Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hii hotuba ya Waziri wa Nishati. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais aliyekuwa mwingi wa fadhila kwa kuwateua Mawaziri wazuri, Manaibu na Makatibu wazuri kwenye Wizara ya Nishati. Rafiki yangu Mheshimiwa Ndejembi, leo nilikuwa na mambo mengi mengi, sasa ninamwona kama vile ananiangalia, lakini ukweli ni kwamba kazi anafanya na hata waliokuwepo kazi walikuwa wanafanya kwenye Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba, sisi Wabunge tuliorudi hapa Bungeni na moja ya hatua kubwa zilizopigwa ni pamoja na kuweka umeme vijijini na kwenye vitongoji. Maeneo mengi sasa hivi wananchi wameshakuwa na wivu. Kitongoji A kikikosa umeme Kitongoji B kinasema sisi kwa nini hatukupata. Tatizo tulilonalo sasa ni usambazaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaiomba sana Wizara; sasa hivi ni kipindi cha kushauri. Taasisi zetu sisi, sekta kwa mfano shule za msingi zote, vituo vya afya vyote, zahanati zote, sekondari zote, sasa ninashindwa kuelewa mambo mengine. Hivi Wizarani kwenu huko hamna data? Kwamba Bunda kuna zahanati tano hazina umeme, kuna vituo vya afya sita havina umeme, kuna shule za msingi tano hazina umeme, kwa nini hawana data hizo? Kwa nini shule moja inaweza ikakaa miaka mingi haina umeme? Wanajenga vituo vya afya havina umeme, tunajenga shule mpya hazina umeme, tunajenga hospitali za wilaya hazina umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupeleka umeme pale wanaenda TANESCO wanaambiwa shilingi milioni 38. Sasa ni mambo gani haya? Kwa hiyo, ninaomba wawe na data za kuweka umeme kwenye sekta maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Bunda; ninaomba hii ieleweke, maana yake tunaenda kwenye Dira yetu ya 2050, ieleweke Mheshimiwa Waziri. Ieleweke wewe ni kijana, ieleweke wazi kwamba, ni kweli Serikali tumepeleka umeme kwenye vijiji, ni kweli Serikali imepeleka umeme kwenye vitongoji, lakini uhalisia ni kwamba kitongoji ni nini na kijiji ni nini? Kijiji ni muunganiko wa vitongoji. Maana yake kama tumepeleka umeme, tunapeleka kwenye centre ya kijiji fulani, ambacho kijiji hicho kina kaya 300 na umeme uliokwenda ni kaya 25 au kaya 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huko tunakokwenda kwenye dira yetu tufikirie namna ya kusambaza umeme kwenye nyumba za watu, siyo kuweka idadi ya vijiji na kuweka idadi ya vitongoji. Kwa hiyo, ninaomba huko tunakokwenda kwenye dira yetu tufikirie mambo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mafuta ninaomba Waziri, ninajua hiyo Bulk Procurement System ni nzuri, imelinda mfumo wa kuwa na mafuta nchini. Hatuwezi kuikataa, nzuri sana; kwa sababu wenzetu kuna wengine wana hela, hawana mafuta. Ni nzuri sana lakini huko tunakokwenda kama hali itakuwa mbaya, ndugu zangu turuhusu watu binafsi kuingiza mafuta. Vinginevyo tunataka twende kupunguza fedha au tozo za mafuta kwenye maeneo mbalimbali ya kimaendeleo. Kama tunaona ni vipi turuhusu watu binafsi ili ushindani uwepo ili tuweze kupata mafuta ambayo yanaweza kutusaidia kwenye hali zetu za kawaida hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba hili lieleweke. Miaka yote ambayo REA imekuwepo, walitwambia kwamba kijiji kinapelekewa nguzo 60 na kitongoji kinapelekewa nguzo 40, miaka yote. Toka tumeanza REA kijiji nguzo 60 wananchi wamekaririshwa wamejua. Saa hizi simu zinapigwa. Juzi wamesambaza nguzo, wamepeleka nguzo 30 kwenye kitongoji. Wananchi walishaelimishwa kwamba kitongoji ni nguzo 40 na kwenye kijiji ni nguzo 60. Kwa nini nguzo zimeenda 30? Ninajua inawezekana kwamba wameona labda kahela walikonako (kasungura) ni kadogo, lakini ni bora pale ambapo tungepeleka vitongoji vitano tukapeleka vitongoji vitatu, lakini kwa nguzo 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hizi nguzo kwenye maeneo ya huko kwetu, kutoka nyumba moja kwenda nyumba nyingine ni nguzo 18. Sasa, sisi ambao tuna maeneo makubwa kiasi hicho unakuta hizo nguzo 30 zinaenda miji mitatu tu. Ndugu zangu hii inatuletea shida. Kwa hiyo, pale ambapo waliona kuna mapungufu ya nguzo 10, kama kuna uwezekano wa kupata hela mahali turudishe. System ieleweke kwamba kitongoji ni nguzo 40 na kijiji ni nguzo 60. Mheshimiwa Waziri kazi wanafanya kubwa sana, kubwa ya umeme, lakini huwa ninajiuliza, hivi system ya umeme ya REA ikifa au siku tukiacha REA, TANESCO itafanya nini? Sijui kama kuna TANESCO saa hizi, maana yake huko kijijini ni REA REA, REA. Hivi sasa TANESCO wako wapi? Wanafanyaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sasa kama kuna mafungu ya TANESCO na ninaomba Waziri, mimi sielewi na kwa nini sijui mimi sielewi. Kwa nini tusianzishe wale watu wenye uwezo wa kupata umeme hata kwa kukopa tuwakopeshe kwa dhamana ya Serikali watakuwa wanakatwa humo humo ndani, hivi hilo haliwezekani?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ninataka kumpa tu taarifa ndugu yangu Mheshimiwa Getere inawezekana REA anaiona kwa wingi sana kwa sababu ya nature ya jimbo lake. Ninataka nimpe tu taarifa kwamba, REA wakikamilisha kazi inakuwa handled na TANESCO thereafter, lakini TANESCO pia kuna maeneo wanafanya hasa kwa sisi ambao tuko kwenye majimbo ya mjini ambayo hayana programu za REA. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere taarifa ya Mheshimiwa Esther unaipokea?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa utaikataaje tena taarifa ya mdogo wako? Unaipokea tu hivyo hivyo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli lazima tupunguze gharama za umeme. Hivi kweli, maana ninauliza hili swali nikiwa na mantiki moja. Kwamba, kijijini tukiacha shilingi 27,000 na wakati TANESCO ni shilingi 320,000/370,00 ni mwanakijiji gani ataingiza umeme? Ataingizaje? Kwa hiyo, ni lazima hata kama REA itakufa, system ya kuweka umeme kwa shilingi 27,000 au hata kwa shilingi 40,000/= itengenezwe na Serikali ili watu wa vijijini waendelee kuweka umeme. Vinginevyo kama tunaleta system ya mjini, kupeleka umeme kwa mtu shilingi 320,000/370,000 mwanakijiji hawezi kuweka umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ninawashukuru sana watu wanafanya kazi kubwa. Watu wa REA ninawashukuru sana wanafanya kazi kubwa, Mkurugenzi wa REA na watu wote wa REA. Kweli mimi REA ndiyo ninawaamini wanafanya kazi kubwa sana, TANESCO tutakutana huko baadaye tukiwa mji. Ahsante.