Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, ninachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, ninachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, hasa katika kuiendesha nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nishati ninaweza kusema katika Mkoa wetu wa Mtwara tayari vijiji 785 vyote vina umeme. Sasa hivi vitongoji 2,798, kati ya vitongoji 3,421 tayari vimeshapata umeme na kazi inayoendelea ni kupeleka umeme katika vitongoji 555. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninapenda kujikita katika mambo machache. Mheshimiwa Profesa Muhongo, mwalimu wangu, ameongea kuhusu data na nitajitahidi kidogo kuzungumzia mambo mawili, matatu ya Mkoa wa Lindi na Mtwara. Jambo la kwanza ni suala la Gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu leo tuna miaka zaidi ya 65, lakini Mkoa wa Lindi na Mtwara haujaunganishwa na Gridi ya Taifa. Sisi Lindi na Mtwara kwa Miradi ya SONGAS, ambayo wakati inafanya kazi ilikuwa inazalisha zaidi ya megawatt 180 mpaka 190, lakini pia, gesi asilia inatoka Mtwara na hizo zote zinachangia katika Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai matumizi ya rasilimali za nchi hii ni ya watu wote, lakini mpaka leo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha bajeti yake kesho, ninaomba alete majawabu kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Ni lini wataunganishwa na Gridi ya Taifa, ambayo katika mikoa yote sasa hivi tumebaki sisi Lindi na Mtwara? Yaani wote wameunganishwa, bado sisi Lindi na Mtwara. Halafu sisi ndiyo tunatoa gesi nyingi, ambayo pia, inachangia katika Gridi yetu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai gesi ni rasilimali ya nchi yote, lakini sisi ambao tuna gesi ni muhimu pia, kupata vipaumbele hivyo. Kwa hiyo, sisi tunajua kuna mkandarasi anayejenga line kubwa, ambayo inatoa umeme kutoka Songea mpaka Masasi anaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 53. Ninaomba Mheshimiwa Waziri aje na majawabu ya lini sasa mkandarasi yule alitoka site? Je, kama yupo, tayari ameanza kazi? Kama hajaanza kazi, Mheshimiwa Waziri ni rafiki yangu, nitashikilia shilingi yake na shemeji yangu yupo pale ili anipe majawabu ya Lindi na Mtwara, lini sasa mradi mkubwa huu na hii mikoa miwili itaunganishwa katika Gridi ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kwenye REA, hesabu ni rahisi sana. Kwa hesabu ya kawaida, hapa katika Mkoa wa Mtwara kuna vijiji 77 katika huu mpango wa pili, yaani Home let Electrification Project 2B, Mkoa wa Mtwara una vijiji 77, Mkoa wa Lindi una vijiji 159, jumla kuu ukijumlisha hivi vijiji vyote unapata vitongoji 77 na vitongoji vya Lindi 159. In total ukijumlisha unapata vitongoji 555.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua tu kuchukua sample. Ukienda Ruvuma wenzetu vitongoji ambavyo vipo katika hii Hepic Two ambayo ni Home let Electrification Project 2B wana jumla ya vitongoji 634, ni zaidi ya vitongoji vyote vya Mtwara na Lindi. Nikachukua hesabu nyingine, Mkoa wa Mwanza wao wana jumla ya vitongoji 634, lakini jumla kuu ya Mtwara na Lindi ni vitongoji 555.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha bajeti yake aje na mpango kabambe wa kuongeza vitongoji katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, ili atuongezee tufikie vitongoji 700 ambapo sasa tutakuwa na 350 Lindi na 350 Mtwara, tutakuwa tumefanya kazi kubwa na tumepiga hatua kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumza Mradi wa Dharura wa Masasi - Newala. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hakika, mwaka huu tulikuwa na RCC, nilizungumza kuhusu shida ya umeme katika Jimbo la Newala na Mkoa mzima wa Mtwara. Mtwara unakatika umeme zaidi ya mara 20, leo Waziri alinipigia aliniambia siyo mara 20 nipunguze kidogo, lakini nikamwambia twende Newala tukakae mimi na yeye, akaniambia ni kweli unakatika sana, lakini hakutaka kukubaliana na mimi zaidi ya mara 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme, baada ya kelele zangu, kumbe Waheshimiwa Wabunge kupiga kelele inasaidia. Mheshimiwa Rais alisikia akaidhinisha 4.6 billion kujenga Mradi wa Dharura kutoka Masasi mpaka Newala. Nichukue nafasi hii, mimi ni mgumu wa kupongeza, lakini nimkupongeze Waziri, pia ninampongeza DG wa TANESCO. Hakika nilimwambia Waziri, asingeweza kukamilisha huu mradi leo hii, kama ningeikamata shilingi yake na mradi huu ukikamilika wananchi wa Newala wanaenda kupata umeme wa uhakika, tena umeme usio na matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunatumia umeme wa kilometa zaidi ya 1,850 kufika Newala. Maana yake utoke unakotoka Lindi, ufike Mtwara, ufike Nanyamba, ufike Tandahimba, unakuja Newala tayari. Shida ikitokea Nanyamba tayari wananchi wa Newala wanaenda kupata matatizo. Kwa hiyo, Waziri anapokuja kuhitimisha bajeti yako, aje na majawabu atuambie sasa huu mradi wetu wa dharura ambao alisema unakamilika Machi mwaka huu, je utakamilika lini ili wananchi wa Newala waweze kunufaika na mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo pia ningependa kuchangia ni Mradi wa LNG. Mradi wa LNG kila siku umekuwa kwenye maneno tu. Nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, wakati huo ndiyo gesi inatoka, haitoki, tulipambana sana na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alitoa shilingi 6,000,000,000 mwaka 2015 kulipa wananchi wa eneo la Likong'o.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa DC kipindi hicho na wakatuambia mradi huu utakuja kusainiwa ndani ya miezi minne au mitano ijayo. Ameondoka, amekuja Mheshimiwa Magufuli naye tukaambiwa mradi huu sasa unahitajika ufanyiwe marekebisho, review kubwa inatakiwa kufanyika, lakini tukae mkao wa kula, lakini wale wananchi wa Likong'o tayari tumeshawalipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amekuja mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanatuambia sasa tuko katika majadiliano ya mwisho. Sisi hatutaki kusikia majadiliano ya mwisho, watuambie wanasaini lini mkataba ule. Maana yake ni nini? Wenzetu wa Msumbiji wana matatizo makubwa sana, tayari wameshakamilisha kusaini, wameshasainiana mikataba ya dola 20,000,000,000 katika Mkoa wa Cabo Delgado, ambayo ni zaidi ya 50,000,000,000,000 katika Mkoa wa Cabo Delgado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu walikuwa na matatizo ya Al-Shabaab na nini na TotalEnergies tayari wameshaanza kazi wanaendelea na kazi pale. Sisi bado maendeleo, sisi mchakato unaendelea, sisi mchakato unaendelea, mchakato unaendelea, wenzetu wa Cabo Delgado, Msumbiji na Mtwara ni baba mmoja, mama mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa Waziri anapokuja kuhitimisha atuambie sasa huu Mradi wa LNG utaanza lini ili na sasa wenzetu wa Msumbiji wakianza kufanya kazi na sisi huku tuanze kufanya kazi ili tuwe na win-win situation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikwambie, huu Mradi wa LNG, ninafikiri wananchi wa Mtwara na Lindi hawataki tena kusikia haya maneno wanasaini, wanasema basi tumwachie Mwenyezi Mungu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuhitimisha, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)