Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Nishati. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa bajeti nzuri, bajeti ambayo imebeba taswira ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ukurasa Namba 16 kwenye maelezo ya chama inasema CCM inatambua kuwa umeme ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa shughuli za maendeleo ya kiuchumi. Kwa kuzingatia haya katika kipindi cha mwaka 2025 - 2030 itatendelea kuisimamia Serikali kuongeza kasi ya uzalishaji wa umeme na kuimarisha usambazaji wake, lengo ni kuona kuwa kila kaya inakuwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri, hii ndiyo bajeti ya kwanza tunashuhudia katika asilimia mia moja ya bajeti, asilimia 97.5 zinaenda kwenye maendeleo. Hakuna mpinzani wa nchi hii anaweza kupinga jambo kubwa kama hili ambalo Waziri anaonyesha kwa dhati na kwa dhamira ya moyo kwamba anaenda kuinua Taifa letu kwenye suala la umeme. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na tunaamini kwamba hata walioko nje, vijana wenzetu watatuunga mkono kwenye Bajeti ya Nishati ya mwaka wa fedha 2025/2026. Hongera sana Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia mambo machache. Jambo la kwanza, niwapongeze Katibu Mkuu wa Wizara, lakini na wote ambao wanasimamia customer care ya TANESCO imebadilika, kumekuwa na improvement kubwa sana. Tunawapongeza kwa kuboresha customer care, kumekuwa kukitokea dharura tunaona kabisa kuna mabadiliko, watu wanapata taarifa kwa wakati, watu wanahudumiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndivyo ambavyo wanasema vijana hawataki kona kona na wao wameonyesha kwamba hawataki kona kona kwenye kutoa taarifa ya changamoto za umeme zinavyotokea ili kuondokana na kipindi hiki ambacho dunia inakimbizana na taarifa potofu, wao wamekuwa wakiwahi, tunawashukuru sana sana sana kitengo cha TANESCO na emergency kwa maana ya kitengo kile cha emergency na customer care.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine kwa Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti yake, asilimia kubwa imejikita kwenye uzalishaji, usambazaji wa umeme. Nizungumze jambo moja tu kwamba, ukisoma Dira matarajio yetu baada ya mwaka 2050, tunategemea kutumia umeme megawatt 20,000 – 59,000, tafsiri yake lazima tuongeze speed ya kuzalisha umeme. Tuzalishe umeme lakini pia tuendelee na hoja yake ya kuimarisha gridi ya Taifa, gridi imara kwa sababu tutazalisha umeme, lakini gridi ya Taifa kama itakuwa au gridi imara itakuwa ni mbovu, umeme hautawafikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kumkumbusha Waziri kwamba, wananchi wa Makete tunalo Bwawa la Umeme la Rumakali. Bwawa hili ni bwawa linalohitajika sana limeshafanya demarcation, limeshafanya evaluation, tunachohitaji ni wananchi walipwe, bwawa liweze kuanza kujengwa na umeme uanze kuzalishwa pale. Wakifanya hivi watasaidia nchi yetu kwa sababu tusije tukafika kipindi ambacho tutapata mgao wa umeme wakati sasa hivi tuna nafasi ya kutafuta vyanzo mbalimbali, vyanzo vya upepo, vyanzo vya gesi na vyanzo vingine. Kwa hiyo kwa niaba ya wananchi wa Makete nikukumbushe hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia kwa sababu Makete wakati ninaingia kuwa Mbunge tulikuwa na vijiji 32 tu vyenye umeme, leo ninazungumza, vijiji vyote vina umeme. Watanzania lazima wafahamu, Taifa letu sisi siyo kijiwe fulani kidogo au kama ni nchi ndogo, unavyozungumzia umeme unawaka Mtwara, ndivyo umeme unavyowaka kule Bunda kwa Esther Bulaya, unavyozungumzia umeme unawaka Makete, ndivyo ambavyo umeme unawaka kule Korogwe, nchi nzima Rais Samia amefikisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa, ni jambo la heshima na nchi yetu siyo nchi tambarare, ni nchi yenye milima na mabonde, lakini TANESCO wamefanya kazi. Tunawapongeza sana kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya usambazaji wa umeme, waendelee kusambaza umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waziri wamesambaza umeme, wametufikia, distribution yetu imeenda vizuri, REA wakimaliza kusambaza umeme, nini kinafuata? Tunajua kuna sheria ya Rural Energy Act ya mwaka 2005, tunaamini baadaye watahitaji kuwachukua REA na kuwaweka TANESCO. Ushauri wangu kama Mbunge na ushauri wa wananchi wengi, kwa sababu distribution itakuwa imeenda sehemu kubwa ya nchi, tafsiri yake ni lazima tuongeze manpower ya watu kuwahudumia tofauti na hapo tutabaki na