Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye sekta hii muhimu sana katika uchumi wa Taifa letu, ambayo ni Sekta ya Nishati. Ninaendelea pia kuipongeza sana Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo kwa ujasiri na uthabiti mkubwa, amejitoa kikweli kweli kabisa kuona kwamba, tunakuwa na mageuzi katika Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nchi yetu inaenda katika uchumi wa kati, uchumi wa viwanda. Ni uchumi ambao unahitaji sana sekta ya nishati kuwa imara, ndiyo hapo kwa hakika tutaweza kufika katika uchumi wa kati wa daraja la juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana Wizara ya Nishati kwa kweli, wameleta mageuzi makubwa kweli kweli, kwenye sekta hii ya umeme. Ndugu zangu tukitaka kujua kwamba, hao watu wamefanya kazi kubwa hebu tuangalie tumetoka wapi, tuko wapi na then tuweze ku-project kuona kwamba, hao watu wanataka kutupeleka wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka mpaka mwaka 2007, takribani miaka 43 toka TANESCO imeanza, Mheshimiwa Prof. Muhongo amesema TANESCO imeanza mwaka 1964; nchi hii vijiji vyenye umeme vilikuwa 506 tu sawa na 4.1% ya vijiji vyote 12,318. Leo hii tunavyoongea vijiji vyote 12,318 tayari vina umeme na zaidi ya 61% ya vitongoji vyote 64,359 vina umeme. Leo tunaona mabadiliko makubwa ya kiuchumi na vilevile ya kijamii kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakati tukiwa shuleni, nimesoma hapa Dodoma, tulikuwa tunasoma kwa kutumia vibatari, tena vibatari vyenyewe vya made by mimi, leo hii mpaka kule vijijini hawa vijana wetu wanasoma kwa kutumia umeme wa TANESCO. Kwa kweli, ni jambo ambalo inabidi tuwapongeze sana na huu umeme vijijini tunaona umeleta mabadiliko makubwa. Leo hii vijana wana shughuli za kiuchumi wanaziendesha kulekule vijijini, tunawapongeza sana kwa kazi kubwa hii mliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke inawezekana miaka miwili, mitatu, hapo nyuma nikisema kero ninaona labda, kama hili neno ni dogo, tulikuwa na janga kubwa sana ndugu zangu Watanzania. Tulikuwa na kitu kinachoitwa mgao wa umeme, mgao wa umeme umetusumbua sana. Ulifanya hata uzalishaji wetu ukawa na changamoto nyingi kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyote vilijiendesha kwa shida na kufanya gharama za uendeshaji kuwa kubwa kwa sababu, walikuwa wanatumia umeme wa majenereta yanayoendeshwa kwa dizeli. Changamoto tulizopata zilikuwa ni kero kubwa kweli kweli, lakini leo hii ndugu zangu, binadamu tumeumbwa yale mambo mabaya huwa tunayasahau, habari ya mgao wa umeme tumeanza kuisahau tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tutakumbuka kwamba, uunganishaji wa umeme miaka mitano, mingapi kule nyuma, ilikuwa ni changamoto kubwa kwelikweli. Unakuta mwananchi amejenga nyumba yake vizuri, lakini kuunganisha umeme ilikuwa ni kazi, afadhali hata kujenga nyumba kuliko kuunganisha umeme; unaomba umeme inachukua miezi sita mpaka mwaka mzima bado hujaunganisha umeme. Leo hii ndani ya siku 10 mpaka 30 ukishaomba unaunganishiwa umeme, sisi wote hapa ni mashahidi. Haya ni mageuzi makubwa na ni mabadiliko makubwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, hata kazi za dharura unaenda kuripoti; miaka mitano iliyopita kule nyuma, unaripoti hapa kwangu, kwenye bomba kuna cheche zinatoka. Ilikuwa inachukua saa 24 mpaka 48 na wakati mwingine uzalendo unakutoka, unawatafuta vishoka wanakuja wanagongagonga pale, ili kuondoa tatizo uweze kuendelea na maisha, lakini leo hii ukiripoti ndani ya saa nne, sisi wote hapa ni mashahidi, tayari unaona vijana wamefika wamefanya kazi yako, maisha yanaendelea. Kwa kweli, ni jambo ambalo linahitaji kupongezwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tunajua TANESCO ilikotoka, walikuwa wanajiendesha kwa hasara, lakini mpaka hivi sasa TANESCO wanaenda kwa faida, tumeona wamerekodi faida ya takribani shilingi bilioni 500, jamani, hayo ni mageuzi makubwa, ndiyo. Waheshimiwa