Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hii Bajeti ya Wizara ya Nishati 2026/2027. Dira ya Maendeleo ya Taifa imethibisha kuwa nishati ni kichocheo muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu ambapo inawezesha ukuaji wa viwanda, inaongeza tija katika uzalishaji, lakini inaboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii sana kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta hii ya nishati, nimpongeze sana kaka yangu Waziri na Naibu Waziri wa Nishati, kazi wanazozifanya zinaonekana kwa vitendo, nishati ni muhimu kwa Taifa letu na tunasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshuhudia kuona maboresho ya uzalishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa sana, tunaona ukamilishaji wa Bwawa kubwa sana la Mwalimu Nyerere limefikia 98%. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niipongeze sana TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania) kwa maboresho ya miundombinu ya umeme katika kupitia Kampuni Tanzu ya ETDCO. Kampuni hii inafanya kazi kubwa. Hivyo, ninaomba niishauri Serikali kuongeza kiasi cha fedha kwenye kampuni hii ili iweze kufikia maeneo mengi Nchini Tanzania. Kwa sababu miundombinu mingi iliyopo ni ya zamani, sehemu nyingi tunatumia nguzo zile za zamani, kwa hiyo unakuta wakati mwingine umeme unakatikakatika kutokana na uchakavu wa miundombinu ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia kwa uzalishaji wa nguzo bora na za kisasa za umeme Nchini Tanzania, kwa kweli hii hatua ni kubwa, maana zamani nguzo zilikuwa zinatoka nje kwa gharama kubwa sana. Ninaomba niishauri Serikali kupitia Shirika hili la TANESCO ambalo ndiyo wasimamizi, hii Kampuni Tanzu ambayo inatwa TCPM inayozalisha hizi nguzo, iangalie namna bora ya kutawanya uzalishaji badala ya kutangaza tenda kwa makampuni yenyewe ikafanye mazungumzo kwenye zile sehemu ambazo zinazalishwa cement, makampuni yale yanayozalisha cement. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hizi nguzo zinatumia cement yale makampuni yatakuwa yana uwezo wa kuzalisha zile nguzo bora kwa kutumia viwango vizuri vya cement. Kwa kuwa Tanzania tuna viwanda vingi sana vya cement kila kiwanda kikitengeneza cement, basi TANESCO iweze kuhudumia kwa zone ambazo kunatokea vile viwanda. Hivyo, itapunguza gharama ya nguzo zile mpya na hatimaye kila Mtanzania atapata nguzo mpya na bora ambazo zile zimetumia cement. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishauri Serikali kwa mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Nishati ni kubwa, ninashauri Wizara hii iongezewe bajeti hasa hasa kwenye Shirika la TPDC. Shirika hili la TPDC linafanya kazi kubwa sana na lina miradi mingi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la TPDC linafanya Mradi wa Kusambaza Miundombinu ya Gesi Asilia Majumbani, mradi ambao unatumia gharama kubwa sana na mpaka sasa hivi ni kaya elfu moja mia mbili na kitu ndizo zimeweza kufikia, lakini ukichunguza ni kutokana na kukosekana kwa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaishauri Serikali ione haja ya kuiongezea Shirika la TPDC bajeti ili waweze kuongeza tija na kuweza kuwafikia wananchi wengi katika usambazaji wa miundombinu ya gesi, ambapo kila Mtanzania aweze na yeye kufanya maamuzi ya kutumia gesi kama vile anavyotumia umeme, kama vile anavyotumia maji. Kwa hiyo, kila nyumba ikipata mtandao huu wa mabomba ya gesi itarahisisha pia kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TPDC pia inashughulika na Mradi wa EACOP, lakini inashughulika na Mradi wa Utafiti wa Gesi Asilia pamoja na mafuta ambao uko Eyasi kule Wembere. Mradi huu una gharama kubwa sana na kwa kuwa sasa hivi tunanyanyasika na mafuta haya kutoka kwa wenzetu huko nje, ninaishauri Serikali kuona haja ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye Shirika hili ili watafiti waongeze kasi ya kutafuta visima vya gesi Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaimani Tanzania tuna rasilimali hii kubwa maeneo mengi sana isiwe tu TPDC kuonekana Mtwara, nina imani hata Mwanza, Manyara na sehemu nyingine za Tanzania pia tunaweza tukapata mafuta kwa wingi na au gesi kwa wingi ili Serikali iweze kuwekeza. Hata hivyo, TPDC ina mradi wa LNG ambao kimsingi utakuwa mkombozi sana Nchini Tanzania endapo utakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nishauri kwamba kwa kuwa Serikali imekuwa na imani kubwa kwa hili Shirika la TPDC kwa kulipa jukumu la kuagiza mafuta nje kwa kipindi hiki cha uhaba wa mafuta. Ninaomba Serikali yetu sikivu iendelee kuliamini Shirika la TPDC kuendelea kuwa waagizaji wakubwa wa mafuta yote nchini ili wale wafanyabiashara wengine wabaki kuwa oil marketing companies. Hii itasaidia Serikali katika kuongeza pato la Taifa na kuongeza ufanisi kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia kuishauri Serikali kuona haja ya kuanzisha Gridi ya Taifa ya Nishati ya Gesi Asilia ya kupikia majumbani, lakini sehemu za biashara, pamoja na viwanda vidogo ili kuwasaidia wajasiriamali kupunguza gharama ambazo sasa hivi wanaingia. (Makofi)
Mheshimiwa kwa mfano sasa hivi Mheshimiwa mjasiriamali unampa mtungi, anapata mtungi leo atapewa mtungi ukishaisha mtungi kwenda kujaza ule mtungi mdogo gharama ni 25,000 lakini akirudi akienda ule mkubwa gharama ni 50,000. Kwa hiyo, unaweza ukakuta faida yote anayoipata inashia kwenye ile mitungi ya gesi na dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha gesi asilia inawanufaisha wajasiriamali wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nishauri pia Serikali kutokana na Gridi ya Taifa kupata break down; kwa mfano juzi Gridi ya Taifa ilipata break down wasafiri wa treni walishindwa kusafiri, treni ilisimama abiria wengi walishuka kwenye ile treni kusubiria stabilization ya umeme ili waanze na safari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niishauri Serikali yangu sikivu kuona namna ya kupeleka power back up kwenye hivi vituo vya gesi ili ikitokea tena tatizo kama hilo ili wasafiri waweze kuendelea, lakini hata kwenye yale maeneo muhimu yanayotoa huduma, huduma zisikwame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)