nafanya kazi Fair Competition nilifanya kazi kwa karibu na Mheshimiwa Dkt. Nyansaho, Waziri huyu alipokwenda pale TANESCO kama Mwenyekiti wa Bodi nchi yetu ilikuwa inapita katika misukosuko mingi sana ya kukatika umeme, nenda-rudi, lakini kwa unyenyevu wake aliacha alama, akaondoka ameacha alama, Taifa letu likawa limetulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Rais wetu amempa heshima Waziri huyu amekuja kwenye Wizara hii ya Ulinzi tunaona utulivu, nidhamu ya Jeshi letu vikiendelea kushamiri katika Taifa letu. Mheshimiwa Waziri, mimi kaka yako na mpakwa mafuta wa bwana ninakutia moyo, endelea na unyenyevu huo kwa sababu ahadi ya unyenyekevu iko katika neno la bwana ambalo nimekusomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitie moyo Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania katika bajeti hii sisi tumepita tumeangalia miradi. Kwanza kabisa nataka niwaambie Mkuu wa Majeshi nafikiri uko hapa ndani, wewe na Katibu wako Mkuu kaka yangu ambaye ametajwa kwa sifa nyingi na majenerali wote walioko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti nataka nikwambie uzalendo wa Jeshi letu katika kulinda tunu za amani na kulinda Katiba unawafanya Watanzania waendelee kulipenda Jeshi hili na kulisemea bila aibu mahali popote. Ninataka nikwambie nidhamu iliyooneshwa na Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu lilipokuwa linapita katika nyakati ngumu, Taifa letu wakati linapita katika nyakati za kujaribiwa, kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusimama katika kutii mamlaka ya nchi na kulinda mipaka na uhuru wa Taifa letu sisi Wabunge tuliotumwa na wananchi kuja katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa dhati ya moyo wetu tunasema nembo ya Uhuru wa Taifa letu ni uadilifu ni pamoja na uadilifu wa kazi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jenerali Mkunda na majenerali wako wote, kwa niaba ya Wabunge wenzangu na Wajumbe wa Kamati ambao sisi tunawasimamia kwa dhati ya moyo wangu Mungu wa Isaka, Ibrahim na Yacobo aendelee kuwaimarisha muendelee kulinda tunu za amani, mshikamano na umoja wa Taifa letu, kwa sababu ninyi mmekuwa chachu ya kukataa chokochoko za mapandikizi yote ambazo zinataka kuvuruga umoja, amani na mshikamo wa Taifa langu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua hata Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia nilisikiliza hotuba zake nyingi aliendelea kulisisitiza jeshi letu muendelee kulinda nidhamu ya hali ya juu, kwa sababu toka historia ya Taifa hili lilivyopata uhuru, mataifa mawili yalipoungana nchi yetu imeendelea kuamini katika mambo ya kwamba uongozi wa Taifa letu ukishapewa ridhaa, hakuna kuangalia mipaka huyu ametoka Ruvuma, huyu ametoka Zanzibar, huyu ametoka Bara, Taifa hili ni moja, kila kiongozi anapopata ridhaa ya kuongoza Taifa hili, sisi kama Watanzania tunajukumu na wajibu wa kumuunga mkono, ndivyo mlivyofanya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kwa sababu bajeti hii sina mengi ya kusema, neno langu la mwisho ninalotaka kuwaomba, endeleeni kuwa wazalendo kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia, endeleeni kuwa wazalendo kwa Amiri Jeshi Mkuu na Rais wetu, na endeleeni kulinda uhuru na mipaka ya Taifa letu. Sisi Wabunge tulioko hapa tutaendelea kuwasemea, tutaendelea kuwaunga mkono, na tutaendelea kuwa mabalozi wenu wema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibidi bajeti hii tuipitishe tu leo mchana, watu hawa wakaendelee kujenga Taifa na kulinda uhuru wa Taifa letu. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja kwa 100%. (Makofi)