Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kupata nafasi hii adhimu kabisa ili niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi ni Mbunge sasa ninaweza kusema ni miongoni mwa Wabunge wachache wa vipindi vingi, ni kipindi changu cha nne hapa Bungeni. Kwa hiyo, nina uzoefu siyo haba, nina uzoefu mkubwa na ninataka niwaambie ndugu zangu, bajeti zote zilizopita za Serikali katika Wizara hii asilimia kubwa ilikuwa inakwenda kwenye matumizi ya kawaida, lakini leo tunaona bajeti hii kwa mara ya kwanza 97% inakwenda kwenye maendeleo. 97% inakwenda kwenye maendeleo, asilimia mbili, tatu tu zinabaki kwa ajili ya matumizi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona nia ya Mheshimiwa Rais, unaona nia ya Waziri pamoja na Wizara yake, namna wanavyotaka kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Ujue unaweza kutenga bajeti kati ya 100%, 70% ikaenda kwenye matumizi binafsi, vitafunwa, mishahara nini, lakini hapa tunaona 97% ya fedha zote zinakwenda kwenye maendeleo kwa wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunaona seriousness ya Serikali katika fedha zote zilizotengwa shilingi 1,500,000,000,000, zote ni za kwetu, zote ni za ndani. Shilingi 63,000,000,000 tu ndiyo zinatoka nje kwa wafadhili. Kwa hiyo, tunaona namna ambavyo Serikali imejitoa muhanga kuhakikisha kwamba mambo haya ya maendeleo kuhusu nishati ya umeme yanafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama hapa nikazungumza sana kuhusu mafuta nikaishauri Serikali kwamba tujenge hifadhi yetu ya mafuta, Serikali yetu ni sikivu ninampongeza sana Rais. Nimeona Wizara hii, Rais walimwalika akaenda kuzindua ujenzi wa matanki ya mafuta ya kwetu, sasa mara nyingi ukijua kulaumu ujue na kusifia, huwezi kujua kitu kimoja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayefanya kazi ya lawama anafanya kazi rahisi siku zote, wewe unajenga nyumba kwa shida kubwa, anakuja mwenzako anakwambia mbovu, nyumba hii mbovu unamuuliza, hata kibanda hana! Kwa hiyo, unaweza kuona namna ambavyo wengine wanafanya kazi ya lawama kwa sababu ni kazi rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpongeze sana Waziri kwa hatua wanazozichukua, tumesambaza umeme kwa kiwango kikubwa, Wabunge wametahadharisha, lakini ninataka niwaombe jambo lingine ambalo humu halijazungumzwa. Umeme mwingi tuliojenga vijijini sasa hivi ugomvi mkubwa watu wanataka umeme mkubwa kwenye kila kijiji, wanataka umeme wa three phase ili ukiwasha mashine ya maji umeme usizimike kwenye taasisi zingine, maana yake sasa hivi ukiwasha mashine ya maji mtu wa kuchomelea hawezi, mtu wa mashine ya kusaga hawezi. Sasa tunataka umeme mkubwa kwenye vijijini ili shughuli zote ziweze kufanyika kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiseme sasa wachomeleaji msichomelee, mashine zimeni, kwa sababu sisi tunajaza maji kwenye tenki, hapana! Vijiji navyo vinahitaji umeme mkubwa kwa ajili ya maendeleo. Hatutaki umeme wa kumulika tu sasa tunataka umeme wa kufanyia kazi kwenye viwanda vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona namna ambavyo Mheshimiwa Rais amepewa u-champion wa gesi duniani. Wizara yenu hii Mheshimiwa Deo pamoja na mwenzake Salome Makamba na Katibu Mkuu Engineer Mramba ni Wizara watambuka. Hao wakizalisha gesi safi ya kupikia ya kutosha wataondoa adha kwenye Wizara zingine, hata mkaa wataokoa hautakatwa mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mkaa unakatwa mwingi kwa sababu watu hawana nishati nyingine ya kupikia, Mheshimiwa Rais kawatwisha zigo hilo wao, wahakikishe kwamba nishati safi ya kupikia inapatikana vijijini na mijini, kwa sababu mijini ndiyo waagizaji wakubwa wa mkaa kutoka vijijini. Kwa hiyo, Wizara hii ni Wizara mtambuka, wakisimamia wakafanya kazi kwa bidii mambo mengi yatakuwa yako safi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO inapoteza mapato mengi sana, kwa nini? Tulisema taasisi za Serikali zisomane, kuna TANESCO kuna nyingine taasisi haiko kwao, ninafikiri inaitwa WMA ambao wao ni Wakala wa Taifa wa Vipimo. Mita nyingi tunazotumia za umeme zinatakiwa kupimwa kabla ya kufungiwa kwa mteja. Sasa tunaangalia kuna mita nyingi zimefungwa kwenye majumba yetu na kwenye taasisi mbalimbali hazijapimwa, matokeo yake nini kinatokea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza umeme tunaibiwa, wale watumiaji wajanja kwenye viwanda kama mita haijapimwa umeme unaweza ukapita bure, pili unaweza ukamwadhibu mtu kwamba ametumia umeme mwingi kumbe mita ile haijapimwa inatumia umeme mwingi wakati yeye hana matumizi