Mawaziri wanastahili pongezi na washikilie palepale kuona kwamba, Watanzania wanazidi kusonga mbele. Kubwa kabisa ndugu zangu Watanzania tusingependa sasa kuona tunarudi kule tulikotoka, tuhakikishe kwamba, haya mafanikio tuliyoyafikia tunayasimamia vizuri, ili kuona kwamba, haturudi tena kwenye mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kusudi tusiweze kurudi kwenye mgao wa umeme tuhakikishe kwamba, Serikali inaendelea kufanya uwekezaji wa uhakika na hususani, kwanza kwenye matengenezo ya mitambo tuliyonayo. Lazima tuhakikishe kwamba, matengenezo yetu yanatengenezwa kulingana na specifications ambazo wataalam wametuwekea. Tukikosa hapo kuna uwezekano tukarudi kule nyuma, kitu ambacho kwa kweli, kitakuwa hakifai na hatutarajii kabisa kuona tunarudi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Mheshimiwa Profesa Muhongo amesema tuendelee katika uzalishaji wa umeme na sina sababu ya kurudia kwa sababu, Profesa ameeleza vizuri kwelikweli, lakini tuhakikishe kwamba, hizi megawatt 4,000, katika Taifa la Watanzania zaidi ya milioni 60 bado hazitoshi. Hata hizo megawatt 8000 kufika mwaka 2030 juhudi iendelee, bado haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameelezea mambo ya energy per capital. Energy per capital wenzetu wako mbali, sisi leo hii bado tuko chini ya kilowatt 300 kwa kila Mtanzania, ni kidogo sana hiyo. Kwa hiyo, tuhakikishe uzalishaji wetu unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, ninarudi sasa upande upande wa REA. Ninaungana na wenzangu wote kupongeza sana taasisi yetu ya REA kwa kweli, wameendelea kufanya kazi nzuri. Leo hii tunaongelea kwamba, vijiji vyote 12,318 vimekwisha, 61% ya vitongoji vyote 64,359 vimekwisha na bado tunaendelea, kufikia mwaka 2030 tutakuwa na 100%, lakini hili linaweza vilevile likatu-take by surprise tukasema kwamba, labda yawezekana kazi ya REA inakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kama ni kazi ya REA sasa ndiyo inaanza kwa sababu, wahenga wetu walituambia, walitufundisha kwamba, kuzaa mtoto siyo kazi, kazi kubwa ni kumlea. REA wametuzalia mtoto; sasa je, huyu mtoto apate kwashakoo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaangalia katika kipindi hiki kifupi katika ule mtandao wa umeme wa msongo wa kilovoti 33 ambao TANESCO wanaumiliki, takriban kilomita 80,000 REA wamechangia zaidi ya kilomita 38,000. Huu mtandao si kitu chepesi ni kitu kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeona njia za umeme za three phases zimekuwa ni kubwa sana. Mradi wa gridi imara tunaomba kwa kweli, usimamiwe kwa nguvu zote kwa sababu, kweli pamoja na mambo mazuri haya, lakini bado kuna changamoto ya kukatika kwa umeme kwa sababu, mtandao wa three phases umekuwa mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuwa na mtandao wa kilomita 80,000 na kwa REA pekee yake 38,000 kwa kipindi kifupi hiki maana yake ni nini? Maana yake mtandao wa kilomita 38,000 ni zaidi ya nguzo 400,000 zimeweza kuingia kwenye system kwa muda huu mmoja. Maana yake ni kwamba, hizi nguzo zimetengenezwa kwa teknolojia moja, kwa spec moja. Maana yake ni kwamba, zitazeeka pamoja na kuna uwezekano zitakufa pamoja. Sasa ni lazima hilo tulione kwamba, ok, sasa tunaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yanaweza yakatokea majanga kwamba, leo umekaa hapo unasikia kwa watani zangu kule Pwani nguzo 800 zimeanguka, hujakaa sawa unaambiwa hapa Dodoma zimeanguka 600, hujakaa sawa unaambiwa kule Kagera zimeanguka 200. Hilo litakuwa ni janga, tuanze kuliangalia na kuona tunaenda namna gani na ndiyo maana nimesema kwamba, kama ni kazi ya REA, sasa kazi yake ndiyo inaanza. Hakika tufanye kila linalowezekana, kama kuna uwezekano tuwaongezee hata bajeti, ili waanze kazi ya kumlea huyu mtoto kusudi aweze kuwa na faida katika Taifa la Tanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Amosy William.

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)