Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi. Ninachukua fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima, lakini kwa namna ya kipekee kabisa ninachukua fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa tunampongeza Mheshimiwa Rais, mwaka huu Februari kwa kuzindua Makao Makuu ya Usalama wa Taifa, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viongozi wetu na wafanyakazi na taasisi za Wizara hii wanakuwa na mazingira bora ya kiutendaji na ya kufanyia kazi kwa ufanisi. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu mradi ule wa makao makuu umeweza kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 120. Haya ni maendeleo makubwa sana ndani ya Wizara hii. Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutuamini vijana na kutupa nafasi za juu kabisa za uongozi wa Taifa letu. Leo tunashuhudia kwenye historia ya Wizara hii tumepata Waziri kijana, mnyenyekevu, mchapa kazi, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho ambaye huyu ni mbobezi na mzamivu wa masuala ya uchumi. Tunampongeza sana kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge, lakini pia kuwa Waziri wa Wizara hii ya Ulinzi. Hakika anaitendea haki Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kama Mjumbe wa Kamati ninataka niwaambie Wabunge wenzangu, mara ya kwanza Mheshimiwa Waziri alipokuja kwenye Kamati alikuwa anaweza kuitafsiri Wizara hii kichwani mwake bila kusoma popote. Kwa hiyo, tumeona kabisa jicho la mama limemwona huyu kijana mwenzetu, mchapakazi, mnyenyekevu, na ninaamini kwa weledi aliokuwa nao, na kwa namna anavyoishi na watu, na uwezo wa kusikiliza na kupambanua mambo, hakika atafika mbali. Tunamwombea sana kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara hii, yeye ndiyo encyclopedia ya Wizara hii. Kijana mnyenyekevu, mchapakazi, kwa kweli anafanya kazi kubwa sana na kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya kipekee ninaomba tumpongeze sana Mkuu wa Majeshi yetu, CDF Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Kamandi zote za vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kuifanya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.
Mheshimiwa Spika, pia bila ya kumsahau mnadhimu wa jeshi ndugu yetu luteni jenerali Salum Haji Othumani, wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana kumsaidia CDF, tunakupongeza sana, lakini pia tunampongeza Mkuu wetu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele pamoja na Mkuu wa SUMA-JKT wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana, tunawapongezeni sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo tunaomba tuwatie moyo wanajeshi wote na vikosi vyote vya usalama, kwamba kazi wanayoifanya ya kulinda amani na usalama wa nchi yetu, sisi kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawapongeza sana na tunawatia moyo na tunathamini kwamba sisi muda tukiwa tunalala wao wapo macho kupambania usalama wa Taifa letu. Tunawapongezeni sana na Mwenyezi Mungu azidi kuwalinda na kuwabariki kwa kuendelea kuimarisha usalama wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba nitume salamu kwa Wizara ya Fedha. Suala la amani halina compromise, tunaweza ku-compromise mambo mengine yote, lakini siyo suala la usalama wan chi yetu. Ninaiomba sana Wizara ya Fedha itusaidie kwenye suala zima la kutoa bajeti ya kutosha kwenye Wizara hii ili Wizara hii waendelee kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano Fungu 57 la Wizara, fedha ambazo zimetoka ni 43.6% lakini pia kwenye fedha za miradi ya maendeleo, kwenye fedha shilingi bilioni 318, fedha zilizotoka ni shilingi bilioni 110 sawa na 34.6%, lakini pia Shirika la Nyumbu fedha ambazo zimetoka ni 32%, Shirika la Mzinga fedha zilizotoka ni 33%.
Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Wizara ya Fedha, kuhakikisha kwamba wanatoa fedha hizi ili taasisi hizi zilizopo chini ya Wizara ziweze kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu sana, kwa sababu bila ya kuwawezesha, maana yake tunawafanya wafanye kazi katika mazingira magumu ya kulinda amani na usalama wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, la pili, niipongeze sana JKT (Jeshi la Kujenga Taifa), wamefanya kazi kubwa na kazi nzuri sana na kupitia SUMA-JKT mwaka huu tumeona wametoa gaio la shilingi bilioni moja kwenye Mfuko wa Hazina, haya ni mafanikio makubwa sana na mimi niungane na Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Fadhili Liwaka, kuwaomba sana waone uwezekano wa vijana wetu wanaohitimu kidato cha sita kuhakikisha kwamba hawa vijana wanapata fursa ya kwenda kupata mafunzo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi capacity ya JKT wanauwezo wa kuchukua vijana 60,000 lakini vijana wanaohitimu kidato cha sita ni 125,000. Niiombe sana Wizara ya Fedha iwape ushirikiano wenzetu wa Wizara ya Ulinzi kupitia JKT, kwa sababu tunaandaa Taifa la kesho na bila kuwaandaa vijana ambao ni wazalendo, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, hatuwezi kupata matokeo tunayoyatarajia. Ninajua mpango wa Wizara ni kuhakikisha mpaka ifikapo mwaka 2031 wanaweza kuwa na capacity ya vijana 120,000; lakini niwaombe Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kupitia SUMA-JKT wauone uwezekano wa kimkakati kabisa kuwezesha hili shirika letu la SUMA-JKT kuweza kufanya miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaona SUMA-JKT wanafanya shughuli za ulinzi kwenye makampuni mbalimbali na kwenye miradi ya kimkakati ikiwemo SGR, wanafanya kazi kubwa sana kwenye Bwawa la Hydropower la Mwalimu Julius Nyerere, wanafanya kazi nzuri sana kwenye miradi ya kimkakati. Tunaomba sana pamoja na hii kazi nzuri wanayoifanya kwenye ulinzi, lakini pia kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali tuone uwezekano wa kutanua wigo kwenye sekta za kimkakati kwa mfano uwezekano wa kuwa na kongani za viwanda, lakini pia kwenye sekta ya madini ili tuendelee kulinda rasilimali za Taifa letu lakini kupitia wao tuweze kupata fedha zakuwezesha JKT iweze kuendesha mafunzo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tunatambua sasa hivi kupitia JKT kuna skimu mbalimbali za umwagiliaji kama pale Chita kuna skimu ya umwagiliaji. Pale Chita tuna hekari 12,000 lakini tuna kilimo cha umwagiliaji hekari 2,500. Niiombe sana Wizara ya Kilimo...
(hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Spika, niiombe sana Wizara ya Kilimo iweze kuwa-support wenzetu...
SPIKA: Nikuombe ...
MHE. ZAINAB ABDALLAH ISSA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante sana.