Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu Wizara ya Nishati ambayo ni tegemeo kubwa kwa nchi, ni tegemeo ambalo sisi Watanzania ni Wizara ambayo ni kiunganishi katika taasisi zote za nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana waandaaji wa mpango wa bajeti hii. Jambo kubwa la msingi na la maana na katika historia ya nchi hii ni pale ambapo umeandika trilioni 1.6 zinatoka mfuko wa ndani, lakini tegemezi ni bilioni 800 na something kidogo, ni jambo kubwa na ni jambo la kujivunia, hongera sana watalam, Katibu Mkuu na watendaji pamoja na Waziri mwenye dhamana na msaidizi wake. Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba nishati hii inaenea katika maeneo ambayo tunayoyatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mpango wa REA, ninaamini katika trilioni 1.6 baadhi ya maeneo kwenye Mkoa wetu wa Simiyu niwapongeze sana Wizara, wameleta ujenzi wa kujenga Kituo cha Kupozea Umeme pale Imalilo na baada ya kuona wakandarasi wanasuasua TANESCO kupitia wataalam wao wameleta na mradi unakwenda vizuri sana, ninawapongezeni sana kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo sisi Wabunge tukiwa tunazungumza kwamba kila wizara itumie ufanisi katika watalam tulionao kwenye Wizara ili waweze kunusuru maendeleo ya Taifa letu na kazi hiyo TANESCO wameifanya. Mradi uko 47%, hongera sana na Mungu awabariki waendelee kuongeza maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikibidi Mheshimiwa Waziri waendelee kuwapeleka vijana wapate ufanisi zaidi kwenye mataifa yaliyoendelea ili kusudi tupate wataalam ndani ya maeneo yetu. Fedha nyingi tunaitoa, lakini tuna vijana wako ndani ya nchi wanaweza wakasimamia, wakafanya kazi nzuri hata tatizo likitokea tunaweza tukawahoji na tukawauliza ni jambo ambalo Wizara hii wameonesha uthubutu wa hali ya juu. Bila kusahau kwamba Mheshimiwa Rais ndiyo amewapa majukumu makubwa kama haya na ndiye mtoa dira, mbeba maono ya nchi. Hapa walipofikia ndiyo mahali penyewe, ni jambo la kuwashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, lakini jambo lingine, Mkoa wetu wa Simiyu ninadhani ni mkoa mkubwa na unaokua kwa kasi. Kwenye suala la REA Vijiji, Wizara inafanya kazi kubwa na REA lakini bado kuna changamoto, wakandarasi wanaowapa hizo tenda wao wanaangalia maeneo ambayo hata kama kuna taasisi ya kiserikali ambayo inahitaji umeme kulingana na mikataba na utaratibu wanaowekeana inakuwa ni changamoto kubwa, kuna shule au kuna zahanati hapa inarukwa kwa sababu scope ile haijafika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri na niwaombe, maeneo yote ambayo yako kimsingi na yako kwenye jambo ambalo tunategea kuwa na teknolojia ya sasa, basi wawaruhusu ili kusudi maafisa waliopo kwenye maeneo ya mikoa ile, wawape dhamana ya kuhakikisha kwamba wanachangisha mawazo mazuri kupitia ngazi za halmashauri. Ili kusudu umeme maeneo yote yaweze kupata umeme wa REA ili kusudi tufikie kule ambako tunapokufikilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninataka nizungumzie suala la EWURA; tunawapongeza wanafanya kazi kubwa na nzuri, lakini Taifa linakua na linaongezeka, mahitaji ni makubwa, pikipiki watu wananunua kila siku, zamani kule usukumani tulikuwa tunatumia baiskeli. Hii dhana Mheshimiwa Waziri ya kwamba kibali tu cha mtu apate leseni ya kuweka kituo katika Kijiji X mpaka Bodi ikae ni jambo ambalo limeshapitwa na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi inatakiwa ishughulike na mambo makubwa, hicho ni chombo kikubwa sana waachieni management watoe hizi leseni kwenye wilaya kule wanakojenga na hiyo inasababisha nini? Inasaidia kuwa na control ya mafuta kwenye nchi, inasaidia kupunguza gharama kwa watumiaji maana kwenye eneo ambalo hakuna kituo cha mafuta, mnunuzi anaweza akauza bei yoyote anayoona anajisikia kwa sababu hakuna control.