Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze nami kutoa mchango wangu kwa Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, ambaye kwa uwezo wake ametuwezesha kuiona leo, siku hii iitwayo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninachukua fursa hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Tabora ambao wameendelea kuniamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee ninatoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi nyingi kwa Waziri Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho na Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe na watumishi wote wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Vilevile, pongezi kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda na wasaidizi wake wote wakiwemo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele na wasaidizi wake wote, wakiwemo Wakuu wa Taasisi za Mzinga, SUMA-JKT, Nyumbu na wakuu wa vikosi mbalimbali, makamanda na askari wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninawapongeza watumishi na makamanda wote wa Fungu 38, Fungu 39 pamoja na Fungu 57 la Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ni ukweli usiofichika jeshi letu linafanya kazi kubwa sana, sana, sana. Ninawiwa kuwashauri, kuwasihi na kuwashawishi. Kwa umoja wetu tuipitishe bajeti hii iliyowasilishwa katika Bunge hili Tukufu, ili kazi nzuri ya utekelezaji wa bajeti iliyofanywa na inayofanywa, sisi wote ni mashahidi, tunashuhudia kazi nzuri ambazo zinafanywa na Wizara hii na majeshi yetu na makamanda wetu. Kazi hizi ziendelee kufanyika katika nchi yetu, kwani ulinzi ndiyo kichocheo cha ukuaji wa uchumi, ulinzi ndiyo kichocheo pia cha shughuli za kijamii, lakini ulinzi ndiyo kichocheo cha kufikia malengo ya Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kwa kipindi kirefu imekuwa ni kisima cha amani na utulivu, Afrika na dunia, hii ni kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na Majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama nchini. Kuna watu wanakesha sisi tunalala, tunapata usingizi mnono. Kuna watu wanafanya kazi kubwa za kulinda mipaka yetu ya nchi kavu, ya anga na majini ili Taifa letu liendelee kuwa salama. Tunalipongeza sana jeshi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi kubwa ambazo zinafanywa na Jeshi letu na bidii, na nidhamu, na uhodari walionao wanajeshi wetu, sisi tumeshuhudia miradi ikitekelezwa kwa vizuri sana. Miradi ambayo tumetembelea sisi Wanakamati nikiwa ni sehemu ya Kamati, ninaunga mkono taarifa yote iliyotolewa na Mwenyekiti wetu wa Kamati. Kazi nzuri tumeziona zikitekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali yetu ya Shirika la Mzinga iliyopo Morogoro, nami ninatumia nafasi hii kuwaambia wananchi waitumie hospitali hii. Serikali imewekeza fedha nyingi ili kuboresha huduma katika hospitali hii iliyipo pale Mzinga, Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi waliopo pale wanafanya kazi nyingi kwa weledi, kwa kujituma, na kwa nidhamu ya hali ya juu. Hatuna shaka na Jeshi letu, hatuna shaka na watumishi wote wa Wizara, hatuna shaka na makamanda wetu. Tuna kila sababu ya kuipitisha bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Majeshi yetu na askari wetu, tunaishauri Serikali na tunaipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuendelea kutoa kipaumbele kwa bajeti kwa Wizara hii kwa kutenga na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinapatikana ili kuendelea kuboresha ufanisi na utendaji wa Wizara na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri tu kwa uchache yafuatayo; kwanza, tunaiomba Serikali iendelee kutoa fedha. Upatikanaji wa fedha za maendeleo ukifanyika kwa wakati na kwa viwango husika, na kwa stahiki ambazo zinahitajika, kwani mchango mkubwa unaofikiwa, unaofanywa na Jeshi letu ni mkubwa. Tunaiomba Serikali yetu iendelee kutoa fedha za maendeleo jinsi ambavyo zinavyohitajika na kwa wakati na kwa muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuongezwa kwa fursa za vijana wa kujiunga na mafunzo ya JKT. Tunahitaji vijana wetu wengi waendelee kupata mafunzo ya ukakamavu, wapate kuwajengea umoja wa Kitaifa, lakini wapate stadi za maisha na kazi ambazo zitawasaidia kujiajiri wanapomaliza mafunzo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na jeshi ufanyike kwa uharaka bila ucheleweshaji. Ninachukua fursa hii kuishukuru Serikali ambayo kwa namna ya pekee imeweza kulipa fidia wananchi wa Mbogwe waliopo Nzega Mkoa wa Tabora, jumla ya shilingi 4,869,631,375. Jumla ya wananchi 989 wameweza kulipwa fidia zao. Hongera sana kwa Wizara yetu ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, pale inapowezekana, vijana wetu waendelee kupewa mafunzo ya kutengeneza teknolojia ya vifaa vya nishati safi, ikiwemo mitambo ya biogas, majiko banifu, majiko ya umeme na gesi ili yaweze kutumika nchini na kulinda mazingira yetu, kuinua uchumi na kulinda afya za watumiaji. Ni wakati sahihi sasa vijana wetu tunapoenda kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia, vijana wetu wafundishwe teknolojia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninaendelea kulipongeza jeshi letu na tunaendelea kuwatia moyo askari wetu na tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwatunza na kuwalinda. Aendelee kuibariki nchi yetu ikiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)