Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Sylivia Francis Sigula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili kuweka mchango wangu katika Wizara yetu hii ya Nishati. Kwanza kabisa ninaanza kwa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia zawadi ya uhai na kuweza kusimama katika Bunge hili Tukufu kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo ninapenda kutoa pongezi zangu na shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake makubwa juu ya kutuletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara. Nikiwa kama Mjumbe wa Kamati kwa kweli tunaridhishwa na namna ambavyo Wizara inapambana kutatua changamoto za wananchi, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na msemo ambao unasema kwamba ‘Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu’, lakini ukitafakari upya utaona kabisa nishati ndiyo engine ya maendeleo ya sekta zote. Ninasema hivyo kwa sababu hakuna viwanda bila nishati ya umeme, hakuna biashara bila nishati ya umeme, hakuna hata hicho kilimo cha kisasa bila nishati ya umeme, lakini hakuna teknolojia bila nishati ya umeme. Hapo utakubaliana nami kwamba nishati ndiyo engine ya maendeleo ya sekta zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Taifa lolote lililowahi kupiga hatua bila kuwekeza kwenye nishati ya umeme. Hapa hata tukiangalia Mataifa ambayo yamefanikiwa, tukiangalia China zamani ilikuwa ni Taifa la kilimo, lakini leo China ni kiwanda cha dunia kwa sababu waliwekeza kwenye nishati ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninaomba kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mwanamama shupavu, jasiri, mzalendo na mwenye maono makubwa. Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani suala la upatikanaji wa umeme vijijini lilikuwa limefika 66%, lakini leo tunavyoongea, suala la umeme vijijini upatikanaji wa umeme vijijini limebaki kuwa ni historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyo ndiyo Rais ambaye anatambua kwamba nishati ya umeme ndiyo engine ya maendeleo ya Taifa letu. Lakini tumeona tumeshatoka kwenye level ya vijiji tuko kwenye vitongoji na kwenyewe tunapiga hatua na muda si mrefu tunakwenda kumaliza tatizo la upatikanaji wa umeme katika vitongoji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutuma salamu za Wanarukwa. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani hajatusahau Wanarukwa. Wakati anafika suala la upatikanaji wa umeme vijijini lilikuwa 58%, leo Rukwa vijiji vyote 339 vina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi Rukwa tuna vitongoji 1,816. Katika vitongoji hivyo, vitongoji 1,507 vyote tayari vina umeme na vitongoji 300 vilivyobaki hivyo, vitongoji 156 tayari mkandarasi yuko site. Tunapotoa kura za kishindo kwa Mheshimiwa Dkt. Samia tuna sababu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hayo ndiyo mafanikio ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya katika sekta hii. Tunaona dhamira yake ya vitendo ya kutuletea maendeleo Taifa letu kupitia nishati. Hapa nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais amewaamini sana, wao ni vijana, kasi yao ni nzuri, tunafurahishwa na namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yao. Mungu awabariki sana, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuleta maombi ya Wanarukwa. Pamoja na jitihada nzuri ambazo zimefanywa na Serikali, kwenye upande wa umeme, tuna Kituo cha Kupozea Umeme cha Malangali, kiko Wilaya ya Sumbawanga Mjini. Sisi Sumbawanga tunachukua umeme pia kutoka Zambia, lakini umeme ule unatutosha kwa matumizi ya mwanga na shughuli za kawaida. Leo Mheshimiwa Rais ameshatoa shilingi bilioni 200 kuwawezesha akina mama na vijana wakajikwamue kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, akina mama watahitaji kuanzisha viwanda vidogo, vijana watahitaji kuanzisha viwanda vidogo. Sasa tunahitaji kupata umeme wa uhakika utakaoenda kukidhi matamanio na matarajio ya wananchi wetu. Upatikanaji wa kituo hiki cha kupozea pale Sumbawanga, Malangali utatusaidia sisi watu wa Rukwa kuwa na umeme wetu wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulipaswa kuwa umekamilika mwezi Aprili mwaka huu, lakini kwa changamoto ambazo zipo, mradi huo mpaka sasa haujakamilika. Ninamwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri, yeye ni msikivu, lakini wewe ni mchapakazi. Namwomba sana atusaidie kuhakikisha Mradi huu wa Kituo cha Kupozea Umeme wa Malangali unakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maombi maalum kutoka kwa wanawake wa Mkoa wa Rukwa. Ukiangalia hali ya nishati safi ya kupikia katika Mkoa wetu wa Rukwa, hii ni ajenda ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan moja ya ajenda zake anatamani kuona akina mama wa Taifa hili wanatumia nishati safi na salama ya kupikia, lakini kwetu sisi Mkoa wa Rukwa, hali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ni 11.4% tu na 88% ya wananchi wa Rukwa wanatumia mkaa na kuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, akina mama wa Rukwa wanahitaji wapewe elimu, akina mama wa Rukwa wanahitaji waambiwe manufaa sahihi ya kutumia nishati safi, lakini akina mama wa Rukwa wanahitaji kuwezeshwa vitendea kazi hasa hiyo mitungi ambayo iko kwenye ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua akina mama ndiyo wako mstari wa mbele kuhakikisha familia zinakwenda vizuri. Kwa hiyo, tutakapotatua changamoto hii ya kuhakikisha akina mama wanapika vizuri, akina mama wanapika kwa haraka lakini akina mama wanapata pia afya njema kutokana na matumizi safi ya kupikia. Kwa hiyo ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Rukwa tuko tayari kupokea mafunzo kutoka Wizarani kwake. Wakati wowote tushirikishe wanawake wapo tutawaandaa waweze kupewa mafunzo, lakini pia waweze kupewa vitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba hapa kwa dhati ya moyo kulipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninampongeza Mheshimiwa Spika, lakini ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo tulishughulikia changamoto ya mafuta wakati imetokea siku chache zilizopita. Mheshimiwa Spika aliongoza vikao vingi, lakini pia timu ya Wizara, lakini na Waheshimiwa Wabunge maoni yao na ushauri wao. Ndiyo maana mpaka leo Taifa letu lipo kwenye utulivu mkubwa sana, Waheshimiwa Wabunge ninawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, tumeona dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais na ameshaelekeza kwamba ofisi yake ibane matumizi, lakini hatujui vita itakwenda mpaka lini. Sisi kama Serikali lazima tujiandae kuchukua tahadhari, mafuta kama yataendelea kupanda hali za wananchi wetu zitakuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo, kama Serikali ninaungana na ushauri wa Kamati, tujiandae kisaikolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mwaka 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilipotokea vita ya Ukraine, alitoa shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kuweka ruzuku kwenye mafuta. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aangalie namna nzuri ambayo kama vita itaendelea tuone namna nzuri ya kwenda kuwasaidia wananchi wetu ili wasiende kupata mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa machache haya, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)