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele kadogo tu unaambiwa Bodi ikae, haijaruhusu wakati kule kuna Serikali, kuna Mkuu wa Mkoa, kuna Mkuu wa Wilaya, kuna Wakurugenzi, kuna viongozi. Ninadhani Mwenyekiti ifike sehemu wafanye mabadiliko maamuzi mazuri, bodi zishughulike na mambo makubwa makubwa, ujenzi wa mabomba ya gesi hayo, LNG basi hata Bodi ikikaa inajadili vitu vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kituo cha pampu mbili Bodi hivi ikae inatumia thamani ya shilingi ngapi kukaa kwenye hilo jambo. Hilo nalo halihitaji yaani linahitaji tu maeneo mafupi kutoa kibali, management ifanye hizo kazi maisha yaendelee na watu waendelee kufurahia na kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, TANESCO sasa hivi tunapanuka, zamani tulikuwa tuna viwanda vichache na tulikuwa tukiamini kwamba uhitaji wa umeme ulikuwa ni mkubwa na gharama ilikuwa kubwa kuliko uhitaji ulioko sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye wawekezaji wote anapokata kile kiwanda malighafi ikiisha anabidi alipe miezi mitatu 75%. Niiombe Serikali kulingana na hali ya sasa ilivyo uwekezaji unapanuka unaenda kwa kasi na tuna-compete na nchi zingine tukiendelea na mfumo huu na uzalishaji wetu ni mdogo. Tukiendelea na mfumo huu wawekezaji wa ndani wataendelea kunyong’onyea, wataendelea kurudi nyuma kwa sababu bili ya mwisho inaweza ikaja labda milioni mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua 75% yake kwa miezi mitatu hazalishi ni suala tu la kitaalam, wakae waangalie ku-review kuangalia namna gani itakayokuwa bora ili na hawa waweze ku-complete na mataifa mengine kwenye biashara ambazo wanazifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana jambo hili ni muhimu sana wakatusaidia ili kusudi kila ambacho tunakitarajia kiweze kufikiwa katika malengo husika na watu waendelee kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwapongeza sana Wizara ya Nishati, kwa maamuzi makubwa ambayo wameyafanya ya kuhakikisha chombo cha ndani kimetajwa na Mbunge aliyemaliza kuzungumza TPDC kukijengea uwezo wa kuweza kuagiza mafuta hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili kidogo ni gumu na linahitaji uthubutu ukigusa mafuta ndiyo mataifa makubwa kule duniani, tunasikia sisi sote tulioko humu ndani. TPDC akipata ni chombo chetu cha ndani, chombo ambacho tunaweza tukaki-regulate na kukisimamia na tunapozungumzia usalama wa nchi ni pamoja na mafuta, hakuna jambo lolote linaweza likafanikiwa bila kuwa na mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali iweze kuwajengea uwezo na hawa TPDC wajiendeshe kibiashara siyo kutengewa fedha, wafanye kama ni miaka miwili inayofuata waanze kuendesha biashara kama Makampuni mengine wa-compete, watengeneze faida ili walete faida walipe kodi Serikalini na waajiri watu katika maeneo ambayo tunayoyatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo Serikali ya CCM, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tutaanza kuona mabadiliko makubwa; na niwaombe wataalam niliangalia Hotuba ya Mheshimiwa Rais alipokuwa akifungua mradi wa kuweka mafuta pale TPA, alieleza kwamba sasa tumekuwa na storage za kutosha. Maana yake Rais alikuwa na masikio, alikuwa anamaanisha kwamba tuwe na storage za kutosha, tuwe na mafuta ya kutosha ndani ya miezi miwili yalitokea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Taifa lisingekuwa na watu wenye uweredi leo hata tusingefika humu ndani na magari yetu hata shughuli zingine zote zingekuwa zimesimama. Sasa niombe watumishi wa umma wajenge uzalendo wa kusimamia kile ambacho tunakitarajia katika Taifa letu. Tukifanya hivyo ninaamini tutapiga hatua na TANESCO – Wizara ya Nishati wameanza vizuri, lakini ninaomba wafanye maamuzi ambayo yatakayosaidia Taifa na kuhakikisha Dira ya Mwaka 2025 - 2050 inafikiwa kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya vizuri zaidi. Niendelee sana kuwaomba katika mkoa wetu na katika Jimbo langu la Itilima bado vitongoji 229 havijapata umeme. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii ya trilioni 1.6, atakapokuja atuambie zinazokwenda kwenye REA ni kiasi gani na anazobakinazo huku ni kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, focus kubwa katika wizara hii ni wizara ambayo inaunganisha wizara zote na wao wakilala tu wizara zingine zote tunasimama. Ukizungumza mafuta wako nayo, ukiizungumza umeme wako nao, ni jambo la kushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana. (Makofi)