Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Nishati. Kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nishati kwa namna ambavyo wameweza kufanya kazi kubwa katika kusambaza umeme kwenye maeneo yetu. Kipekee zaidi ninawapongeza Shirika la REA kwa kazi kubwa na ya kihistoria ambayo wameifanya, ya kusambaza umeme katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wa pili kwa sasa ukiacha Afrika Kusini kwenye connectivity ya umeme. Yaani ule umeme ambao sasa unaenda kwa mlaji sisi tupo nafasi ya pili. Jambo hili ni kubwa kwetu kihistoria; na ninataka niseme, kwamba tuendelee kuiunga mkono Wizara hii ya Nishati pamoja na REA ili Watanzania wengi waweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Waziri wa Nishati. Katika vitongoji ambavyo vimeweza kutoka kwa maeneo mengi kwa Wabunge, nimepata vitongoji 98; na Wilaya yangu ya Bahi ina vitongoji 520 na sasa vitongoji 300 vitakuwa na umeme. Kasi hii tunayoenda nayo ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, kwamba bado lipo tatizo la kuunganishiwa umeme. Mwananchi akitaka kuweka umeme kwenye nyumba yake anaambiwa unatakiwa uchangie nguzo hapa nne, nguzo tatu, inafika mpaka shilingi 600,000 mwananchi atoe. Ninadhani hatutendi haki katika jambo hili. Suala la kununua nguzo, suala la kuweka nguzo si suala la yule mlaji wa mwisho, ni suala la TANESCO ndiyo wanaotakiwa waniletee nguzo pale. Kwa kufanya hivyo, kwa sababu mimi ni mteja wao wa kudumu ile gharama ya nguzo itakuja kukatwa baadaye. Tukifanya hivi tutasaidia wananchi wengi waweze kuweka umeme katika nyumba zao; lakini kumwambia mwananchi alipie umeme mimi ninaiona siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine; umeme wetu sasa tunazalisha megawati 4,522, lakini umeme wetu kama ilivyo katika maeneo mengine, ni kwamba unatoka kwenye source mpaka kule unakokwenda kuwashwa kwenye balbu, hakuna sehemu unasema utautunza halafu baadaye uweze kwenda kwa mlaji wa mwisho, tunafanya hivi. Sasa, bado ninaishauri Serikali ipime exactly megawatt tunazozipata kwa walaji ni kiasi gani. Sawa tuna jumla ya tunazozalisha lakini je, exactly kwa walaji ni kiasi gani? Maana yangu nini; ni kwamba upo upotevu mkubwa wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nichangie kuhusu upimaji wa mita tunazofungiwa kwa ajili ya LUKU zetu za umeme. Wakala wa vipimo ndiye anayepima zile mita za LUKU kabla mlaji hajaanza kuzitumia. Bahati mbaya TANESCO, ukilinganisha na wenzao wa Wizara ya Maji, imekuwa haipimi zile mita. TANESCO kwa mwaka inatumia mita kati ya 500,000 mpaka 800,000 lakini hazipimwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hazipimwi shida inakuja wapi? Ninaweza nikapewa LUKU au mita ambayo inakuwa haiwezi kusoma umeme. Ninaweza nikanunua umeme, nikakaa nao miezi mitano au ninaweza nikanunua umeme nikatumia siku mbili umeme umekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko kwenye Kamati ya Viwanda. Tulitembelea pale kwa Wakala wa Vipimo na wakasema na kilio hiki ni kikubwa. Walisema kwamba TANESCO hawataki. Sisi tukasema, tusiiseme TANESCO pamoja kama TANESCO, ninadhani ni ile idara ya manunuzi. Kwa sababu mtu anayeuza zile mita jukumu la kwamba lazima zipimwe ni suala la kisheria katika ile Sheria ya Vipimo, Sura Na. 340. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mtu mwingine anaweza akajiuliza umuhimu wa kupima ni nini? Umuhimu wa kupima zile mita ndiyo kama huu niliosema; ninaweza nikauziwa mita ambayo haisomi au ninaweza nikauziwa mita ambayo nikiweka umeme wangu unaisha haraka, vile vile, hata hitilafu nyingine za umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kupima kiwango cha umeme kupitia kwenye ile sheria na kwenye kanuni ile ya 22 unaangalia kiwango cha watts zilizokwenda, lakini vile vile hata kiwango cha temperature; sasa hiyo ni ya kitaalam. Kwa hiyo, shida nyingine ya nyumba zetu kuungua na ajali za umeme zinatokana na kifaa kile ambacho pale kinasoma umeme unaoingia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba Mheshimiwa Waziri anavyokuja ku-windup kwenye bajeti hii, ni kwamba TANESCO ni lazima wale supplier wanaowauzia mita wasiwape kabla hazijapimwa kwa sababu watu wa maji wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mita moja kwa mlaji wa kawaida ni shilingi 10,000 halafu wale wa biashara ni shilingi 20,000. Wale wa migodi nadhani na viwanda nayo iko juu kidogo. Sasa bei ile wanaweza wakaifanya kwamba wakai-subsidize kwamba badala ya yule supplier alipe pale, wao wanaweza kuweka utaratibu gani namna ambavyo wanaweza kuifidia. Ninaomba jambo hili liweze kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1976 tuliweza kuzindua TIPER (kampuni ya kusafisha mafuta hapa nchini). Bahati mbaya tukaja kuacha zoezi lile la kusafisha mafuta tumekuwa tunaagiza. Ninaomba jambo hili Serikali sasa ilifanyie kazi. Kwanza kwa mwaka jana tumepitisha lita bilioni 11, bilioni sita za mafuta ya hapa nchini, bilioni tano kwa mafuta kwa ajili ya transit. Kwa hiyo tuna mahitaji makubwa sana. Kwa kufanya hivyo sisi tutakuwa tuna-supply mafuta kwa Nchi za Congo na nchi zote zinazotutegemea. Sawa mafuta ya Uganda yanapita kwetu hapa na yana mkataba na yale makampuni mawili ya Ufaransa na China. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukaongea kwamba na sisi tununue crude oil tusafishe hapa tuweze kuuza na nchi yetu itakuwa haina shida ya mafuta. Ninadhani Serikali isiwaze hela, iwaze wazo zuri hili kwamba tuwe na refinery hapa ili tuweze kutengeneza mafuta ya kwetu hapa na tuweze kuziuzia nchi zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, imetokea kwamba suala zima la sintofahamu iliyotokea ya kupanda kwa mafuta na hili ninaloliongea tukishakuwa na refinery ya kwetu ina maana tutakuwa na uwezo wa kuwa na stability kubwa na security of supply ya mafuta katika nchi yetu na wananchi wetu tutaweza kuwauzia katika bei ndogo zaidi kwa sababu mafuta tutazalisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)