TANESCO wako Wilayani tu kwenye Kata na pengine kutakuwa na changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vema kama Waziri afikirie ni jinsi gani ya kuifanya REA iendelee ku-exist ili ihudumie distribution. Tunatamani shirika la TANESCO libaki kwenye production na transmission, suala la distribution tuiachie REA ifanye kazi hiyo isimamie hapo ili wananchi wetu tena wasigeuke kero kwa sababu katika nchi yoyote ile revolution inafanyika kwenye mambo mawili ambayo ni barabara na umeme na wamefanya kazi kubwa sana kwenye umeme, tunahitaji wananchi wapate huduma nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu ninatamani angalia namna gani sasa wananchi huko waliko, umeme KIOSK zipatikane kwenye kila Kata au kila Tarafa ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati waweze kuhudumiwa kuliko kusubiria wilayani. Kwa sababu kuna sehemu kama Makete ukitoka Matamba kwenda kuitafuta kata nyingine iliko ni zaidi ya kilometa mia moja, huyo mwananchi akisubiria hilo tatizo linalomsumbua. Kwa hiyo, ninatamani waimarishe hilo eneo la kuhakikisha kwamba huduma inawafikia wananchi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, nchi yetu katika nchi 20 Barani Afrika sisi tumo kwenye usambazaji wa umeme, hii ni ripoti ya World Bank ya mwaka 2023. Katika nchi 20 ambazo zipo katika Barani Afrika sisi tuko katika usambazaji wa umeme kwa wananchi wetu. Tafsiri yake ni nini Mheshimiwa Waziri? Tafsiri yake ni kwamba wananchi wengi watahitaji kuendelea kuutumia umeme na watahitaji huduma ya umeme hususani kwenye viwanda na maeneo mengine kwa sababu tunayo ilani yetu ambayo inasema tunaenda kujenga viwanda, kongani ya viwanda kwenye kila wilaya. Tafsiri yake ni kwamba matumizi ya umeme yatakuwa ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapa tu mfano mmoja Matumizi ya umeme kwa Mkoa wa Iringa kwa mwaka mmoja ni sawasawa na matumizi ya mwezi mmoja ya Mgodi wa Geita. Mgodi wa Geita unatumia umeme kwa mwezi mmoja ambao ni sawasawa na mwaka mzima wa Mkoa Iringa, tafsiri yake mahitaji ya umeme yataendelea kuwa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza kwamba sasa hivi Geita wameingiza gridi ya Taifa kwa sababu pale nyuma walikuwa wanakata kutokana na kwamba walikuwa na changamoto, tunahitaji kuongeza uzalishaji wa umeme kwenye nchi yetu, ajitahidi sana Mheshimiwa Deo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku moja Rais alitumia lugha hii, unaweza ukawa kiongozi lakini usipate nafasi ya kuongoza, lakini unaweza ukawa kiongozi ukapata matukio mawili tu ya kuongoza katika uongozi wako. Moja kati ya tukio ambalo Waziri ameongoza ni hili la mafuta na tunaamini lingine atakalotuongoza ni jinsi gani ya kuhudumia na kuhakikisha kwamba umeme unazalishwa ndani ya nchi yetu, siyo kila kiongozi anapata nafasi ya kutuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Magufuli alikuwa ni kiongozi, lakini alipata nafasi ya kutuongoza kwenye miradi ya kimkakati ambayo hadi sasa tunaendelea nayo, alipata nafasi ya kutuongoza kwenye suala la COVID, nchi ikatoka na ikaenda, sasa tunaamini hata wao kwenye Wizara hii kama vijana, wana maono wanafikiria, watuongoze kwenye uzalishaji wa umeme mwingine zaidi ili aweze kuwasaidia Watanzania wengi kadri ambavyo tunafikiria. Kwa sababu tofauti na hapo Mheshimiwa Waziri tutaenda kwenye disaster, umeme utakwisha, umeme utapungua, mahitaji ni makubwa na tumesambaza kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Makete niendelee kusisitiza Mheshimiwa Deo, sina mambo mengi ya kuzungumza, ninaomba wananchi na Wabunge wenzangu wote tuunge mkono hii bajeti ya Nishati. Tuunge mkono bajeti ya Nishati kwa sababu ukizungumzia vijana wa Tanzania umeme ulivyowafikia vijijini, wengi wameanzisha saluni, wengi wameanzisha sehemu ya kuchomelea, wengi wameanzisha vitu vingi. Vijana Tanzania Wizara hii wamewafanya wainuke kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Wabunge bajeti hii 97.5% tuwaunge mkono Mheshimiwa Deo, tumuunge mkono Naibu Waziri Salome, hatumuungi tu mkono Mheshimiwa Deo tunaunga mkono Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Ilani ambayo imebeba mustakabali wa Taifa letu, Ilani ambayo imebeba revolution ya viwanda ya Taifa letu, Ilani ambayo imebeba kwamba tunaenda kufanya mabadiliko ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana na nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)