makubwa ya umeme kiasi hicho. Kwa hiyo, tunashauri mita za umeme zipimwe na zifungwe seal ili mwananchi ajue mita yangu ni sahihi. Watu weo wakija kukagua kwa mwananchi wanasema wewe unaiba umeme, kumbe haibi umeme mita ni mbovu, mita haijapimwa! Sasa unamlaumu vipi mlaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafikiri wakizipima mita zote za umeme nchi nzima wakawafungia wananchi, uwezekano wa ninyi kukusanya mapato halali ni mkubwa kuliko sasa ambapo wanachukua tu mita zingine zinafungwa bila kupimwa. Hebu chukulia viwanda vikubwa, vitatu tu vikiwa vinapitisha umeme kwenye mita bila kuhesabiwa ni hasara kiasi gani TANESCO inapata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, chukulia mwananchi wa kawaida tu mtaani, unapita unamwambia anaiba umeme, unamfungia kupata huduma za umeme. Hapana, tusifanye ulinzi wa buibui! Buibui anaweka ulinzi wa uzi mwenye ule uzi anaouweka buibui ananasa mbu, ananasa nzi lakini akija ndege anauchukua ule uzi anapita nao moja kwa moja, tuweke sheria zinazoangalia pande zote mbili mlaji na wao wenyewe

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kadri unavyosambaza huduma za umeme ndivyo ambavyo unahitaji vifaa vingi. Ninashauri Serikali iimarishe viwanda vya ndani vya kuzalisha vifaa vya umeme, ili wakati mwingine tusije tukakaa hapa tunasubiri transformer itoke China, tunasubiri sijui nini itoke wapi, sisi wenyewe hatuna uwezo wa kutengeneza? Tuimarishe viwanda vyetu ili hivi vifaa viwe vinazunguka katika mzunguko wa ndani ya Taifa, tukitaka vifaa tuvipate hapa na viwe na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna wanasayansi wa kutosha, Mawaziri vijana wamewekwa hapo, hebu wssomane pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith waone namna gani wanaweza wakatufanyia kazi nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kwenye vitongoji, hapa nimeona tunazungumzia habari ya Ilani ya Chama ni sawa, lakini tungekuwa kila Wizara ikae pamoja na kitabu cha sensa ya watu na makazi, kitawaongoza kujua wingi wa watu hapa. Unajua kuna sehemu wamepeleka huduma nyingi, watu wachache, kuna sehemu watu wengi, huduma kidogo, kwa sababu hawakai na kitabu cha sensa mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri akiwa na sensa ya watu na makazi itamwongoza kusema hivi umeme ninaowapelekea hawa watu utawatosha, lakini waking'ang'ana tu kwamba tunapeleka kila wilaya, kwa mfano hata huduma tu za emergency hivi utalinganisha Wilaya ya Chamwino na baadhi ya Wilaya? Wilaya ya Chamwino square kilometa zake tu sehemu nyingine ni Mkoa. Sasa nguzo kumi zikianguka Ilangali, nguzo zingine zimeanguka Haneti hilo gari linaanzia wapi? Tunawagombanisha wananchi na Rais wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wengine wa TANESCO ambao siyo waadilifu wanasema unajua tuko tunashughulikia Ikulu, unashughulikia Ikulu wananchi nao si wanatakiwa wapate umeme? Kwa hiyo, ningeshauri tuangalie ukubwa wa wilaya ikiwezekana tuzikate katika zones, wilaya inayostahili magari mawili ipewe magari mawili, hata kama wilaya ni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wilaya zingine wataziumiza kwa sababu ni wilaya kubwa na zinahudumia watu wengi, kama Wilaya ya Uyui ninaambiwa hapa nayo anapeleka gari moja haiwezekani! Ninaona ndugu yangu Mheshimiwa Nape anatingisha anasema bwana hata Jimboni kwangu nikipata nafasi nitapiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwamba tufike mahali tukiimarishe Kitengo cha Emergency kifanye kazi, hawa watu wamepambana mwaka huu kwenye mvua hii tumewaona, tunapita huko mitaani tunakuta vijana wetu wanakesha kubeba nguzo kwenye mapori makubwa, wanastahili pongezi jamani siyo kila kitu ni kulaumu tu! Watu wanajitoa kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wameng'atwa na nyoka wengine huko porini wamepoteza Maisha, sisi tulipata taarifa, ni vitu vya kutisha wanalipambania Taifa hili liweze kwenda, sisi hatuwezi kukaa hapa kama hatuoni, tuongeze juhudi za kuwasogezea vifaa karibu, vifaa vingi na ikiwezekana tuendelee kusomesha vijana wetu ili waendelee kulibeba Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo yamezungumzwa mengi katika Wizara hii, lakini nilisema nizungumze kuipongeza Serikali, kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa msimamo wake hasa wa kuhakikisha kwamba akina mama wanapika kwa kutumia gesi iliyo salama kuhakikisha tunakuwa champion wa gesi, haya mambo mengine tutaendelea tutasukumana taratibu, lakini yale ya msingi tuyasimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)